SURA YA 98
Mitume Wabishana Tena Kuhusu Umashuhuri
MATHAYO 20:17-28 MARKO 10:32-45 LUKA 18:31-34
-
YESU ATABIRI TENA KUHUSU KIFO CHAKE
-
AWASHAURI MITUME KUHUSU TAMAA YAO YA KUJITAFUTIA UMASHUHURI
Yesu na mitume wake wanapomalizia safari yao ya kwenda kusini huko Perea wakielekea Yerusalemu, wanavuka Mto Yordani karibu na Yeriko. Kuna watu wengine wanaosafiri pamoja nao kwenda kwenye Pasaka ya mwaka wa 33 W.K.
Yesu anatembea akiwa amewatangulia wanafunzi wake kwa sababu ameazimia kutochelewa kufika jijini kwa ajili ya Pasaka. Lakini wanafunzi wanaogopa. Hapo awali, Lazaro alipokufa na Yesu alipokuwa karibu kuondoka Perea kwenda Yudea, Tomasi aliwaambia hivi wenzake: “Sisi pia, twendeni tukafe pamoja naye.” (Yohana 11:16, 47-53) Kwa hiyo, ni hatari kwenda Yerusalemu na inaeleweka kwamba wanafunzi wanaogopa.
Ili kuwatayarisha kwa ajili ya mambo yatakayotokea Yesu anawapeleka kando wanafunzi wake na kuwaambia: “Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa binadamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi. Nao watamhukumia kifo na kumtia mikononi mwa watu wa mataifa ili wamdhihaki, wampige mijeledi, na kumuua kwenye mti; na siku ya tatu atafufuliwa.”—Mathayo 20:18, 19.
Hii ni mara ya tatu ambayo Yesu anawaambia wanafunzi wake kwamba atakufa na kufufuliwa. (Mathayo 16:21; 17:22, 23) Hata hivyo, mara hii anawaambia kwamba atauawa kwenye mti. Wanamsikiliza lakini hawaelewi anachomaanisha. Labda wanatarajia kwamba ufalme wa Israeli utarudishwa hapa duniani, nao wanataka kufurahia utukufu na heshima pamoja na Kristo katika ufalme huo hapa duniani.
Salome, ambaye inaelekea ndiye mama ya mitume Yakobo na Yohana, yumo miongoni mwa wasafiri. Yesu aliwapa mitume hao wawili jina linalomaanisha “Wana wa Ngurumo,” kwa sababu walikuwa wenye hasira. (Marko 3:17; ) Kwa muda fulani, mitume hao wawili wamekuwa na tamaa ya kuwa mashuhuri katika Ufalme wa Kristo. Mama yao anajua jambo hilo. Sasa anamjia Yesu kwa niaba yao, anamsujudia na kumwomba amfanyie jambo fulani. Yesu anamuuliza: “Unataka nini?” Salome anamjibu: “Toa agizo kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja upande wako wa kuume na mwingine upande wako wa kushoto, katika Ufalme wako.”— Luka 9:54Mathayo 20:20, 21.
Kwa kweli, ombi hilo linatoka kwa Yakobo na Yohana. Kwa kuwa tayari Yesu ametaja kuhusu aibu na fedheha atakayopata, anawaambia: “Hamjui kile mnachoomba. Je, mnaweza kunywa kikombe ambacho niko karibu kukinywa?” Wanamjibu: “Tunaweza.” (Mathayo 20:22) Inaelekea bado hawaelewi kikamili jambo hilo linamaanisha nini kwao.
Hata hivyo, Yesu anawaambia hivi: “Kwa kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi upande wangu wa kuume na upande wangu wa kushoto si haki yangu kutoa, bali wataketi wale ambao Baba yangu amewatayarishia.”—Mathayo 20:23.
Wale mitume wengine kumi wanapojua kuhusu ombi la Yakobo na Yohana, wanakasirika. Je, huenda Yakobo na Yohana walisisitiza maoni yao mitume walipobishana hapo awali kuhusu aliye mkuu zaidi? (Luka 9:46-48) Vyovyote vile, ombi hilo linaonyesha kwamba wale 12 hawajatumia ushauri ambao Yesu aliwapa kuhusu kujiendesha kama aliye mdogo zaidi. Bado wana tamaa ya kuwa mashuhuri.
Yesu anaamua kushughulikia mabishano hayo na mzozo unaotokea. Anawaita wale 12 na kwa upendo anawapa ushauri huu: “Mnajua kwamba wale wanaotawala mataifa hupiga ubwana juu yao na wakuu wao hutumia mamlaka juu yao. Haipaswi kuwa hivyo kati yenu; lakini yeyote anayetaka kuwa mkubwa kati yenu lazima awe mhudumu wenu, na yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu lazima awe mtumwa wa wote.”—Marko 10:42-44.
Yesu anatoa mfano ambao wanapaswa kuiga, yaani, mfano wake. Anaeleza hivi: “Mwana wa binadamu [alikuja], si kuhudumiwa, bali kuhudumu na kutoa uhai wake uwe fidia badala ya wengi.” (Mathayo 20:28) Kwa miaka mitatu hivi, Yesu amekuwa akiwahudumia wengine. Naye ataendelea kufanya hivyo, hata atakufa kwa ajili ya wanadamu! Wanafunzi wanahitaji kuwa na mtazamo kama wa Kristo wa kutaka kuhudumu bali si kuhudumiwa, kuwa aliye mdogo zaidi badala ya kuwa mashuhuri.