Desturi za Krismasi-Je, Ni za Kikristo?
Desturi za Krismasi-Je, Ni za Kikristo?
MSIMU wa Krismasi umefika. Hilo lamaanisha nini kwako, kwa familia yako na marafiki wako? Je, ni pindi ya kiroho, au ni pindi ya kusherehekea tu? Je, ni wakati wa kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo au ni wakati wa kutojishughulisha na desturi za Kikristo?
Unapofikiria maswali hayo, kumbuka kwamba desturi za Krismasi zaweza kutofautiana ikitegemea mahali unapoishi. Mathalani, katika nchi ya Mexico na nchi nyinginezo za Amerika ya Kusini, hata jina lenyewe ni tofauti. Ensaiklopedia moja yasema kwamba jina la Kiingereza Christmas “latokana na neno la Kiingereza cha Enzi za Kati Christes Masse, Misa ya Kristo.” Lakini, neno La Navidad, au Uzaliwa, kama Krismasi iitwavyo katika nchi hizi za Amerika ya Kusini, larejezea kuzaliwa kwa Kristo. Ebu fikiria kwa muda mfupi baadhi ya desturi za nchi ya Mexico. Huenda kufanya hivyo kukakusaidia ubadili maoni yako kuhusu msimu wa sikukuu hii.
Posada, “Wanaume Watatu Wenye Hekima,” na Nacimiento
Sherehe huanza Desemba 16 kwa posada. Kitabu Mexico’s Feasts of Life chasema hivi: “Ni wakati wa posada, siku tisa zenye kupendeza sana kabla ya Mkesha wa Krismasi, ambazo huashiria safari yenye upweke ya Yosefu na Maria ya kuzungukazunguka katika jiji la Bethlehemu na wakati ambapo hatimaye walionyeshwa fadhili na kupewa makao. Familia na marafiki hukusanyika pamoja kila usiku ili kuigiza siku zilizotangulia kuzaliwa kwa Kristo.”
Kimapokeo, kikundi cha watu hubeba sanamu ya Maria na Yosefu kwenye nyumba na kuomba makao au posada kwa kuimba. Wale waliomo nyumbani huimba kwa kuitikia hadi mwishowe wageni wanaruhusiwa kuingia ndani. Kisha karamu huanza ambapo watu fulani—wakiwa wamefungwa macho kwa kitambaa na wakiwa na bakora mkononi—hupokezana zamu wakijaribu kuvunja piñata, nyungu kubwa iliyopambwa ambayo inaning’inia kwenye kamba. Baada ya kuvunjwa, vitu vilivyomo ndani (peremende, matunda, na kadhalika) hukusanywa na watu wanaosherehekea. Baada ya hapo kunakuwa na chakula, vinywaji, muziki, na dansi. Karamu nane za posada hufanywa kuanzia Desemba 16 hadi Desemba 23. Tarehe 24, Nochebuena (mkesha wa Krismasi) husherehekewa, na familia hujitahidi kukutana pamoja ili kula mlo wa pekee.
Baada ya muda mfupi kuna Sikukuu ya Mwaka Mpya, ambayo husherehekewa kwa karamu zenye makelele mengi sana. Jioni ya Januari 5, Tres Reyes Magos (“wanaume watatu wenye hekima”) wanatazamiwa kuletea watoto vichezeo. Kilele huashiriwa na karamu inayofanywa Januari 6, ambapo rosca de Reyes (keki yenye umbo la duara) huandaliwa. Keki hiyo inapoliwa, mtu fulani hupata katika kipande chake mwanasesere mdogo anayefananisha mtoto Yesu. Anayepata mwanasesere huyo huwajibika kupanga na kuandaa karamu ya mwisho Februari 2. (Katika sehemu fulani kuna wanasesere wadogo watatu, wanaofananisha “wanaume watatu wenye hekima.”) Kama uonavyo, karamu zinazohusiana na Krismasi huendelea kwa muda mrefu.
