Kutembea Kwenye Njia ya Watumwa
Kutembea Kwenye Njia ya Watumwa
KUANZIA karne ya 17 hadi karne ya 19, jiji la Ouidah lilikuwa kituo kikuu cha biashara ya watumwa katika Afrika Magharibi. Zaidi ya watumwa milioni moja walisafirishwa kutoka jiji hilo ambalo leo liko katika Jamhuri ya Benin. Mara nyingi, Waafrika waliwatoa Waafrika wenzao kuwa watumwa ili wapate mvinyo, nguo, bangili, visu, panga, na hasa bunduki, ambazo zilihitajiwa sana kwa sababu ya vita vya kikabila.
Kati ya karne ya 16 na 19, inakadiriwa kwamba Waafrika milioni 12 walisafirishwa kwa meli kupitia Bahari ya Atlantiki ili wakatumikishwe katika mashamba na migodi ya mabara ya Amerika. Kitabu American Slavery—1619-1877 kinasema kwamba asilimia 85 hivi ya watumwa hao “walipelekwa Brazili na huko Karibea katika nchi zilizokuwa koloni za Uingereza, Ufaransa, Hispania, na Uholanzi.” Asilimia 6 hivi walipelekwa kwenye koloni ambazo zingekuja kuwa sehemu ya Marekani. *
Mwanzoni mwa safari yao, wengi wa watumwa hao—wakiwa wamefungwa minyororo, kupigwa, na kutiwa alama mwilini kwa chuma moto—walitembea umbali wa kilomita nne kutoka ngome iliyojengwa upya ambayo sasa ni Jumba la Makumbusho la Historia la Ouidah, hadi ufuoni kwenye ule unaoitwa Door of No Return (Mlango wa Mwisho). Mlango huo ndio mwisho wa Njia ya Watumwa. Si mlango halisi kwa kuwa watumwa wote hawakusafirishwa kutoka hapo. Kwa nini biashara ya watumwa ilipendwa sana?
Historia Ndefu Isiyopendeza
Tangu hapo zamani, watawala Waafrika waliwauza mateka wao wa vita kwa Waarabu. Baadaye, nchi za Ulaya ziliingia kwenye biashara hiyo ya watumwa, hasa baada ya kupata koloni katika mabara ya Amerika. Wakati huo, vita vya kikabila na mateka waliochukuliwa walifanya kuwe na watumwa wengi, na hilo likafanya vita kuwa biashara yenye kuleta faida nyingi kwa washindi na pia kwa wafanyabiashara ya utumwa waliokuwa na pupa. Isitoshe, watumwa walitekwa nyara na wengine waliletwa na wafanyabiashara Waafrika kutoka sehemu za ndani za Afrika. Mtu yeyote angeweza kuuzwa kama mtumwa, hata mwana wa mfalme ambaye alikuwa amepoteza kibali cha mfalme.
Mbrazili, Francisco Félix de Souza, alikuwa muuzaji wa watumwa aliyejulikana sana. Katika mwaka wa 1788, De Souza alisimamia ngome ambayo ilikuwa kituo cha soko la watumwa la Ouidah katika Ghuba ya Benin. Wakati huo, Ouidah ilikuwa chini ya Ufalme wa Dahomey. Hata hivyo, De Souza na Mfalme Adandozan wa Dahomey walikosana. Hivyo, De Souza, huenda akiwa gerezani, alipanga njama na ndugu ya mfalme, na pamoja wakampindua mtawala huyo katika mwaka wa 1818. Mapinduzi hayo yalianzisha uhusiano wa kibiashara kati ya mfalme mpya aliyeitwa Ghezo, na De Souza, ambaye aliwekwa asimamie biashara ya watumwa.Ghezo alitaka kupanua ufalme wake na alihitaji silaha kutoka Ulaya ili kufanya hivyo. Kwa hiyo, alimweka rasmi De Souza kuwa gavana mkuu wa Ouidah ili afanye biashara na Wazungu. Kwa kuwa alikuwa na mamlaka kamili juu ya biashara ya watumwa katika sehemu hiyo ya Afrika, De Souza alijikusanyia mali nyingi, na soko la watumwa ambalo lilikuwa karibu na nyumba yake, likawa kituo kikuu kwa wanunuzi wageni na wenyeji.
