Hamia kwenye habari

Awamu ya 7 ya Picha za Warwick (Septemba 2016 —Februari 2017)

Awamu ya 7 ya Picha za Warwick (Septemba 2016 —Februari 2017)

Katika mfululizo huu wa picha, ona jinsi kazi katika makao makuu mapya ya Mashahidi wa Yehova ilivyokamilika na jinsi wajitoleaji walivyoanza kuyatumia majengo hayo kati ya Septemba 2016 na Februari 2017.

Picha ya majengo ya Warwick. Kuanzia kushoto juu kwenda kulia:

  1. Jengo la Gereji

  2. Jengo la Maegesho ya Magari ya Wageni

  3. Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji

  4. Jengo la Makazi B

  5. Jengo la Makazi D

  6. Jengo la Makazi C

  7. Jengo la Makazi A

  8. Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Septemba 8, 2016​—eneo la Warwick

Majengo yote katika eneo la Warwick sasa yanatumika. Mwanzoni mwa Septemba, watu 500 hivi walikuwa wakiishi huko Warwick. Idadi hiyo ilitia ndani wajitoleaji wa ujenzi na watumishi wa wakati wote waliohamia kutoka Brooklyn.

Septemba 20, 2016​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Mchoraji akikagua vigae vilivyotumiwa katika kuta za mwingilio za maonyesho “Watu kwa Ajili ya Jina la Yehova.” Vigae hivyo vilitayarishwa ili vionyeshe hali ya kizamani ili kutimiza kusudi la maonyesho hayo ya kihistoria.

Septemba 28, 2016​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Stephen Lett, mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova, alikuwa mwenyekiti wa programu ya kwanza ya Ibada ya Familia iliyofanyiwa Warwick. Asubuhi hiyo, Ndugu Lett alisoma barua ya kuwashukuru wajitoleaji zaidi ya 27,000 waliosaidia ujenzi wa makao hayo mapya na wengine wengi waliotegemeza mradi huo kwa njia mbalimbali.

Oktoba 3, 2016​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Seremala apanga herufi za mwingilio kwa ajili ya mojawapo ya maonyesho matatu. Maonyesho yenye kichwa, “Watu kwa Ajili ya Jina la Yehova,” yanaonyesha historia ya kisasa ya Mashahidi wa Yehova kuanzia miaka ya 1870 hadi sasa.

Oktoba 5, 2016​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Halmashauri ya Uandikaji inakutana na wasaidizi wake na washiriki wa Idara ya Uandikaji. Skrini kubwa zinaonyesha picha zilizopendekezwa kwa ajili ya machapisho ya wakati ujao na kuruhusu idara mbalimbali katika maeneo mengine kuwasiliana na halmashauri hiyo wakati wa mikutano. Meza ambayo ilitolewa kama mchango miaka kadhaa iliyopita ilihamishwa kutoka Brooklyn hadi Warwick.

Oktoba 20, 2016​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Msaidizi wa Halmashauri ya Waratibu, pamoja na wengine wanaofanya kazi chini ya mwongozo wa halmashauri hiyo, wanazungumzia njia za kuwasaidia walioathiriwa na Kimbunga Haima (Lawin), kilichokuwa kimepiga nchi ya Filipino siku moja kabla. Vifaa vinavyowezesha kuwasiliana kwa njia ya video vinasaidia idara za makao makuu kushughulikia mambo haraka na kuwasiliana na ofisi za tawi ulimwenguni pote.

Oktoba 28, 2016​—Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji

Kidimbwi kinatenganisha Jengo la Udumishaji na barabara kuu. Kidimbwi hicho na vingine vilivyopo kwenye eneo la Warwick vinatumia mbinu za asili kukusanya na kuchuja uchafu kutoka katika maji ya mvua na hivyo kuokoa asilimia 50 ya gharama za kuweka mfumo wa kawaida wa kuruhusu maji yapite. Pia, maji hayo yaliyosafishwa na kuchujwa yanaingia kwenye vijito vya maji na kuandaa mazingira yanayofaa mimea na wanyama.

Novemba 4, 2016​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Kikosi cha kuhamisha kinapakua bidhaa. Wafanyakazi 80 hivi waliwasaidia ndugu kuhama kutoka Brooklyn hadi makao yao mapya Warwick.

Desemba 14, 2016​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Waokaji wanavingirisha donge kubwa la unga. Kwa kuwa donge kama hilo linaweza kuwa na uzito wa zaidi ya kilo 45, kifaa cha kuliinua kinafanya kazi iwe rahisi na salama zaidi. Eneo la kuokea la Warwick pia lina kifaa kinachoweza kutumiwa kuharakisha hatua za kuchachisha donge kwa kudhibiti kiwango cha joto na unyevu. Kifaa hicho kinapunguza idadi ya watu wanaohitajika kuoka mikate mingi kila juma.

Desemba 14, 2016​—Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji

Wafanyakazi wanatoa takataka katika Jengo la Udumishaji. Tofauti na ilivyokuwa Brooklyn, majengo mengi Warwick yameunganishwa, hivyo wafanyakazi na magari mengi hayahitajiwi ili kuzoa taka na vitu vinavyoweza kutumiwa tena.

