SOMO LA 38
Yehova Alimfanya Samsoni Awe na Nguvu
Wengi kati ya Waisraeli walianza tena kuabudu miungu ya uwongo, hivyo, Yehova akaruhusu watawaliwe na Wafilisti. Hata hivyo, kulikuwa na baadhi ya Waisraeli ambao walimpenda Yehova. Mmoja wao aliitwa Manoa. Yeye na mke wake hawakuwa na watoto. Siku moja, Yehova alimtuma malaika kwa mke wa Manoa. Malaika alimwambia hivi: ‘Utazaa mwana. Atawakomboa Waisraeli kutoka kwa Wafilisti. Naye atakuwa Mnadhiri.’ Je, unajua Wanadhiri walikuwa nani? Walikuwa watumishi wa pekee wa Yehova. Wanadhiri hawakuruhusiwa kunyoa nywele.
Baada ya muda, walipata mtoto nao wakamwita Samsoni. Alipokuwa mtu mzima, Yehova alimfanya kuwa mwenye nguvu nyingi. Samsoni angeweza kuua simba kwa mikono yake tu. Wakati fulani, Samsoni aliua Wafilisti 30 akiwa peke yake. Wafilisti walimchukia na walitafuta njia za kumuua. Usiku mmoja, Samsoni alipokuwa amelala huko Gaza, Wafilisti walimsubiri kwenye lango la jiji ili itakapofika asubuhi wamkamate na kumuua. Hata hivyo, katikati ya usiku, Samsoni aliamka, akaenda kwenye lango la jiji na kuling’oa. Kisha, akalibeba lango hilo mabegani mwake mpaka kwenye kilele cha mlima ulio karibu na Hebroni!
Baadaye, Wafilisti walimwendea Delila, mchumba wa Samsoni, na kumwambia: ‘Tutakupa maelfu ya vipande vya fedha ukituambia siri ya nguvu za Samsoni. Tunataka kumkamata na kumfunga gerezani.’ Delila alikubali kwa sababu alitaka pesa. Mwanzoni, Samsoni alikataa kumwambia chanzo cha nguvu zake. Hata hivyo, Delila aliendelea kumsumbua hadi akamfunulia siri ya nguvu zake. Alimwambia hivi: ‘Sijawahi kunyolewa nywele, kwa kuwa mimi ni Mnadhiri. Nikinyolewa tu, sitakuwa na nguvu tena.’ Samsoni alikosea sana kumfunulia siri yake, sivyo?
Mara moja, Delila akawaambia Wafilisti: ‘Ninajua siri yake!’ Akamlaza Samsoni katika paja lake, halafu akamwita mtu amnyoe nywele. Kisha, Delila akasema kwa sauti kubwa: ‘Samsoni, Wafilisti wamekuja!’ Samsoni akaamka, lakini hakuwa na nguvu. Wafilisti wakamkamata, wakamng’oa macho na kumfunga gerezani.
Siku moja, maelfu ya Wafilisti walikusanyika katika hekalu la mungu wao Dagoni wakishangilia na kusema, ‘mungu wetu amemtia Samsoni mikononi mwetu! Mleteni Samsoni nje ili atutumbuize.’ Wakamsimamisha katikati ya nguzo mbili na kuanza kumdhihaki. Samsoni akasali hivi: ‘Ee Yehova, tafadhali nitie nguvu, mara hii moja tu.’ Wakati huo, nywele za Samsoni zilikuwa zimekua tena. Samsoni akasukuma nguzo za hekalu kwa nguvu zake zote. Jengo lote likaanguka na kuwaua watu wote waliokuwemo kutia ndani Samsoni.
“Kwa mambo yote nina nguvu kupitia yule anayenipa nguvu.”—Wafilipi 4:13