Unaweza Kudumisha Usafi wa Kiadili Katika Ulimwengu Usio na Maadili
Unaweza Kudumisha Usafi wa Kiadili Katika Ulimwengu Usio na Maadili
KULIKUWA na mwanamume mmoja mweusi hivi na mwenye sura ya kupendeza. Na kulikuwa na mwanamke mrembo mwenye kipawa. Walifanya kazi katika kampuni moja. Huyo mwanamke alimtongoza yule mwanamume waziwazi. Naye mwanamume akamwonyesha anapendezwa naye. Wakanunuliana zawadi. Punde si punde walikuwa wapenzi. Mwanamume akamwacha mke wake ili aishi na yule mwanamke. Hatimaye, yule mwanamke akaamua kuvunja uhusiano huo na kuishi tena na mume wake. Mwanamume yule naye akajaribu shingo upande kumrudia mke wake. Kwa kuwa alikosa majuto ya kweli hakufanikiwa. Watu hao wote waliohusika waliendelea na maisha, ingawa walikuwa wameumizwa.
Adili njema za kingono hazionwi tena kuwa muhimu katika ulimwengu huu. Ufuatiaji wa raha na starehe bila kizuizi waonekana kuwa ndilo jambo la kawaida. Kichapo The New Encyclopædia Britannica chataarifu hivi: “Uzinzi waonekana kuwa jambo la kawaida, na katika maeneo mengine, ni wa kawaida kama ndoa.”
Lakini, Yehova Mungu hutaka ndoa iwe “yenye kuheshimika miongoni mwa wote” na kitanda cha ndoa kiwe “bila kutiwa unajisi.” (Waebrania 13:4) Maandiko husema wazi hivi: “Msiongozwe vibaya. Wala waasherati, wala waabudu-sanamu, wala wazinzi, wala wanaume watunzwao kwa makusudi yasiyo ya asili, wala wanaume walalao pamoja na wanaume . . . hawatarithi ufalme wa Mungu.” (1 Wakorintho 6:9, 10) Kwa hiyo, ili tupate upendeleo wa Mungu, tunahitaji kudumisha usafi wa kiadili katika ulimwengu uliopotoka kiadili.
Tunaweza kujilindaje kutokana na uvutano unaotuzingira? Mfalme Solomoni wa Israeli la kale atoa majibu katika sura 5 ya kitabu cha Biblia cha Mithali. Ebu tuchunguze yale anayosema.
Uwezo wa Kufikiri Utakulinda Wewe
Mfalme huyo wa Israeli aanza kwa kusema hivi: “Mwanangu sikiliza hekima yangu,” Yeye aongezea: “Tega sikio lako, mzisikie akili zangu [“ufahamu wangu,” “NW”]; upate kuilinda busara [“uwezo wa kufikiri” “NW”], na midomo yako iyahifadhi maarifa.”—Mithali 5:1, 2.
Ili kukinza vishawishi kuelekea ukosefu wa adili, tunahitaji kuwa na hekima, yaani ule uwezo wa kutumia ujuzi wa Kimaandiko, na ufahamu, au uwezo wa kutofautisha lililo sahihi na lililo kosa na kuchagua mwendo bora. Tunasihiwa kusikiliza hekima na ufahamu ili kulinda uwezo wetu wa kufikiri. Twaweza kufanyaje hivyo? Tunapojifunza Neno la Mungu, Biblia, tunahitaji kuwa macho kuona jinsi Yehova hufanya mambo na kuelekeza fikira zetu kwa mapenzi yake na makusudi yake. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tukiongoza fikira zetu katika mambo yenye kufaa. Hivyo uwezo wa kufikiri tunaojipatia unapatana na hekima na ujuzi wa Mungu. Unapotumiwa barabara, uwezo huo hutulinda tusinaswe na vishawishi visivyo vya adili.
Jihadhari na Kinywa Laini
Linalofanya uwezo wa kufikiri uwe wa maana katika kudumisha usafi wa kiadili katika ulimwengu mchafu ni kwa sababu njia za mtu asiye mwadilifu huvutia. Solomoni aonya hivi: “Maana midomo ya malaya [“mwanamke mgeni,” “NW”] hudondoza asali, na kinywa chake ni laini kuliko mafuta; lakini mwisho wake ni mchungu kuliko pakanga; ni mkali kama upanga wa makali kuwili.”—Mithali 5:3, 4.