Katika pindi hii, nacimiento (Mandhari ya kuzaliwa kwa Kristo) huwa yenye kutokeza sana. Ni nini kinachohusika katika pindi hii? Katika
sehemu za umma na vilevile makanisani na nyumbani, mandhari hujengwa yakiwa na sanamu (kubwa au ndogo) zilizotengenezwa kwa kauri, mbao, au udongo. Sanamu hizo hufananisha Yosefu na Maria wakipiga magoti mbele za hori yenye kitoto kilichotoka tu kuzaliwa. Mara nyingi kunakuwa na wachungaji na Los Reyes Magos (“wanaume wenye hekima”). Mandhari hiyo huonyesha hori, na huenda kukawa na wanyama kadhaa ili kuikamilisha. Hata hivyo, sanamu iliyo muhimu zaidi ni mtoto mchanga aliyezaliwa, ambaye anaitwa kwa Kihispania el Niño Dios (Mtoto-Mungu). Sanamu ya mtoto huyo mchanga yaweza kuwekwa hapo kwenye Mkesha wa Krismasi.Kuchunguza Desturi za Kuzaliwa kwa Kristo
Kuhusu sherehe za Krismasi kama zijulikanavyo ulimwenguni pote, kichapo The Encyclopedia Americana chasema: “Desturi nyingi zinazohusianishwa na Krismasi leo hazikuwa desturi za Krismasi hapo awali, badala yake zilikuwa desturi za kabla ya Ukristo na zisizo za Kikristo ambazo zilikubaliwa na kanisa la Kikristo. Desturi nyingi za Krismasi zenye shangwe, hufuata kigezo cha Saturnalia, ambayo ni sherehe ya Kiroma iliyosherehekewa katikati ya Desemba. Kwa mfano, kutokana na sherehe hii, kulitokea karamu zenye madoido mengi, kupeana zawadi, na kuwasha mishumaa.”
Katika Amerika ya Kusini, desturi hizo za msingi za Kuzaliwa kwa Kristo, pamoja na desturi nyinginezo hufuatwa. Huenda ukajiuliza ‘zilitoka wapi?’ Kwa kweli, wengi wanaotaka kutii Biblia wanatambua kwamba desturi fulani ni sherehe za ibada ya Waazteki. Gazeti El Universal la Mexico City, lilisema hivi: “Watawa kutoka mashirika mbalimbali ya watawa walitumia sherehe za Waazteki kutegemeza kazi yao ya kueneza-evanjeli na ya umishonari kwa sababu sherehe hizo, kulingana na kalenda ya kidini ya Waazteki, zilisadifiana na kalenda ya Katoliki ya liturujia. Mahali pa sherehe za miungu ya kabla ya enzi ya Kihispania pakachukuliwa na sherehe za miungu ya Kikristo, wakaanzisha sherehe za Ulaya na kutumia pia sherehe za Kihindi, ambazo zilitokeza mchanganyiko wa tamaduni ambazo ni chimbuko la maneno ya Kimexico cha asili.”
Kichapo The Encyclopedia Americana chaeleza hivi: “Michezo ya kuigiza ya Kuzaliwa kwa Kristo ikawa sehemu ya sherehe ya Krismasi hapo awali . . . Inasemekana michezo hiyo ya kuigiza hori kanisani ilianzishwa na Mtakatifu Francis.” Michezo hii ya kuigiza inayokazia kuzaliwa kwa Kristo ilifanywa katika makanisa wakati Mexico ilipofanywa kuwa koloni. Ilipangwa na watawa wa kiume wa “Mtakatifu Francis” ili kufundisha Wahindi kuhusu Kuzaliwa kwa Kristo. Baadaye posada zikawa mashuhuri zaidi. Bila kujali kusudi lake la awali, namna posada zinavyofanywa leo yafunua asili yao ya kweli. Ukiwa Mexico wakati wa msimu huu, unaweza kuona au kuhisi kitu fulani ambacho mwandishi wa El Universal alikazia katika maelezo yake: “Posada ambazo zilikuwa njia ya kutukumbusha safari ya wazazi wa Yesu wakitafuta makao ambapo Mtoto-Mungu angeweza kuzaliwa, leo ni siku za ulevi, matendo mabaya kupindukia, ulafi, mambo ya ubatili, na uhalifu mwingi zaidi.”
