Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

MATUKIO MUHIMU YA MWAKA ULIOPITA

Ujenzi wa Majumba ya Ufalme Waharakishwa

Ujenzi wa Majumba ya Ufalme Waharakishwa

INASISIMUA sana kuona jinsi ambavyo Yehova anaharakisha ukuzi wa ibada ya kweli ulimwenguni pote. (Isa. 60:22) Hivyo, kumekuwa na uhitaji mkubwa unaongezeka wa Majumba ya Ufalme. Ulimwenguni pote, Majumba ya Ufalme zaidi ya 13,000 yanahitaji kujengwa au kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Ili kujenga haraka na kwa gharama ndogo, Baraza Linaloongoza limefanya mabadiliko katika idara mbalimbali za ujenzi. Hivi karibuni, idara inayoitwa Idara ya Ulimwenguni Pote ya Usanifu-Majengo na Ujenzi (WDC) iliyo katika makao makuu huko Brooklyn, New York, ilianzishwa ili kushughulikia na kuharakisha miradi ya ujenzi na ukarabati ulimwenguni pote. Idara za Mkoa za Usanifu-Majengo na Ujenzi zilizoko katika ofisi ya tawi ya Afrika Kusini, Australia, Marekani, na Ujerumani huratibu ujenzi katika maeneo yao, hasa ujenzi wa Majumba ya Ufalme kwa muda mfupi na kwa gharama ndogo. Idara hiyo pia huandaa mazoezi kwa ndugu na dada wanaodumisha majengo katika eneo la ofisi yao ya tawi. Pia, katika kila ofisi ya tawi, Idara ya Mahali ya Usanifu-Majengo na Ujenzi huratibu ujenzi na udumishaji wa Majumba ya Ufalme na ya Kusanyiko.

Mwezi wa Januari 2015, wazee wote nchini Marekani walihudhuria mkutano uliounganishwa kupitia video uliozungumzia utaratibu mpya wa kusanifu, kujenga na kudumisha Majumba ya Ufalme. Walijifunza mambo yafuatayo.

  • Ujenzi: Muundo na vifaa vya ujenzi utategemea hali ya eneo na mwongozo kutoka Halmashauri ya Uchapishaji ya Baraza Linaloongoza. Majengo hayo yanapendeza, ni imara na rahisi kuyadumisha.

  • Udumishaji: Katika kila kutaniko, wajitoleaji watazoezwa jinsi ya kutunza majengo yetu ya ibada ili yadumu.

Kwa kweli, kujenga na kudumisha majengo ni kazi kubwa. Hata hivyo, bidii ya watu wa Mungu itaharakisha kazi, na hivyo michango itatumiwa kwa busara.