Katika mithali hii, mtu mpotovu aitwa “mwanamke mgeni”—malaya. * Maneno yake ya kutongoza ni matamu kama asali na ni laini kuliko mafuta ya zeituni. Je, mara nyingi kutongoza hakuanzi hivyo? Kwa mfano, fikiria yaliyompata mwanamke mrembo wa miaka 27 aitwaye Amy, ambaye ni karani. Yeye anasimulia: “Kuna mwanamume fulani kazini kwetu ambaye huniangalia daima na kunisifu kila wakati. Inapendeza kuonyeshwa shauku. Lakini naweza kuona waziwazi kuwa anataka tu kulala nami. Mimi sitadanganywa na utongozaji wake.” Kwa kawaida maneno laini ya mtongozaji hunasa haraka tukishindwa kutambua lengo lake. Kwa sababu hiyo tunahitaji kutumia uwezo wetu wa kufikiri.
Matokeo ya ukosefu wa adili kingono ni machungu kama pakanga na makali kama upanga wenye makali kuwili, yaani ni machungu na huleta kifo. Dhamiri mbaya, mimba haramu, au maradhi yenye kuambukizwa kingono kwa kawaida ndiyo matokeo machungu ya mwenendo wa aina hiyo. Na ebu fikiria maumivu makali ya kihisia-moyo yanayompata mwenzi wa ndoa wa mtu asiye mwaminifu. Tendo moja la uzinzi laweza kuleta maumivu yenye kudumu maishani. Naam, ukosefu wa adili huumiza.
Akitoa maelezo juu ya mtindo-maisha wa mwanamke mpotovu, mfalme mwenye hekima aendelea kusema: “Miguu yake inatelemkia mauti; hatua zake zinashikamana na kuzimu [“Sheoli,” “NW”]; hata asiweze kuiona njia sawa ya uzima; njia zake ni za kutanga-tanga wala hana habari.” (Mithali 5:5, 6) Njia zake mwanamke asiye na adili humwongoza kwenye mauti—hatua zake huelekea Sheoli, kaburi la ujumla la wanadamu. Kuenea kwa magonjwa yenye kupitishwa kingono, na hasa UKIMWI, kunathibitisha maneno hayo kwelikweli! Mwisho wake unakuwa sawa na wa wale wanaoandamana naye katika njia zake potovu.
Akihangaika moyoni, mfalme asihi hivi: “Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, wala msiache maneno ya kinywa changu. Itenge njia yako mbali naye, wala usiukaribie mlango wa nyumba yake.”— Mithali 5:7, 8.
Tunahitaji kujitenga mbali tuwezavyo na uvutano wa watu wapotovu kiadili. Kwa nini tuzipe nafasi njia zao kupitia kusikiliza muziki unaoshusha heshima, kutazama vitumbuizo vyenye kufisidi, au kusoma vichapo vyenye ponografia? (Mithali 6:27; 1 Wakorintho 15:33; Waefeso 5:3-5) Na ni upumbavu ulioje kukaribisha uvutano wao kwa ubembe au kwa kujipamba na kuvalia kusiko kwa adabu!—1 Timotheo 4:8; 1 Petro 3:3, 4.
Hasara Kubwa Mno
Tuna sababu gani nyingine ya kujitenga mbali na njia za mtu mpotovu? Solomoni anajibu: “Usije ukawapa wengine heshima yako, na wakorofi miaka yako; wageni wasije wakashiba nguvu zako; kazi zako zikawa ndani ya nyumba ya mgeni; nawe ukaziombolea siku zako za mwisho, nyama yako na mwili wako utakapoangamia.”— Mithali 5:9-11.
Hivyo Solomoni anakazia ile hasara kubwa ya kushindwa na ukosefu wa adili. Uzinzi na kujipotezea heshima huambatana pamoja. Je, kwa kweli si jambo la kujifedhehesha kutumika tu kama chombo cha kutosheleza harara zako au za mtu mwingine zisizo za adili? Na si kukosa kujistahi unapojiingiza katika mahusiano ya kingono na mtu ambaye si mwenzi wako wa ndoa?
