Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Ekuado

Mwaka wa 2007, nchi ya Ekuado ilitangaza mipango ya kugharimia kulinda eneo lenye ukubwa wa karibu kilomita 10,000 za mraba la msitu wa mvua wa Amazoni ili lisichimbwe mafuta. Mipango hiyo ilisitishwa kwa sababu nchi zingine hazikutoa mchango wa kifedha kwa ajili ya mradi huo. Eneo hilo la msitu wa mvua ni moja kati ya maeneo yenye viumbe wengi sana ulimwenguni.

Japani

Gazeti The Japan News linasema kwamba ni vigumu sana kugundua virusi damu inapopimwa. Taarifa hiyo ilitokana na kisa kilichotokea mwaka wa 2013, ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 60 hivi aliambukizwa virusi vya UKIMWI kwa kutiwa damu mishipani. Ikiwa damu iliyotolewa ina virusi vya UKIMWI, kuna kipindi ambacho si rahisi kugundua virusi hivyo damu inapopimwa.

Zimbabwe

Ingawa mapigano katika mpaka wa nchi ya Zimbabwe na Msumbiji yaliisha zaidi ya miaka 30 iliyopita, mabomu ya ardhini yameendelea kuwalemaza na kuwaua watu. Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu liliripoti hivi: “Tangu mwaka 1980, mabomu hayo yameua zaidi ya watu 1,500 na mifugo 120,000 na kuwalemaza watu 2,000 kwenye upande wa mpaka wa Zimbabwe.”

Australia

Kulingana na uchunguzi fulani, mara nyingi mume na mke wanaotalikiana hugombana kuhusu jinsi watakavyowatunza wanyama-vipenzi. Wanyama-vipenzi huwa katika orodha ya vitu vinavyogombaniwa kama vile nyumba na mashamba, pesa na vitu fulani vya kibinafsi.