HADITHI YA 28
Namna Mtoto Musa Alivyookolewa
TAZAMA mtoto mchanga analia, akakikamata kidole cha mama yule. Huyu ni Musa. Unajua mama huyo mzuri ni nani? Ni binti mfalme wa Misri, binti ya Farao mwenyewe.
Mama ya Musa alimficha mtoto wake mpaka alipokuwa mwenye umri wa miezi mitatu, kwa sababu hakutaka auawe na Wamisri. Lakini alijua kwamba huenda Musa akaonekana, basi akafanya hivyo ili amwokoe.
Alichukua kikapu akakitengeneza ili maji yasiingie ndani. Kisha akamweka Musa ndani yake, akakiweka kikapu hicho katika majani marefu kando ya Mto Nailo. Miriamu, dada yake Musa aliambiwa asimame karibu aone itakavyokuwa.
Upesi binti Farao akaja kwenye Mto Nailo aoge. Mara moja akaona kikapu katika majani marefu. Akamwita mtumishi wake mmoja, akamwambia: ‘Kaniletee kikapu kile.’ Binti mfalme alipofungua kikapu hicho, lo! aliona mtoto mzuri kama nini! Mtoto Musa alikuwa akilia, naye binti mfalme akamhurumia. Hakutaka amruhusu auawe.
Miriamu akaja. Unaweza kumwona katika picha hii. Miriamu akamwuliza binti Farao hivi: ‘Niende nikamwite mwanamke Mwisraeli akulelee mtoto huyu?’
‘Nenda tafadhali,’ akasema binti mfalme.
Basi Miriamu akakimbia haraka kwenda kumwambia mama yake. Mama ya Musa alipokuja kwa binti mfalme, binti mfalme akasema: ‘Mchukue mtoto huyu unilelee, nami nitakulipa.’
Basi mama ya Musa akalea mtoto wake mwenyewe. Baadaye Musa alipokuwa mkubwa kidogo, mama yake alimpeleka kwa binti Farao, aliyemlea kama mwanawe mwenyewe. Hivyo ndivyo Musa alivyokua katika nyumba ya Farao.