Je, Wajua?
Kuna uthibitisho gani tofauti na Biblia unaoonyesha kwamba Waisraeli walikuwa watumwa huko Misri?
Biblia inaripoti kwamba baada ya Wamidiani kumpeleka Yosefu nchini Misri, mzee wa ukoo Yakobo pamoja na familia yake walihama kutoka Kanaani na kwenda Misri. Waliishi Misri katika eneo la Gosheni, kwenye delta ya Mto Nile. (Mwa. 47:1, 6) Waisraeli “wakazidi kuwa wengi na kuwa na nguvu isivyo kawaida.” Hivyo, Wamisri wakazidi kuwaogopa Waisraeli nao wakawalazimisha kuwa watumwa.—Kut. 1:7-14.
Baadhi ya wachambuzi katika nyakati zetu wamedhihaki kwamba simulizi hilo la Biblia ni hekaya. Lakini kuna uthibitisho kwamba Wasemiti, yaani, wazao wa Shemu * waliishi wakiwa watumwa katika nchi ya kale ya Misri.
Kwa mfano, wachimbuaji wa vitu vya kale wamechimbua maeneo ya kale yaliyokaliwa na watu kwenye upande wa kaskazini wa nchi ya Misri. Dr. John Bimson anaripoti kwamba kwenye eneo hilo lililo kaskazini mwa nchi ya Misri, kuna uthibitisho wa maeneo 20 au zaidi yaliyokaliwa na Wasemiti. Zaidi ya hayo, James K. Hoffmeier, mchunguzi wa vitu vya kale vya Misri, anasema hivi: “Kuanzia mwaka wa 1800 hadi 1540 K.W.K. hivi, Wasemiti kutoka magharibi mwa Asia waliiona nchi ya Misri kuwa mahali pazuri pa kuhamia.” Anaongezea hivi: “Kipindi hicho cha wakati ndicho kipindi kilekile cha ‘Enzi za Wazee wa Ukoo’ na hivyo kinalingana na wakati na hali zinazofafanuliwa kwenye kitabu cha Mwanzo.”
Kuna uthibitisho mwingine uliopatikana kusini mwa nchi ya Misri. Kipande cha hati za mafunjo cha wakati wa Ufalme wa Katikati (m. 2000– m. 1600 K.W.K.) kina orodha ya majina ya watumwa waliofanya kazi katika nyumba fulani huko kusini mwa Misri. Zaidi ya majina 40 ya watumwa hao ni ya Kisemiti. Watumwa au watumishi hao walikuwa wapishi, wafumaji, na vibarua. Hoffmeier, anaendelea kusema hivi: “Kwa kuwa zaidi ya Wasemiti arobaini walifanya kazi katika nyumba moja kwenye eneo la Thebaid [kusini mwa Misri], inaonekana kwamba idadi yao kotekote nchini Misri na hasa eneo la Delta, ilikuwa kubwa.”
David Rohl, mchimbuaji wa vitu vya kale, aliandika kwamba baadhi ya majina ya watumwa walio kwenye orodha hiyo “yanafanana sana na majina ya watu wanaotajwa katika Biblia.” Kwa mfano, vipande hivyo vina majina yanayofanana na majina kama vile Isakari, Asheri, na Shifra. (Kut. 1:3, 4, 15) Rohl anamalizia hivi: “Huo ni uthibitisho halisi wa kwamba Waisraeli walikuwa watumwa nchini Misri wakati huo.”
Dkt. Bimson anaeleza hivi: “Masimulizi ya Biblia kuhusu utumwa nchini Misri na kuhusu Safari ya Kutoka huko yanategemea msingi thabiti wa kihistoria.”
^ fu. 4 Jina Wasemiti linatokana na Shemu aliyekuwa mmoja wa wana watatu wa Noa. Inaelekea wazao wa Shemu walitia ndani Waelamu, Waashuru, Wakaldayo wa kale, Waebrania, Wasiria, na makabila kadhaa ya Waarabu.