Wazo la nacimiento liliibuka nyakati za Ukoloni kutokana na michezo iliyoigizwa na watu katika makanisa. Ingawa watu fulani huvutiwa na wazo hilo, je, linaonyesha kwa usahihi kile ambacho Biblia husema? Hilo ni swali linalofaa. Wakati wanaoitwa wanaume watatu wenye hekima—ambao kwa kweli walikuwa wanajimu—walipozuru Yesu na familia yao hawakuwa wakiishi tena katika hori. Muda ulikuwa umepita, na familia hiyo ilikuwa inaishi katika nyumba. Utafurahia kusoma habari kamili ya simulizi hili lililopuliziwa linalopatikana katika Mathayo 2:1, 11. Unaweza kuona pia kwamba Biblia haisemi kulikuwa na wanajimu wangapi. *
Katika Amerika ya Kusini, wale wanaume watatu wenye hekima wanachukua mahali pa Baba Krismasi. Bado, kama ifanywavyo katika nchi nyingine, wazazi wengi huficha vichezeo katika nyumba. Kisha asubuhi ya Januari 6, watoto huvitafuta, kana kwamba vililetwa na wale wanaume watatu wenye hekima. Wakati huo wauza-vichezeo hupata pesa nyingi, na wengine wametajirika kutokana na jambo ambalo watu wengi wanyofu huliona kuwa fantasia tu. Watu wengi kutia ndani watoto wadogo, wanazidi kukosa imani katika ngano ya wanaume watatu wenye hekima. Ingawa wengine hawafurahii kupungua kwa watu wanaoamini ngano hiyo, mtu aweza kutarajia iweje kwa fantasia inayofuatwa tu kwa sababu ya desturi na kujinufaisha kifedha?
Wakristo wa mapema hawakusherehekea Krismasi, wala Kuzaliwa kwa Kristo. Ensaiklopedia moja yasema hivi kuhusu jambo hilo: “Sherehe hii haikuadhimishwa na kanisa la Kikristo katika karne za kwanza-kwanza, kwa kuwa ilikuwa desturi ya Wakristo kwa ujumla kuadhimisha vifo vya watu mashuhuri wala si kuzaliwa kwao.” Biblia huhusianisha kuadhimisha siku za kuzaliwa na wapagani, si waabudu wa kweli wa Mungu.—Mathayo 14:6-10.
Bila shaka, hiyo haimaanishi kwamba mtu hawezi kufaidika kwa kujifunza na kukumbuka matukio halisi yaliyohusika wakati wa kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu. Simulizi la kweli la Biblia huandaa ufahamu wenye kina ulio wa maana na pia masomo kwa wote wanaotaka kufanya mapenzi ya Mungu.
Kuzaliwa kwa Yesu Kulingana na Biblia
Utapata habari zenye kutegemeka kuhusu kuzaliwa kwa Yesu katika Gospeli za Mathayo na Luka. Zinaonyesha kwamba malaika Gabrieli alimzuru mwanamke mchanga aitwaye Maria ambaye hakuwa ameolewa, katika mji wa Galilaya Luka 1:31-33.
wa Nazareti. Alimletea ujumbe gani? “Tazama! utachukua mimba katika tumbo lako la uzazi na kuzaa mwana, nawe itakupasa kumwita jina lake Yesu. Huyu atakuwa mkubwa na ataitwa Mwana wa Aliye Juu Zaidi Sana; na Yehova Mungu atampa kiti cha ufalme cha Daudi baba yake, naye atatawala akiwa mfalme juu ya nyumba ya Yakobo milele, na hakutakuwa na mwisho wa ufalme wake.”—Maria alishangazwa sana na ujumbe huo. Kwa kuwa hakuwa ameolewa alisema: “Hilo litakuwaje, kwa kuwa huwa sifanyi ngono na mwanamume?” Malaika alijibu: “Roho takatifu itakuja juu yako, na nguvu ya Aliye Juu Zaidi Sana itakufunika kivuli. Kwa sababu hiyo pia kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.” Akitambua kwamba haya yalikuwa mapenzi ya Mungu, Maria alisema hivi: “Tazama! Msichana mtumwa wa Yehova! Na litendeke kwangu kulingana na tangazo lako.”—Luka 1:34-38.