Safari Iliyojaa Majonzi
Mtu anapotembelea Njia ya Watumwa ya Ouidah leo, ataanza matembezi yake katika ngome ya Wareno iliyojengwa upya. Ngome hiyo iliyojengwa kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 1721 sasa ni jumba la makumbusho kama ilivyotajwa hapo awali. Mateka ambao wangeuzwa kama watumwa walifungiwa katika ua mkubwa uliokuwa katikati. Wengi wao walikuwa wametembea kwa siku nyingi usiku wakiwa wamefungwa minyororo pamoja kabla ya kuwasili hapo. Kwa nini walisafirishwa usiku? Giza liliwafanya wachanganyikiwe na kufanya iwe vigumu kwa wale waliotoroka kurudi nyumbani.
Kikundi cha watumwa kilipowasili, mnada ulifanywa, na wafanyabiashara waliwatia alama watumwa waliowanunua kwa chuma moto. Watumwa ambao wangesafirishwa hadi nchi za ng’ambo walipelekwa ufuoni ambapo mitumbwi au mashua ndogo ziliwasafirisha hadi kwenye meli.
Sehemu nyingine katika Njia ya Watumwa ya kale ilikuwa ule Mti wa Usahaulifu. Leo, nguzo imejengwa iwe kumbukumbu la mahali ambapo kulikuwa na mti ambao watumwa walilazimishwa watembee kuuzunguka—inasemekana kwamba wanaume waliuzunguka mara tisa na wanawake mara saba. Waliambiwa kwamba kuuzunguka kungewasaidia kufuta kumbukumbu zozote za nyumbani kwao, na kuwazuia kuasi.
Njia hiyo pia ina nguzo iliyojengwa kuwa kumbukumbu ya nyumba za Zomaï ambazo hazipo siku hizi. Zomaï inamaanisha giza lililokuwa ndani ya nyumba hizo ambazo zilikuwa zimekusudiwa
kuwafanya mateka wazoee hali mbovu ambazo wangepata ndani ya meli zilizosongamana. Kwa kweli, huenda walifungiwa ndani ya nyumba hizo kwa miezi kadhaa wakingojea usafiri. Wale waliokufa chini ya hali hizo mbovu walitupwa ndani ya kaburi la jumla.Nguzo inayoitwa Zomachi, ambayo inawakilisha toba na upatano, ni kikumbusho chenye kuhuzunisha. Kila Januari (Mwezi wa 1), wazao wa watumwa na wazao wa wafanyabiashara ya watumwa hukusanyika hapo ili kuwaombea msamaha wale waliotekeleza matendo hayo yasiyo ya haki.
Kituo cha mwisho kwenye njia hiyo ni ule Mlango wa Mwisho—ambao ni ukumbusho wa dakika za mwisho za watumwa barani Afrika. Mwingilio huo mkubwa wenye tao una michongo inayoonyesha safu mbili za Waafrika waliofungwa minyororo wakiwa wamekusanyika katika ufuo ulio karibu, wakielekea kwenye Bahari ya Atlantiki. Inasemekana kwamba mateka fulani walipofika hapo walikula mchanga ili kukumbuka nchi yao. Wengine waliamua kujiua kwa kujinyonga kwa minyororo waliyokuwa wamefungwa nayo.
Kuwekwa Huru!
