Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Samsoni angewezaje kugusa maiti za watu alioua na bado abaki Mnadhiri?
Katika Israeli la kale, mtu angeweza kuweka nadhiri kwa hiari na awe Mnadhiri kwa muda fulani. * Mojawapo ya vizuizi vilivyokuwa juu ya mtu aliyeweka nadhiri kilisema hivi: “Siku zote za kutengwa kwake kwa ajili ya Yehova asikaribie nafsi yoyote iliyokufa. Hata kwa ajili ya baba yake au mama yake au ndugu yake au dada yake asijitie unajisi watakapokufa.” Namna gani ikiwa mtu fulani ‘angekufa ghafula kando yake’? Kugusa maiti bila kukusudia kungenajisi Unadhiri wake. Hivyo, ilisemekana: “Siku zile za kwanza hazitahesabiwa.” Angehitaji kufanya sherehe za utakaso na kuanza tena kipindi cha Unadhiri.—Hesabu 6:6-12.
Hata hivyo, Samsoni, alikuwa Mnadhiri katika maana tofauti. Kabla ya kuzaliwa kwa Samsoni, malaika wa Yehova alimwambia mama yake hivi: “Tazama! utachukua mimba, nawe utazaa mwana, na wembe wowote usipite juu ya kichwa chake, kwa maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu atakapotoka tumboni; naye ndiye atakayeongoza katika kuokoa Israeli kutoka mkononi mwa Wafilisti.” (Waamuzi 13:5) Samsoni hakuweka nadhiri ya kuwa Mnadhiri. Mungu ndiye aliyemweka rasmi kuwa Mnadhiri, naye angekuwa Mnadhiri maisha yake yote. Katazo kuhusu kugusa maiti halikumhusu. Kama lingemhusu naye aguse maiti bila kukusudia, angewezaje kuanza tena Unadhiri wake ambao ulianza alipozaliwa? Basi, yaonekana kwamba kwa njia fulani, matakwa ya Wanadhiri wa maisha yalitofautiana na ya wale waliojitoa wenyewe kuwa Wanadhiri.
Fikiria amri zinazopatikana katika Biblia ambazo Yehova aliwapa watu watatu ambao walibaki Wanadhiri maisha yao yote, yaani, Samsoni, Samweli, na Yohana Mbatizaji. Kama ilivyotajwa awali, Samsoni hakupaswa kunyoa nywele za kichwa chake. Kabla ya kuchukua mimba ya Samweli, Hana aliweka nadhiri hii: “Nitamtoa kwa Yehova siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita juu ya kichwa chake.” (1 Samweli 1:11) Kuhusu kisa cha Yohana Mbatizaji, malaika wa Yehova alisema hivi: “Asinywe divai na kileo hata kidogo.” (Luka 1:15) Isitoshe, “Yohana [huyu] mavazi yake yalikuwa ya manyoya ya ngamia na alikuwa na mshipi wa ngozi kiunoni mwake; nacho chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.” (Mathayo 3:4) Hakuna mmoja kati ya watu hao watatu aliyeagizwa kutokaribia maiti.
Ingawa alikuwa Mnadhiri, Samsoni alikuwa kati ya waamuzi ambao Yehova aliweka ili kukomboa Waisraeli kutoka mikononi mwa waporaji wao. (Waamuzi 2:16) Ili kutimiza mgawo huo, aligusa maiti. Pindi moja, Samsoni aliua Wafilisti 30 naye akawavua mavazi yao. Baadaye, alienda kuwapiga maadui, “akirundika miguu juu ya mapaja kwa mauaji makubwa.” Pia alichukua mfupa mbichi wa taya ya punda-dume naye akawaua watu elfu moja na mfupa huo. (Waamuzi 14:19; 15:8, 15) Samsoni alifanya yote hayo akiwa na kibali na msaada wa Yehova. Maandiko yanamtaja kuwa mwanamume aliye kielelezo bora cha imani.—Waebrania 11:32; 12:1.
Je, taarifa ya kwamba Samsoni alimpasua simba “kama vile mtu anavyompasua mwana-mbuzi vipande viwili” inaonyesha kwamba katika siku zake lilikuwa zoea la kawaida kupasua wana-mbuzi?
Hakuna uthibitisho unaoonyesha kwamba katika siku za Waamuzi wa Israeli, lilikuwa jambo la kawaida watu kupasua wana-mbuzi. Andiko la Waamuzi 14:6 linasema hivi: “Roho ya Yehova ikaanza kutenda kazi juu [ya Samsoni], naye akampasua [mwana-simba mwenye manyoya shingoni] vipande viwili, kama vile mtu anavyompasua mwana-mbuzi vipande viwili, wala hapakuwa na kitu chochote mkononi mwake.” Yaelekea maneno hayo ni usemi wa mfano.
Maneno “akampasua vipande viwili” yanaweza kuwa na maana mbili. Pengine Samsoni alimshika simba huyo kwenye mataya na kumpasua au kwa njia fulani alimrarua vipande-vipande. Ikiwa alimshika mataya na kumpasua, basi mwanadamu anaweza kumshika mwana-mbuzi mataya na kumpasua. Katika kisa hiki, mfano huo unaonyesha kwamba lingekuwa jambo rahisi kwa Samsoni kumuua simba kwa mikono mitupu sawa tu na kumwua mwana-mbuzi kwa mikono. Hata hivyo, namna gani ikiwa Samsoni alimuua simba huyo kwa kumrarua vipande-vipande? Basi maneno hayo yanapaswa kueleweka kuwa ya mfano. Mfano huo ungemaanisha kwamba roho ya Yehova ilimwezesha Samsoni kufanya kazi iliyohitaji nguvu zisizo za kawaida. Kwa vyovyote vile, ulinganifu unaoelezwa kwenye Waamuzi 14:6 unaonyesha kwamba kwa msaada wa Yehova, simba mwenye nguvu hakuonekana kuwa mkali kwa Samsoni kama vile mwana-mbuzi angekuwa kwa mtu mwenye nguvu za kawaida.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Kuhusu urefu wa wakati wa kipindi cha Unadhiri, mtu aliyeweka nadhiri ndiye aliyeamua muda ambao angeendelea kuwa chini ya nadhiri hiyo. Hata hivyo, kulingana na mapokeo ya Wayahudi, mtu hangeweza kuweka nadhiri kwa muda unaopungua siku 30. Ilifikiriwa kwamba kuweka nadhiri kwa muda unaopungua siku 30 kungeifanya ionekane kuwa jambo la kawaida tu.