Malaika alimwambia Yosefu kuhusu kuzaliwa huko kwa muujiza ili asimtaliki Maria, jambo alilokuwa anapanga kufanya baada ya kugundua kwamba alikuwa mjamzito. Ndipo akawa tayari kutwaa daraka la kumlea Mwana wa Mungu.—Mathayo 1:18-25.
Kisha amri kutoka kwa Augusto Kaisari ikamlazimu Yosefu na Maria kusafiri kutoka Nazareti la Galilaya hadi Bethlehemu la Yudea, jiji la baba zao wa zamani, ili kusajiliwa. “Walipokuwa huko, siku zikakamilika apate kuzaa. Naye akamzaa mwana wake, mzaliwa wa kwanza, naye akamfunga vitambaa vya nguo na kumlaza katika hori, kwa sababu kulikuwa hakuna mahali kwa ajili yao katika chumba cha makao.”—Luka 2:1-7.
Andiko la Luka 2:8-14 lafafanua kilichofuata: “Katika nchi hiyohiyo kulikuwako pia wachungaji wakiishi nje na wakishika malindo usiku juu ya makundi yao. Na kwa ghafula malaika wa Yehova akasimama kando yao, na utukufu wa Yehova ukamulika kuwazunguka, nao wakawa wenye hofu sana. Lakini malaika akawaambia: ‘Msiwe na hofu, kwa maana, tazama! ninawatangazia nyinyi habari njema ya shangwe kubwa ambayo watu wote watakuwa nayo, kwa sababu kumezaliwa kwenu leo Mwokozi, ambaye, ni Kristo Bwana, katika jiji la Daudi. Na hii ndiyo ishara kwenu: mtapata kitoto kichanga kimefungwa katika vitambaa vya nguo na kikiwa kimelala katika hori.’ Na kwa ghafula kukaja kuwa pamoja na yule malaika umati wa jeshi la kimbingu, ukimsifu Mungu na kusema: ‘Utukufu katika mahali pa juu kwa Mungu, na juu ya dunia amani miongoni mwa watu wa nia njema.’”
Wanajimu
Simulizi la Mathayo lataja kwamba wanajimu kutoka Mashariki walikuja Yerusalemu wakitafuta mahali alipozaliwa Mfalme wa Wayahudi. Mfalme Herode alipendezwa sana na habari hizo—lakini si kwa kusudi zuri. “Akiwatuma Bethlehemu, akasema: ‘Nendeni mkamtafute kwa uangalifu mtoto mchanga, na mkiisha kumpata leteni ripoti kwangu, ili mimi vilevile nipate kwenda na kumsujudia.’” Wanajimu walimpata huyo mtoto mchanga, “wakafungua hazina zao na kumtolea zawadi, dhahabu na ubani na manemane.” Lakini hawakurudi kwa Herode. “Walipewa onyo la kimungu katika ndoto wasirudi kwa Herode.” Mungu alitumia malaika kumwonya Yosefu kuhusu makusudio ya Herode. Ndipo Yosefu na Maria wakatorokea Misri pamoja na mwana wao. Kisha, katika jitihada ya kumwangamiza Mfalme mpya, Mfalme Herode mkatili akaagiza wavulana wauawe katika eneo la Bethlehemu. Wavulana gani? Waliokuwa na umri wa miaka miwili na walio chini ya umri huo.—Mathayo 2:1-16.
Twaweza Kujifunza Nini Kutokana na Simulizi Hilo?