Lakini ‘kuwapa wakorofi au wageni miaka yetu, nguvu zetu, na kazi zetu’ hutia ndani nini? Kitabu kimoja cha marejezo chataarifu hivi: “Jambo kuu katika mistari hii liko wazi kabisa: Uzinzi huenda ukaleta hasara kubwa; kwa kuwa kila kitu ambacho mtu hujitaabisha kutafuta—wadhifa, uwezo, ufanisi—vyote hivyo vyaweza kupotea kutokana na madai yenye pupa ya mwanamke huyo au malipo ya kufunika aibu ya ukoo wa watu wake.”
Ukosefu wa adili kingono waweza kuleta hasara kubwa!Baada ya kupoteza heshima na mali yake, mtu mpumbavu huguna, akisema: “Jinsi nilivyochukia maonyo, na moyo wangu ukadharau kukemewa; wala sikuisikia sauti ya waalimu wangu, wala sikuwategea sikio langu walionifundisha! Nalikuwa karibu na kuingia katika maovu yote, katikati ya mkutano na kusanyiko.”— Mithali 5:12-14.
Hatimaye, mwenye dhambi huyo husema maneno ambayo msomi mmoja ayaita “orodha ndefu ya ‘laiti ninge . . . ’: laiti ningemsikiliza baba yangu; laiti ningeacha kujitegemea mwenyewe; laiti ningesikiliza mashauri ya wengine.” Hata hivyo, utambuzi huo huja ukiwa umechelewa mno. Kufikia hapo maisha machafu na adhama ya mtu huyo huwa yameharibika kabisa. Jinsi ilivyo muhimu sana kwetu kufikiria kwa uzito hasara kubwa ya kushiriki katika ukosefu wa adili kingono kabla ya kumezwa ndani yake!
“Unywe Maji ya Birika Lako Mwenyewe”
Je, Biblia yaona aibu kuyataja mambo yanayohusu ngono? Sivyo kamwe. Upendo na msisimuko ulio kati ya mwanamume na mwanamke ni zawadi kutoka kwa Mungu. Hata hivyo, uhusiano huo wapaswa kufurahiwa na wenzi waliooana tu. Hivyo kwa mtu aliyeoa, Solomoni atoa himizo hili: “Unywe maji ya birika lako mwenyewe, na maji yenye kububujika katika kisima chako. Je! chemchemi zako zitawanyike mbali, na mito ya maji katika njia kuu? Yawe yako mwenyewe peke yako, wala si ya wageni pamoja nawe.”—Mithali 5:15-17.
“Birika lako mwenyewe” na “kisima chako” ni semi za kishairi zinazomhusu mke anayependwa. Kuwa na uhusiano wa ngono pamoja naye hufananishwa na kunywa maji yenye kuburudisha. Tofauti na maji ya umma, birika au kisima huonwa kuwa mali ya mtu binafsi. Na mwanamume anashauriwa kuzaa watoto nyumbani pamoja na mke wake badala ya kutawanya mbegu zake katika njia kuu, yaani, miongoni mwa wanawake wengineo. Kwa wazi, shauri hilo lamtaka mwanamume awe mwaminifu kwa mke wake.
Mtu huyo mwenye hekima aendelea kusema:“Chemchemi yako ibarikiwe; nawe umfurahie mke wa ujana wako. Ni ayala apendaye na paa apendezaye; maziwa yake yakutoshe sikuzote; na kwa upendo wake ushangilie daima.”—Mithali 5:18, 19.
“Chemchemi” ya maji hurejezea chanzo cha uradhi katika ngono. Furaha ya ngono pamoja na mwenzi wa ndoa ‘imebarikiwa’ na ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kwa sababu hiyo, mwanamume anasihiwa amfurahie mke wa ujana wake. Kwake yeye, mke wake ni mpendwa na mrembo kama paa jike na mwenye kupendeza na madaha kama mbuzi wa mlimani.
Kisha Solomoni auliza maswali mawili ya kufikiriwa: “Mwanangu! mbona unashangilia malaya [“mwanamke mgeni,” “NW”], na kukikumbatia kifua cha mgeni?” (Mithali 5:20) Naam, mbona mtu ambaye amefunga ndoa ashawishiwe kufanya ngono nje ya ndoa kupitia mahusiano kazini, shuleni, au penginepo?
