Mwanzo 44:1-34
44 Baadaye Yosefu akamwamuru hivi msimamizi wa nyumba yake: “Ijaze mifuko ya watu hawa kiasi cha chakula wanachoweza kubeba, na uweke pesa za kila mmoja wao katika mdomo wa mfuko wake.+
2 Lakini kiweke kile kikombe changu, kikombe changu cha fedha, katika mdomo wa mfuko wa yule mdogo, pamoja na pesa zake za nafaka.” Basi akafanya kama Yosefu alivyoagiza.
3 Asubuhi kulipopambazuka, wanaume hao waliruhusiwa kuondoka pamoja na punda wao.
4 Kabla hawajafika mbali kutoka jijini, Yosefu akamwambia yule msimamizi wa nyumba yake: “Ondoka! Wafuatie haraka wanaume hao! Utakapowafikia, waulize, ‘Kwa nini mmelipa uovu kwa wema?
5 Je, hiki si kikombe anachotumia bwana wangu kunywea na kukitumia kusoma kwa ustadi ishara za ubashiri? Jambo mlilotenda ni ovu.’”
6 Basi msimamizi huyo akawafikia na kuwaambia maneno hayo.
7 Lakini wakamwambia: “Kwa nini bwana wetu unasema jambo kama hili? Sisi watumishi wako hatuwezi kamwe kuwazia kufanya jambo lolote kama hilo.
8 Kwa kweli, pesa tulizopata kwenye midomo ya mifuko yetu tulikurudishia kutoka katika nchi ya Kanaani.+ Basi tungewezaje kuiba fedha au dhahabu katika nyumba ya bwana wako?
9 Yeyote kati ya watumwa wako atakayepatikana nacho, na auawe, na sisi wengine tutakuwa pia watumwa wa bwana wako.”
10 Kwa hiyo akasema: “Na iwe kama mlivyosema: Yule atakayepatikana nacho atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine hamtakuwa na hatia.”
11 Basi kila mmoja akaushusha chini upesi mfuko wake na kuufungua.
12 Akaipekua mifuko hiyo kwa makini, akianza na mfuko wa yule mkubwa na kumalizia na mfuko wa yule mdogo. Hatimaye kikombe hicho kikapatikana katika mfuko wa Benjamini.+
13 Ndipo wakayararua mavazi yao, na kila mmoja akamtwika punda wake mfuko wake, wakarudi jijini.
14 Yuda+ na ndugu zake walipoingia katika nyumba ya Yosefu, bado alikuwemo; nao wakajiangusha chini mbele yake.+
15 Yosefu akawauliza: “Ni jambo gani hili mlilofanya? Je, hamkujua kwamba mtu kama mimi anaweza kusoma kwa ustadi ishara za ubashiri?”+
16 Yuda akamjibu: “Tukuambie nini bwana wetu? Tuseme nini? Tutathibitisha jinsi gani kwamba sisi ni waadilifu? Mungu wa kweli amefichua kosa letu sisi watumwa wako.+ Sasa sisi ni watumwa wako bwana wetu, sisi na yule aliyepatikana na kikombe hicho!”
17 Lakini akawaambia: “Siwezi kamwe kuwazia kufanya hivyo! Mtu aliyepatikana na kikombe hicho ndiye atakayekuwa mtumwa wangu.+ Lakini ninyi wengine, pandeni kwa amani mwende zenu kwa baba yenu.”
18 Sasa Yuda akamkaribia na kumwambia: “Nakusihi, bwana wangu, tafadhali niruhusu mimi mtumwa wako nikwambie neno moja bwana wangu, wala usinikasirikie mimi mtumwa wako, kwa maana wewe ni kama Farao.+
19 Bwana wangu ulituuliza sisi watumwa wako, ‘Je, mna baba au ndugu?’
20 Bwana wangu tukakuambia, ‘Tuna baba aliyezeeka na mtoto aliyemzaa uzeeni, yule mdogo.+ Lakini ndugu yake alikufa,+ kwa hiyo ndiye mwana pekee aliyebaki wa mama yake,+ na baba yake anampenda.’
21 Kisha ukatuambia sisi watumwa wako, ‘Mleteni huku chini ili nimwone.’+
22 Lakini bwana wangu tukakwambia, ‘Mvulana huyo hawezi kumwacha baba yake. Akimwacha, kwa hakika baba yake atakufa.’+
23 Kisha ukatuambia sisi watumwa wako, ‘Ndugu yenu mdogo asiposhuka huku pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.’+
24 “Basi tukapanda kwenda kwa mtumwa wako, baba yetu, na kumwambia maneno yako bwana wangu.
25 Baadaye baba yetu akatuambia, ‘Rudini huko mkatununulie chakula kidogo.’+
26 Lakini tukamwambia, ‘Hatuwezi kushuka huko. Tutashuka ikiwa ndugu yetu mdogo atakuwa pamoja nasi, kwa sababu hatuwezi kuuona uso wa mtu huyo ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi.’+
27 Kisha mtumwa wako baba yetu akatuambia, ‘Mnajua vizuri kwamba mke wangu alinizalia wana wawili tu.+
28 Lakini mmoja wao aliniacha, nikasema: “Kwa hakika mnyama wa mwituni amemrarua vipandevipande!”+ nami sijamwona mpaka sasa.
29 Mkimchukua huyu pia nisimwone, kisha apatwe na madhara na kufa, hakika mtazishusha mvi zangu Kaburini*+ kwa msiba.’+
30 “Na sasa nikirudi bila mvulana huyu kwa mtumwa wako baba yangu, kwa kuwa uhai wake umefungamana na uhai wa* mvulana huyu,
31 basi mara tu atakapoona mvulana huyu hayupo, atakufa, na kwa kweli sisi watumwa wako tutazishusha mvi za mtumwa wako baba yetu Kaburini* kwa huzuni.
32 Mimi mtumwa wako nilijitoa kuwa dhamana kwa baba yangu kwa ajili ya mvulana huyu, kwa kumwambia, ‘Nisipomrudisha kwako, nitakuwa nimekutendea dhambi milele baba yangu.’+
33 Basi sasa tafadhali, acha niwe mtumwa wako bwana wangu badala ya mvulana huyu, ili arudi pamoja na ndugu zake.
34 Nitarudije kwa baba yangu bila mvulana huyu? Siwezi kustahimili kuona msiba huo ukimpata baba yangu!”
Maelezo ya Chini
^ Au “nafsi yake imefungamana na nafsi ya.”