HADITHI YA 74
Mwanamume Asiyeogopa
WATAZAME watu hawa wakimcheka kijana huyu. Unajua ni nani? Ni Yeremia. Ni nabii wa maana sana wa Mungu.
Mfalme Yosia akiisha anza kuziharibu sanamu katika nchi, Yehova anamwambia Yeremia awe nabii Wake. Lakini, Yeremia anajiona kuwa mtoto mno kuwa nabii. Lakini Yehova anasema atamsaidia.
Yeremia anawaambia Waisraeli waache kutenda mabaya. ‘Miungu ambayo mataifa wanaabudu ni ya uongo,’ anasema. Lakini Waisraeli wengi wanapenda kuabudu sanamu kuliko kumwabudu Mungu wa kweli Yehova. Yeremia anapowaambia watu kwamba Mungu atawaadhibu kwa ubaya wao, wanamcheka tu.
Miaka yapita. Yosia anakufa, na miezi mitatu baadaye mwanawe Yehoyakimu (Yoyakimu) anakuwa mfalme. Yeremia azidi kuwaambia watu hivi: ‘Yerusalemu utaharibiwa msipobadili njia zenu mbaya.’ Makuhani wanamkamata Yeremia na kupiga kelele hivi: ‘Unapaswa kuuawa kwa kusema hayo.’ Halafu wanawaambia wakuu wa Israeli hivi: ‘Yeremia anapaswa kuuawa, kwa sababu amesema mabaya juu ya mji wetu.’
Sasa Yeremia atafanya nini? Haogopi! Anawaambia wote hivi: ‘Yehova alinituma niwaambie mambo hayo. Msipobadili maisha yenu mabaya, Yehova atauharibu Yerusalemu. Lakini hakikisheni hili: Mkiniua, mtaua mtu asiye na kosa.’
Wakuu hao wanamwacha Yeremia aishi, lakini Waisraeli hawabadili njia zao mbaya. Baadaye Nebukadreza, mfalme wa Babeli, aja kuupiga Yerusalemu. Mwishowe Nebukadreza anawafanya Waisraeli kuwa watumwa wake. Anawachukua maelfu mengi Babeli. Ebu wazia ingekuwaje kama wageni wangekupeleka kwenye nchi usiyojua!