HADITHI YA 85
Yesu Anazaliwa Katika Boma la Ng’ombe
UNAJUA mtoto mdogo huyu ni nani? Ni Yesu. Amezaliwa sasa hivi katika boma la ng’ombe. Mariamu anamlaza katika chombo cha kuwekea chakula cha punda na wanyama wengine. Lakini kwa nini Mariamu na Yusufu wako humu pamoja na wanyama? Hapa si mahali pa kuzalia mtoto, sivyo?
Sivyo. Lakini sababu ni hii: Kaisari Augusto, mtawala wa Roma alitunga sheria ili kila mtu arudie mji alikozaliwa, jina lake likaandikwe katika kitabu. Yusufu alizaliwa humu Bethlehemu. Lakini yeye na Mariamu walipofika, nafasi haikupatikana popote. Basi ikawapasa wawe humu pamoja na wanyama. Na siku iyo hiyo Mariamu akazaa Yesu! Lakini mtoto yuko salama, kama unavyoona.
Unaona wachungaji wakija kumwona Yesu? Walikuwa mashambani usiku wakichunga kondoo zao, na mwangaza mwingi uling’aa pande zao zote. Kumbe ni malaika! Wachungaji hao waliogopa sana. Lakini malaika huyo akawaambia: “Msiogope! Nimewaletea habari njema. Leo huko Bethlehemu, Kristo Bwana amezaliwa. Ataokoa watu! Mtamwona amefungwa vitambaa na kulazwa katika hori.’ Mara wakaja malaika wengi wakaanza kumsifu Mungu. Basi mara hiyo wachungaji hao wakafanya haraka kumtafuta Yesu, na sasa wamempata.
Unajua sababu Yesu ni mtoto wa pekee sana? Unajua ni nani hasa? Kumbuka, katika hadithi ya kwanza ya kitabu hiki tulisimulia habari ya Mwana wa Mungu wa kwanza. Mwana huyo alifanya kazi pamoja na Yehova katika kuumba mbingu na dunia na kila kitu kingine. Basi, huyo ndiye Yesu!
Yehova alihamisha uhai wa Mwanawe mbinguni akautia ndani ya Mariamu. Mara hiyo mtoto mchanga akaanza kukua tumboni mwake kama watoto wengine. Lakini mtoto huyo alikuwa Mwana wa Mungu. Mwishowe Yesu akazaliwa humu katika boma la ng’ombe katika Bethlehemu. Unajua sasa kwa nini malaika walifurahia sana kuwaambia watu kwamba Yesu amezaliwa?