Desemba 14, 2016​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Blauzi inanyunyiziwa maji kupunguza makunyanzi na kupigwa pasi kutumia kifaa. Kwa kawaida, Idara ya Dobi iliyoko Warwick inasafisha kilo 5,000 za nguo na matandiko kila juma. Ili kutambua nguo, wale wanaofanya kazi dobi wanazitia alama. Alama hizo zinakaguliwa mara kadhaa huko dobi ili kuhakikisha kwamba nguo zote zimeshughulikiwa ifaavyo na kupelekwa kwenye idara au chumba kinachofaa.

Desemba 20, 2016​—Jengo la Udumishaji na Maegesho ya Wenyeji

Fundi wa magari akikagua na kudumisha kifaa fulani. Kufanya hivyo kunafanya vifaa vidumu kwa muda mrefu na kuhakikisha usalama wa wanaovitumia.

Januari 10, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Ndugu akishughulikia mfumo wa kompyuta unaoonyesha maonyesho ya “Imani Yenye Matendo”.

Januari 11, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Mafundi seremala wanaandaa baiskeli iliyotengenezwa mwaka wa 1903, kwa ajili ya maonyesho “Watu kwa Ajili ya Jina la Yehova.” Baiskeli iliyotolewa ikiwa mchango ilirekebishwa na wafanyakazi wa Warwick na inatumiwa kuonyesha jitihada na kujidhabihu kwa Wanafunzi wa Biblia (baadaye wameitwa Mashahidi wa Yehova) ambao walitumia usafiri kama huo walipoeneza ujumbe wa Biblia.

Januari 12, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Mafundi seremala wakiweka kioo ambacho kitafunika eneo lenye vitu vinavyohusiana na “Photo-Drama of Creation,” sinema ya Biblia na picha iliyotolewa mwaka wa 1914. Watu milioni tisa hivi waliitazama mwaka huo.

Januari 12, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Wachoraji na wanaohifadhi vitu vya kale wakirekebisha toleo la 1544 la Biblia ya Kilatini ya Zurich kwa ajili ya maonyesho “Biblia na Jina la Mungu.” Alama nyekundu inayoonekana katika Biblia inaonyesha jina la kibinafsi la Mungu, Yehova. Watu wanaohifadhi vitu vya kale wanachukua tahadhari ili kuhifadhi Biblia hizo za zamani. Kwa mfano, kurasa zimeshikiliwa na aina fulani ya karatasi, joto na unyevu unadhibitiwa katika chumba hicho, na wanahakikisha kwamba taa zinazotumiwa hazitaharibu karatasi hizo.

Januari 16, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Wageni wanaotembezwa wanaona eneo la kupendeza la Warwick kutoka mnara wenye urefu wa mita 23. Watu walioomba mapema walianza kutembelea maonyesho hayo na majengo ya Warwick Aprili 3, 2017. Wale wanaotaka kutembelea eneo hilo lazima waombe mapema kupitia mfumo ulio kwenye mtandao katika sehemu ya KUTUHUSU > OFISI NA MATEMBEZI.

Januari 19, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Mtu anayehifadhi vitu vya kale akiweka toleo la kwanza lisilopatikana kwa urahisi la King James Version mahali pake. Sehemu za kuweka vitu vya kale zilibuniwa na kutengenezwa na ndugu hapo Warwick.

Januari 19, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Mchoraji akiweka kofia mahali pake. Kofia hiyo ilikuwa ya Joseph F. Rutherford, ambaye alianza kusimamia kazi ya kuhubiri ya Mashahidi wa Yehova miaka mia moja iliyopita. Sehemu hiyo ambayo ni sehemu ya maonyesho “Watu kwa Ajili ya Jina la Yehova,” inaonyesha jitihada za Mashahidi wa mapema za kuhubiri habari njema za Ufalme.

Januari 20, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Akisaidiwa na timu ya kurekodi, msomaji anasimulia maonyesho ya “Biblia na Jina la Mungu.” Juma moja hivi baada ya kuhamisha vifaa na chumba cha kurekodia kutoka Brooklyn hadi Warwick, studio ilianza kufanya kazi tena. Studio hii (sehemu ya studio kubwa zilizo Kituo cha Elimu cha Watchtower kilichoko Patterson) inatumiwa pia kurekodi Tafsiri ya Ulimwengu Mpya, Mnara wa Mlinzi na Amkeni!, makala za jw.org, na vitabu vingine.

Januari 27, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Msaidizi wa fundi seremala akipaka rangi. Sehemu hiyo ni sehemu ya maonyesho “Watu kwa Ajili ya Jina la Yehova,” na yenye picha za Wanafunzi wa Biblia wa karne ya 19.

Februari 15, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Mchoraji akipaka rangi mchoro wa Caleb anayetumiwa katika mfululizo wa vibonzo vyenye kichwa Uwe Rafiki ya Yehova. Mchoro huo utaonekana katika sehemu inayoonyesha vifaa na programu ambazo Mashahidi wa Yehova wamebuni hasa kwa ajili ya watoto.

Februari 15, 2017​—Jengo la Ofisi na Huduma Mbalimbali

Seremala akikata picha na mabango kwa ajili ya maonyesho “Watu kwa Ajili ya Jina la Yehova.” Watu zaidi ya 250 walifanya kazi kutayarisha maonyesho hayo matatu tangu mwanzo hadi mwisho. Walitia ndani mafundi seremala, watu wanaotengeneza programu za kompyuta, wabunifu wa michoro, mafundi umeme, mafundi wa kuweka vigae, wapiga video, na waandishi.