Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 HABARI KUU | MUNGU ANA MAONI GANI KUHUSU KUVUTA SIGARA?

Janga la Ulimwenguni Pote

Janga la Ulimwenguni Pote

Kuvuta sigara kunasababisha vifo vya watu wengi.

  • Uvutaji sigara uliua watu milioni 100 katika karne iliyopita.

  • Uvutaji sigara huua watu milioni 6 kila mwaka.

  • Kwa wastani, kila baada ya sekunde sita mtu mmoja hufa kwa sababu ya kuvuta sigara.

Hakuna dalili za kupungua kwa tatizo hilo.

Wataalamu wanaonya kwamba ikiwa mambo hayatabadilika, kufikia mwaka 2030, uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu milioni 8 kila mwaka. Pia, wanatabiri kwamba uvutaji wa sigara utasababisha vifo vya watu bilioni 1 hivi kufikia mwishoni mwa karne ya 21.

Hata watu wasiovuta sigara huathiriwa pia. Wanatia ndani watu wa familia, ambao huteseka kihisia na kiuchumi baada ya mvutaji kufa, na vilevile watu 600,000 ambao hufa kila mwaka kwa sababu ya kupumua moshi wa sigara. Hatimaye sisi sote huathiriwa kwa sababu ya kupanda kwa gharama za matibabu.

Kinyume na magonjwa mengine hatari ambayo hufanya madaktari wahangaike kutafuta tiba, suluhisho la tatizo hili linajulikana waziwazi. Dakt. Margaret Chan, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni anasema hivi: “Janga la matumizi ya tumbaku linasababishwa na wanadamu wenyewe, na linaweza kumalizwa kwa ushirikiano kati ya serikali na jamii.”

Mataifa mengi yamefanya jitihada nyingi ili kupambana na janga hili la kiafya. Kufikia Agosti 2012, nchi 175 zilikubaliana kuchukua hatua za kukomesha matumizi ya tumbaku. * Hata hivyo, kuna mambo yanayoendeleza zoea hilo. Kila mwaka, kampuni za kutengeneza tumbaku hutumia pesa nyingi katika matangazo ya kibiashara ili kuvutia wateja wapya, hasa wanawake na vijana katika nchi zinazoendelea. Kwa sababu tumbaku husababisha uraibu, watu zaidi ya bilioni moja wanaoendelea kutumia tumbaku ulimwenguni watazidi kuathiriwa. Zoea hilo lisipokomeshwa, idadi ya watu wanaokufa itaongezeka haraka katika kipindi cha miaka 40 ijayo.

Watu wengi wanatamani kuacha kuvuta sigara lakini wanashindwa kwa sababu ya uraibu na matangazo ya kibiashara. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Naoko. Alianza kuvuta sigara akiwa msichana mdogo. Alihisi kwamba kwa kuiga matangazo ya sigara angekuwa mtu wa kisasa. Licha ya kuona wazazi wake wakifa kwa kansa ya mapafu, aliendelea kuvuta sigara, hata alipokuwa akilea binti zake wawili. Alisema: “Niliogopa kupata kansa ya mapafu na nilihangaikia afya ya watoto wangu, lakini nilishindwa kuacha. Nilidhani nisingeweza kuacha kuvuta sigara.”

Hata hivyo, Naoko alifanikiwa kuacha kuvuta sigara. Kilichomchochea Naoko kuacha kuvuta sigara kimewachochea wengi pia kuepuka zoea hilo. Ni nini hicho? Tafadhali endelea kusoma ili ujue mengi.

^ fu. 11 Hatua hizo zinatia ndani kuwaelimisha watu kuhusu madhara ya kuvuta sigara, kuzuia matangazo ya sigara, kutoza kodi kubwa kwenye bidhaa za tumbaku, na kuanzisha mafunzo ya kuwasaidia watu kuacha kuvuta sigara.