Kurasa Chache Zaidi, Lugha Nyingi Zaidi
Kuanzia Januari 2013, gazeti Amkeni! na toleo la watu wote la gazeti Mnara wa Mlinzi yatapunguzwa kutoka kurasa 32 mpaka kurasa 16 kwa toleo.
Kwa sababu magazeti hayo yatakuwa na kurasa chache, vikundi wa kutafsiri vitaweza kuyatafsiri katika lugha nyingi zaidi. Kwa mfano, gazeti la Amkeni! la Desemba 2012 lilitafsiriwa katika lugha 84, na gazeti la Mnara wa Mlinzi la Desemba 2012 katika lugha 195. Hata hivyo, kuanzia Januari 2013, gazeti Amkeni! linatafsiriwa katika lugha 98, na Mnara wa Mlinzi katika lugha 204.
Toleo la funzo la Mnara wa Mlinzi litaendelea kuwa na kurasa 32.
Kurasa Chache Zaidi Kuchapwa—Kurasa Nyingi Zaidi Kwenye Intaneti
Kwa kuwa magazeti yatakuwa na kurasa chache, jambo hilo litaathiri habari tunayoweka katika tovuti yetu ya www.jw.org katika njia mbili.
Baadhi ya habari ambazo awali zilichapishwa kwenye magazeti zitapatikana tu kwenye tovuti hiyo. Kwa mfano, makala “Kwa Ajili ya Vijana,” “Masomo Yangu ya Biblia” na ripoti ya kuhitimu kwa madarasa ya Gileadi kutoka katika gazeti la Mnara wa Mlinzi toleo la watu wote pamoja na “Mazungumzo ya Familia” na “Vijana Huuliza” kutoka katika gazeti la Amkeni! zitapatikana tu kwenye tovuti yetu.
Mnara wa Mlinzi na Amkeni! yatapatikana katika miundo zaidi ya kielektroniki. Kwa miaka kadhaa, magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Amkeni! yamepatikana kwenye tovuti ya www.jw.org yakiwa katika muundo wa PDF. Sasa magazeti haya yatapatikana katika muundo wa HTML, kwa hiyo itakuwa rahisi zaidi kuyapata na kuyasoma moja kwa moja kutoka kwenye kompyuta au simu ya mkononi. Pia utaweza kupata kwa urahisi machapisho yetu mengine kwenye tovuti yetu katika lugha 400 hivi.