Awamu ya 5 ya Picha za Warwick (Septemba 2015 Hadi Februari 2016)
Katika mfululizo huu wa picha, ona maendeleo yaliyofanywa kwenye ujenzi wa makao makuu mapya ya Mashahidi wa Yehova na jinsi wajitoleaji walivyosaidia katika kazi hiyo ya ujenzi kuanzia mwezi wa Septemba 2015 hadi Februari 2016
Oktoba 7, 2015—Eneo la ujenzi la Warwick
Tao la daraja likipelekwa kwenye msingi wa daraja. Tao hilo liliposhushwa kwa mara ya kwanza kutoka kwenye lori, lilisimamishwa juu ya magurudumu. Daraja hilo linalinda mazingira ya eneo lenye majimaji.
Oktoba 13, 2015—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali
Paa la jengo lililotandazwa aina ya mimea inayoitwa sedum. Mimea hiyo hubadilika rangi kisha inaacha kukua wakati wa majira ya baridi kali. Aina kumi na sita za mmea wa sedum zimepandwa katika paa za majengo mbalimbali. Mimea hiyo iliyopandwa juu ya paa husaidia kulinda mazingira kwa kudhibiti maji ya mvua, hupunguza gharama za matumizi ya nishati na yanatunzwa kwa kuondoa tu magugu.
Oktoba 13, 2015—Jengo la Makazi D
Fundi seremala akishughulikia kabati za jikoni katika chumba kimoja cha makazi. Kufikia Februari 2016, Idara ya Useremala ilikuwa imeweka zaidi ya asilimia 60 ya makabati yote yanayohitajika.
Oktoba 16, 2015—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali
Fundi umeme wakifunga taa (LED) zitakazomulika ishara ya Mnara wa Mlinzi iliyowekwa kwenye jengo lililo na mnara.
Oktoba 21, 2015—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali
Taa zikiwa zimewashwa usiku kwenye Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali lililo na mnara na eneo la mapokezi. Mnara huo utawawezesha wageni kuona mandhari ya pekee ya eneo la Warwick na mazingira yake.
Oktoba 22, 2015—Eneo la ujenzi la Warwick
Wajenzi wakiandaa barabara kwa ajili ya magari ya dharura, kwa kuweka msingi kisha kumwaga zege. Sehemu ya pembeni ya barabara imefunikwa na kitambaa cha katani kuzuia mmomonyoko wa ardhi wakati wa ujenzi.
Novemba 9, 2015—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali
Wafanyakazi wakiweka dirisha la kupitisha mwangaza wa asili lililo juu ya lifti ya eneo la mapokezi. Madirisha kumi na moja ya aina hiyo yamewekwa katika Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali kuruhusu mwangaza wa asili uingie ndani ya jengo hilo.
Novemba 16, 2015—Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji
Fundi akikata bomba la chuma kwa kutumia mashine. Mabomba hayo yatatumiwa kutengeneza mfumo wa kupooza hewa unaotumia maji baridi.
Novemba 30, 2015—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali
Fundi seremala akiandaa sehemu za kuwekea fremu za madirisha. Baada ya sehemu hizo kuwa tayari na kuta kumalizwa, fremu za madirisha zitawekwa.
Desemba 17, 2015—Eneo la ujenzi la Warwick
Matofali madogo yakipangwa barabarani huku mvua ikinyesha. Sehemu ya katikati ya picha upande wa kulia, inaonyesha kifaa kirefu cheupe kinachosawazisha changarawe. Kwa mbele, tunaona gari likinyanyua matofali na kuyaweka mahali pake. Upande wa kushoto, kitambaa cha plastiki kimefunika udongo kuzuia mmomonyoko.
Desemba 24, 2015—Eneo la ujenzi la Warwick
Wafanyakazi wakivuta nyaya kwenda kwenye kituo kidogo cha umeme, kinachotoa umeme kwa eneo la ujenzi la Warwick.
Januari 5, 2016—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali
Mfanyakazi akimalizia kutengeneza fremu kwa ajili ya njia iliyofunikwa itakayokuwa kati ya jengo la Maegesho ya Magari ya Wageni na la Ofisi na Huduma Mbalimbali. Njia hiyo iliyofunikwa itawalinda wageni dhidi ya mvua na theluji.
Januari 5, 2016—Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji
Fundi akirekebisha kifaa kinachoendesha matangi ya kuchemsha maji. Matangi yote manne ya kuchemsha maji katika eneo la ujenzi la Warwick tayari yanafanya kazi.
Februari 8, 2016—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali
Mafundi wakiweka mashine za kukausha nguo kwenye Idara ya Dobi. Mashine hizo zina uwezo kwa kukausha nguo zenye uzito wa kati ya kilogramu 6 hadi 45. Mashine za kufua zitawekwa ukutani upande wa kushoto.
Februari 8, 2016—Eneo la Tuxedo
Gerrit Lösch, mshiriki wa Baraza Linaloongoza, akiongoza Funzo la Mnara wa Mlinzi la familia ya Betheli. Programu hiyo hurushwa katika maeneo mengine ambapo wafanyakazi wa Warwick wanaishi.
Februari 19, 2016—Jengo la Makazi A
Wafanyakazi wa Idara inayoshughulikia ukamilishaji wa ndani wa majengo wakibeba zulia kwa ajili ya jengo mojawapo la makazi. Zaidi ya mita za mraba 65,000 za mazulia ziliagizwa kwa ajili ya majengo ya Warwick.
Februari 22, 2016—Eneo la ujenzi la Warwick
Kati ya mwezi wa Septemba 2015 na wa Februari 2016, vibali vya kuishi katika Majengo ya Makazi C na D vilipatikana, na hivyo baadhi ya wafanyakazi wakahamia humo. Lifti za majengo yote zilikuwa zimewekwa. Ujenzi wa barabara ya Residence Drive, kutia ndani kuwekwa kwa matofali yake madogo, ulikamilika. Kwa sababu majira ya baridi hayakuwa makali, maeneo ya bustani yalianza kutengenezwa mbele ya ratiba.
Februari 24, 2016—Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji
Mshiriki wa kikosi cha kutengeneza dari akitembea kwa kutumia magongo ili kuweka mihimili ya dari. Idara ya Kuta na Dari inashughulikia utengenezaji wa fremu, uwekaji wa mifumo ya kutunza joto, kupandisha na kukamilisha kuta na kupiga plasta, kutia ndani mifumo ya kuzuia moto kusambaa kwenye kuta.