Kuanzia miaka ya mapema ya 1800, jitihada nyingi zilifanywa ili kukomesha biashara ya watumwa. Mashua ya mwisho iliyobeba watumwa kutoka Ouidah iliwasili huko Mobile, Alabama, Marekani, mnamo Julai 1860. Hata hivyo, utumwa wao ulikuwa wa muda mfupi kwa kuwa serikali ya Marekani ilitoa Tangazo la Kuwekwa Huru mnamo 1863. Hatimaye, utumwa ulifikia kikomo katika Mabara ya Amerika wakati ambapo Brazili ilikomesha zoea hilo mwaka wa 1888. *
Kumbukumbu inayoonekana ya biashara ya watumwa ni idadi kubwa ya Waafrika waliotapakaa katika sehemu mbalimbali za mabara ya Amerika. Hilo limebadili sana idadi ya watu na utamaduni katika mabara hayo. Jambo lingine linalowakumbusha watu kuhusu biashara hiyo ni kuenea kwa dini inayohusisha mambo ya uchawi na ulozi (voodoo) kama ule ulio maarufu huko Haiti. Encyclopædia Britannica inasema kwamba “neno voodoo linatokana na neno vodun, linalomaanisha mungu, au roho, katika lugha ya Fon huko Benin (ambayo zamani iliitwa Dahomey).”
Kwa kusikitisha, watu wengi leo wako chini ya aina nyingine ya utumwa, ingawa si kwa njia halisi. Kwa mfano, mamilioni wanamenyeka ili wajiruzuku chini ya hali ngumu za kiuchumi. Wengine wanateseka chini ya mamlaka za kisiasa zenye kukandamiza. (Mhubiri 8:9) Na mamilioni wengine wako chini ya utumwa wa mafundisho ya dini za uwongo na ushirikina. Je, serikali za wanadamu zinaweza kuwaweka huru raia zake kutokana na utumwa wa aina hiyo? La! Ni Yehova Mungu peke yake anayeweza kufanya hivyo, naye atafanya hivyo! Kwa kweli, Biblia ambayo ni Neno lake lililoandikwa, inaahidi kwamba siku moja wote wanaomwabudu Yehova kulingana na kweli ya Biblia—kweli ambayo huwaweka watu huru—watafurahia “uhuru wenye utukufu wa watoto wa Mungu.”—Waroma 8:21; Yohana 8:32.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Idadi ndogo ya watumwa waliokuwepo mwanzoni huko Marekani iliongezeka, hasa kwa sababu ya watumwa kuzaana.
^ fu. 7 Jina “Ghezo” linaandikwa kwa njia mbalimbali.
^ fu. 17 Maoni ya Biblia kuhusu utumwa yanazungumziwa katika habari, “Maoni ya Biblia: Je, Mungu Alikubali Biashara ya Watumwa?” katika toleo la Amkeni! la Septemba 8, 2001 (8/9/2001).
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]
“MWANADAMU AMEMTAWALA MWANADAMU KWA KUMUUMIZA”
Watu wengi wanaamini kwamba wafanyabiashara ya utumwa walipata mawindo yao kwa kushambulia vijiji na kuteka nyara mtu yeyote waliyetaka. Ingawa huenda ilikuwa hivyo, inaelekea kwamba wafanyabiashara hao hawangeweza kuchukua mamilioni ya watumwa “bila ushirikiano wa viongozi na wafanyabiashara Waafrika,” alisema Dakt. Robert Harms, profesa wa historia ya Afrika, katika mahojiano kwenye redio. Ni wazi kwamba “mwanadamu amemtawala mwanadamu kwa kumuumiza”!—Mhubiri 8:9.
[Hisani]
© Réunion des Musées Nationaux/Art Resource, NY
[Ramani katika ukurasa wa 22]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Inakadiriwa kwamba Waafrika milioni 12 walisafirishwa kwenye Bahari ya Atlantiki wakawe watumwa
AFRIKA
BENIN
Ouidah
Pwani ya Watumwa
[Picha katika ukurasa wa 22, 23]
Ngome hii iliyojengwa na Wareno mwaka wa 1721, sasa ni Jumba la Makumbusho la Historia la Ouidah
[Hisani]
© Gary Cook/Alamy
[Picha katika ukurasa wa 23]
Sanamu ya mtumwa akiwa amefungwa mdomo na mikono
[Picha katika ukurasa wa 23]
Mlango wa Mwisho—ukumbusho wa dakika za mwisho za watumwa barani Afrika
[Hisani]
© Danita Delimont/Alamy