Wanajimu waliozuru—bila kujali walikuwa wangapi—hawakuwa waabudu wa Mungu wa kweli. Tafsiri ya Biblia ya La Nueva Biblia Latinoamérica (Chapa ya 1989) yasema hivi katika kielezi-chini: “Mamajusi hao hawakuwa wafalme, bali wapiga-ramli na makuhani wa dini ya kipagani.” Walikuja kwa sababu ya ujuzi wao kuhusu nyota ambazo walikuwa wamejitoa kwake. Kama Mungu angetaka kuwaongoza hadi kwa mtoto mchanga, wangeelekezwa mahali penyewe hasa bila wao kulazimika kwenda Yerusalemu kwanza kisha kwenye jumba la mfalme Herode. Baadaye, Mungu aliingilia kati ili kugeuza safari yao kusudi amlinde mtoto huyo.
Danieli 2:44; Mathayo 6:9, 10.
Wakati wa Krismasi mara nyingi simulizi hilo hujaa ngano na mambo ya kuwazia-wazia ambayo huficha jambo la maana zaidi: kwamba mtoto huyu alizaliwa awe Mfalme mtukufu, kupatana na tangazo lililotolewa kwa Maria na kwa wachungaji. La, Yesu Kristo si mtoto mchanga tena. Yeye ni Mfalme anayetawala wa Ufalme wa Mungu, ambao hivi karibuni utaondoa serikali zote zinazopinga mapenzi ya Mungu, naye atatatua matatizo yote ya wanadamu. Huo ndio Ufalme tunaoomba katika Sala ya Bwana.—Kupitia tangazo lililotolewa na malaika kwa wachungaji, twajifunza kwamba fursa ya wokovu inapatikana kwa wote ambao wako tayari kusikia ujumbe wa habari njema. Wale wanaopata upendeleo wa Mungu huwa “watu wa nia njema.” Kuna matazamio ya ajabu kuhusiana na amani katika ulimwengu wote chini ya Ufalme wa Yesu Kristo, lakini lazima watu wawe tayari kufanya mapenzi ya Mungu. Je, msimu wa Krismasi huchangia matazamio hayo, na je, msimu huo unadhihirisha tamaa hiyo? Watu wengi wanyofu wanaotaka kuitii Biblia wanaona kwamba jibu ni wazi.—Luka 2:10, 11, 14.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 13 Kuna habari nyingine ambazo hazipasi kupuuzwa: Katika nacimiento ya Mexico, mtoto anaitwa “Mtoto-Mungu” kukiwa na wazo la kwamba Mungu mwenyewe ndiye aliyekuja duniani kama mtoto. Hata hivyo, Biblia huonyesha Yesu kuwa Mwana wa Mungu aliyezaliwa duniani; hakuwa sawa wala hakutoshana na Yehova, Mungu mweza yote. Ona ukweli wa jambo hilo, unaopatikana katika Luka 1:35; Yohana 3:16; 5:37; 14:1, 6, 9, 28; 17:1, 3; 20:17.
[Sanduku katika ukurasa wa 4]
WENGINE WANGESHANGAA
Katika kitabu chake The Trouble With Christmas, mwandishi Tom Flynn alitaja mikataa iliyofikiwa baada ya uchunguzi wa miaka mingi kuhusu Krismasi:
“Mapokeo mengi tunayohusianisha sasa na Krismasi yalitokana na desturi za kipagani za dini za kabla ya Ukristo. Baadhi ya desturi hizo zinahusisha mambo ya kijamii, kingono, au elimu ya kilimwengu ambayo yaweza kufanya watu wa kisasa walioelimika na wanaojali sana mambo ya utamaduni wapuuze desturi hizo wanapoelewa waziwazi chanzo chake.”—Ukurasa wa 19.
Baada ya kutoa uthibitisho chungu nzima wa kuunga mkono habari hiyo, Flynn arejezea jambo la msingi: “Mojawapo ya mambo yenye kushangaza kuhusu Krismasi ni kwamba mambo mengi yanayoihusu si ya Kikristo. Tunapoondoa mambo ya kabla ya Ukristo, mengi ya yale yanayobaki ni ya baada ya Ukristo, na hayatokani na Ukristo wa kweli.”—Ukurasa wa 155.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Tangazo la kuzaliwa kwa Yesu liliwekea msingi daraka lake akiwa Mfalme aliyeteuliwa na Mungu