Kuutazama Ulimwengu
Hispania
Kikundi fulani cha wanasayansi kinaamini kwamba inawezekana shughuli za wanadamu zilichangia kutokea kwa tetemeko la ardhi mwaka wa 2011 huko Lorca, kusini mwa Hispania, ambalo liliua watu tisa na kuwajeruhi wengi. Wanajiolojia walihusianisha tetemeko hilo na maji mengi yaliyokuwa yamechimbwa chini ya ardhi kwa ajili ya kumwagilia mashamba.
China
Watalii kutoka China walitumia dola bilioni 102 za Marekani kutembelea nchi za nje mwaka wa 2012. Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Ulimwenguni, kiasi hicho kinafanya China iwe kati ya nchi zilizotumia pesa nyingi zaidi katika utalii, hata kuliko watalii kutoka Ujerumani waliotumia dola bilioni 84 na watalii kutoka Marekani waliotumia dola bilioni 83.
Japani
Gazeti la kitiba linaloitwa BMJ la Uingereza lilichapisha utafiti uliofanyiwa watu 68,000 hivi kwa kipindi cha miaka 23 huko Japani. Watafiti walisema kwamba wanawake waliozaliwa kati ya mwaka wa 1920 na 1945 ambao walianza kuvuta sigara kabla ya kufikisha umri wa miaka 20 walikufa miaka kumi hivi mapema kuliko wanawake ambao hawakuvuta sigara kamwe; wanaume walikufa miaka minane mapema.
Mauritania
Serikali imepiga marufuku kuingizwa, kutengenezwa, na kutumiwa kwa mifuko ya plastiki ili kulinda viumbe wa baharini na wa nchi kavu. Badala yake, serikali inahimiza watu watumie mifuko inayoweza kuoza.
Ulimwenguni
Kila mwaka, kampuni za bima zinatumia dola bilioni 50 hivi za Marekani kulipia hasara zinazotokana na misiba inayoletwa na hali ya hewa. Inakadiriwa kwamba kuanzia miaka ya 1980, hasara hizo zinaongezeka maradufu kila baada ya miaka kumi.