SEHEMU YA 1
Je, Maisha Yenye Kuridhisha Ni Ndoto?
KATIKA nchi ambayo imesitawi, nyumba yenye vitu vya starehe inaweza kuonekana kuwa yenye ufanisi. Lakini unapotembelea nyumba hiyo utakuta hali gani? Hali ngumu isiyo na furaha. Utapata vijana wakiwa wamenuna wakiwajibu wazazi wao tu “Ndiyo,” au “La.” Mama anatamani mume wake amjali. Naye baba hataki kusumbuliwa. Wazazi waliozeeka wa familia hiyo ambao wanaishi kwingine wanatamani kuwaona, kwani hawajawaona kwa miezi kadhaa. Kwa upande mwingine, kuna familia zenye mikazo kama hiyo ambazo zimeweza kusuluhisha matatizo yao na ambazo kwa kweli zina furaha. Je, unajua sababu?
2 Hebu fikiria familia fulani katika nchi inayositawi, labda katika sehemu nyingine ya ulimwengu. Familia hiyo ya watu saba inaishi katika nyumba mbovu inayoweza kuanguka wakati wowote. Hawajui watapata lini mlo mwingine—kikumbusha chenye kusikitisha kwamba mwanadamu bado hajaweza kuondoa njaa na umaskini ulimwenguni. Hata hivyo, kuna familia nyingi duniani ambazo ni maskini lakini zina furaha. Kwa nini?
3 Hata katika nchi tajiri, matatizo ya kifedha yanaweza kutokea. Familia moja nchini Japani ilinunua nyumba uchumi ulipokuwa mzuri kabisa. Wakiwa na hakika kwamba wataongezewa mshahara, walinunua nyumba kwa deni kubwa. Lakini uchumi ulipoharibika walishindwa kulipa deni la nyumba hiyo na wakalazimika kuiuza kwa bei ya chini sana kuliko walivyoinunua. Ingawa sasa familia hiyo haiishi katika ile nyumba, bado wanalipa deni hilo. Isitoshe pia, wanang’ang’ana kulipa madeni yaliyotokana na kutumia vibaya kadi za mkopo. Baba anacheza kamari ya mbio za farasi, na familia inazidi kudidimia kwenye madeni. Lakini familia nyingi zimefanya marekebisho ambayo yamefanya wapate furaha. Je, ungependa kujua wameipataje?
4 Hata uwe unaishi wapi, mahusiano kati ya wanadamu yanaweza kusababisha mikazo na kufanya usifurahie maisha. Huenda ukasengenywa kazini. Mambo
ambayo umetimiza yanaweza kuwafanya wengine wakuonee wivu na kufanya uchambuliwe. Huenda mtu ambaye unashughulika naye kila siku anakuudhi kwa sababu anasisitiza sana maoni yake. Labda mtoto wako ananyanyaswa, anadhulumiwa au kupuuzwa shuleni. Ikiwa wewe ni mzazi asiye na mwenzi wa ndoa, unajua kwamba hali hiyo inaongeza mzigo wa matatizo yako maishani. Matatizo hayo yote yanawazidishia mikazo wanaume na wanawake wengi leo.5 Bila kujua, athari za mikazo zinaweza kuongezeka polepole kwa muda fulani mpaka mtu alemewe kabisa. Hiyo ndiyo sababu mkazo umeitwa muuaji wa kimyakimya, na mkazo wa daima kuitwa sumu inayoua polepole. “Leo, mkazo na magonjwa yanayosababishwa na mkazo yanaathiri wafanyakazi karibu ulimwenguni kote,” ndivyo anavyosema Profesa Robert L. Veninga wa Chuo Kikuu cha Minnesota. Inasemekana kwamba magonjwa yanayoletwa na mkazo yanagharimu Marekani dola bilioni 200 kila mwaka. Mkazo umetoka Marekani na kuenea hata katika nchi nyinginezo, na maneno yanayorejelea “mkazo” yanapatikana katika lugha nyingi kubwa ulimwenguni. Ikiwa una mkazo na unashindwa kutimiza mambo uliyotaka kufanya, huenda ukaanza kuhisi hatia. Uchunguzi mmoja uliofanywa karibuni unaonyesha kwamba mtu wa kawaida hujiona ana hatia kwa muda wa saa mbili kila siku. Lakini, wengine wameweza kukabili mkazo na kufaulu maishani.
6 Unawezaje kukabiliana na matatizo hayo ya kila siku na bado uishi maisha yenye kuridhisha? Wengine husoma vitabu vyenye ushauri mbalimbali na maagizo ya wataalamu. Je, vitabu hivyo vinategemeka? Dakt. Benjamin Spock, ambaye kitabu chake kuhusu kulea watoto kimetafsiriwa katika lugha 42 na ambacho nakala milioni 50 hivi zimeuzwa, alisema kwamba “kutokuwa thabiti . . . ndilo tatizo la kawaida zaidi la wazazi nchini Marekani leo.” Kisha akasema kwamba wataalamu, kutia ndani yeye mwenyewe, ndio wenye kulaumika sana. “Hatukutambua jambo hilo mpaka ikawa kuchelewa mno,” akasema, “mtazamo wetu kwamba tunajua mambo yote unafanya wazazi wasiwe na uhakika.” Basi, huenda tukajiuliza: ‘Tunaweza kufuata ushauri wa nani ili tuishi maisha yenye kuridhisha leo na wakati ujao?’