Mtume Paulo awapa Wakristo waliofunga ndoa shauri hili: “Nisemalo 1 Wakorintho 7:29) Hilo lamaanisha nini? Bila shaka, wanafunzi wa Yesu Kristo wapaswa ‘kufuliza kutafuta kwanza ufalme.” (Mathayo 6:33) Kwa hiyo, wenzi wa ndoa hawapaswi kufikiria mno mambo yao wenyewe hata waweke masilahi ya Ufalme mahali pa pili maishani mwao.
ni hili, akina ndugu, wakati ubakio umepunguzwa. Tangu sasa acheni wale walio na wake wawe kama kwamba hawana.” (Uhitaji wa Kujidhibiti
Tamaa za ngono zaweza kudhibitiwa. Wale wanaotamani kibali cha Yehova ni lazima wazidhibiti. Mtume Paulo alitoa onyo hili la upole: “Haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kule kutakaswa kwenu, kwamba mjiepushe na uasherati; kwamba kila mmoja wenu apaswe kujua jinsi ya kupata umiliki wa chombo chake mwenyewe katika utakaso na heshima.”—1 Wathesalonike 4:3, 4.
Hivyo basi, vijana hawapaswi kuoa haraka-haraka wahisipo tu misukumo ya kingono kwa mara ya kwanza. Ndoa huhitaji kujitolea, na kutimiza daraka hilo huhitaji ukomavu. (Mwanzo 2:24) Lililo bora zaidi ni kungojea hadi ‘upite mchanuko wa ujana’—ule wakati wa kilele cha hisi za ngono ambao waweza kupotoa maamuzi ya mtu. (1 Wakorintho 7:36) Ni ukosefu wa hekima na dhambi iliyoje kwa mtu anayetamani kuoa kuanza uhusiano wa kingono usio na adili eti tu kwa sababu hakuweza kumpata mwenzi wa ndoa anayefaa!
“Maovu Yake Yeye Yatampata Mdhalimu”
Sababu kuu inayofanya ukosefu wa adili katika ngono uwe kosa ni kwamba Yehova, Mpaji wa uhai na Mwenye kuweka ndani yetu uwezo wa kingono, huukataa. Hivyo Mfalme Solomoni, akitoa kichocheo chenye nguvu cha kuwa safi kiadili ataarifu hivi: “Kwa maana njia za mwanadamu zi mbele za macho ya BWANA, na mienendo yake yote huitafakari.” (Mithali 5:21) Naam, hakuna kilichofichika machoni pa Mungu, “ambaye kwake sisi tuna kutoa hesabu.” (Waebrania 4:13) Tendo lolote lile lisilo safi kiadili, hata athari yake ya kimwili na ya kijamii iweje, halina budi kuharibu uhusiano wetu pamoja na Yehova. Ni upumbavu jinsi gani kupoteza amani pamoja na Mungu kwa sababu ya kufurahia dhambi kwa muda mfupi!
Baadhi ya wale wanaojitia mno bila aibu katika mienendo isiyo ya adili huenda wakaonekana kufanya hivyo bila kupata adhabu yoyote—lakini si kwa kitambo kirefu. Solomoni atangaza hivi: “Maovu yake yeye yatampata mdhalimu, naye atashikwa kwa kamba za dhambi zake. Atakufa huyo kwa kukosa maonyo, naye atapotea kwa wingi wa ujinga wake.”—Mithali 5:22, 23.
Mbona yeyote kati yetu apotee? Kwani, kitabu cha Mithali hutuonya kimbele juu ya njia zenye utongozi za ulimwengu huu. Na chaonyesha wazi hasara inayoletwa na ukosefu wa adili katika ngono—kama vile kuharibu afya yetu, mali zetu, nguvu yetu, na heshima yetu. Tukiwa wenye busara ya namna hiyo hatutasema kamwe maneno mengi ya “laiti ninge . . . ” Naam, kwa kutumia mashauri ambayo Yehova ameandaa katika Neno lake lililopuliziwa, tunaweza kudumisha usafi wa kiadili katika ulimwengu usio na maadili.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 11 Neno “mgeni” lilitumiwa kwa wale walioacha kutenda kupatana na Sheria na hivyo wakajitenga wenyewe mbali na Yehova. Kwa hivyo, malaya anarejezewa kuwa “mwanamke mgeni.”
[Picha katika ukurasa wa 30]
Matokeo ya ukosefu wa adili katika ngono ni machungu kuliko pakanga
[Picha katika ukurasa wa 31]
“Umfurahie mke wa ujana wako”