Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ninaishi kati ya tamaduni mbili Nifanye nini?

Ninaishi kati ya tamaduni mbili Nifanye nini?

Vijana Huuliza . . .

Ninaishi kati ya tamaduni mbili Nifanye nini?

“Familia yetu ni ya Kiitaliano, nasi huonyeshana upendo na uchangamfu waziwazi. Sasa tunaishi Uingereza. Waingereza ni watu watulivu wanaopenda kujitenga. Sijui nifuate utamaduni gani, sijioni kuwa Mwitaliano wala Mwingereza.”—Giosuè, Uingereza.

“Shuleni mwalimu aliniambia nimtazame usoni anapozungumza. Lakini nilipomtazama hivyo Baba, aliniambia sina adabu. Tamaduni hizo mbili zilinitatanisha.”—Patrick, Mwalgeria aliyehamia Ufaransa.

Je, baba au mama yako ni mhamiaji?

□ Ndiyo □ Hapana

Je, shuleni kwenu watu wanatumia lugha au kufuata utamaduni tofauti na ule unaofuatwa nyumbani kwenu?

□ Ndiyo □ Hapana

KILA mwaka, mamilioni ya watu huhamia nchi nyingine na wengi wao hukumbwa na matatizo makubwa. Ghafula wanajikuta wamezungukwa na watu wenye lugha, utamaduni, na mavazi tofauti na yao. Kwa sababu hiyo mara nyingi wahamiaji hudhihakiwa. Msichana anayeitwa Noor alipatwa na hali hiyo. Familia yao ilihamia Amerika ya Kaskazini kutoka Jordan. Anasema: “Tulivaa mavazi tofauti na hivyo watu walitucheka, pia hatukuelewa vichekesho vya Wamarekani.”

Msichana aitwaye Nadia alikabili hali tofauti na hiyo. Anasema hivi: “Nilizaliwa Ujerumani. Kwa kuwa wazazi wangu ni Waitaliano, mimi huzungumza Kijerumani chenye lafudhi ya Kiitaliano na hivyo watoto shuleni wananiita ‘mhamiaji mjinga.’ Lakini ninapoenda Italia, ninajikuta nikizungumza Kiitaliano chenye lafudhi ya Kijerumani. Hivyo mimi hujihisi si Mwitaliano wala si Mjerumani. Kila ninakoenda mimi ni mgeni.”

Ni matatizo gani mengine ambayo watoto wa wahamiaji hukumbana nayo? Na wanawezaje kutumia hali hiyo vizuri?

Tofauti za Utamaduni na Lugha

Hata nyumbani huenda watoto wa wahamiaji wakaona utamaduni tofauti ukisitawi. Jinsi gani? Watoto hujifunza utamaduni mpya kwa urahisi kuliko wazazi wao. Kwa mfano, Ana alikuwa na umri wa miaka minane wakati familia yao ilipohamia Uingereza. Anasema: “Ilikuwa rahisi kwangu na kwa ndugu yangu kuzoea maisha ya London. Lakini ilikuwa vigumu sana kwa wazazi wangu ambao walikuwa wameishi kwa miaka mingi katika kisiwa kidogo cha Madeira, huko Ureno.” Voeun ambaye alikuwa na umri wa miaka mitatu wazazi wake walipohamia Australia kutoka Kambodia, anasema: “Wazazi wangu hawakuzoea utamaduni na mazingira mapya haraka. Mara nyingi Baba alikasirika kwa sababu sikuelewa mtazamo na njia yake ya kufikiri.”

Tofauti hiyo ya utamaduni ni kama mtaro unaowatenganisha vijana na wazazi wao. Kisha kama ukuta uliojengwa kando ya mtaro huo, huenda tofauti ya lugha ikagawa familia hata zaidi. Mgawanyiko huo huanza hasa wakati watoto wanapojifunza lugha mpya haraka kuliko wazazi wao. Nao huongezeka watoto wanapoanza kusahau lugha ya mama na inakuwa vigumu zaidi kuwasiliana.

Ian, ambaye sasa ana miaka 14, aliona mgawanyiko kama huo ukisitawi kati yake na wazazi wake walipohamia New York kutoka Ekuado. “Sasa mimi huzungumza Kiingereza zaidi kuliko Kihispania,” anasema. “Walimu wangu huzungumza Kiingereza, rafiki zangu huzungumza Kiingereza, nami huzungumza Kiingereza na ndugu yangu. Kichwa changu kimejaa Kiingereza nacho Kihispania kinapotea.”

Je, hali zako ni sawa na za Ian? Ikiwa familia yenu ilihama ulipokuwa mdogo, huenda hukutambua kwamba lugha yako ya mama ingeweza kukusaidia baadaye maishani. Kwa hiyo, huenda uliamua tu kuipuuza. Noor, aliyetajwa awali, anasema: “Baba yangu alisisitiza tuzungumze lugha yake nyumbani, lakini hatukutaka kuzungumza Kiarabu. Tuliona kuwa kujifunza Kiarabu ni mzigo. Rafiki zetu walizungumza Kiingereza. Vipindi vya televisheni vilikuwa katika Kiingereza. Kwa hiyo hatukuona sababu ya kujifunza Kiarabu.”

Kadiri umri unavyoongezeka huenda ukaanza kutambua faida za kuzungumza lugha ya mama vizuri. Hata hivyo, huenda ukaona ni vigumu kukumbuka maneno ambayo ulikuwa unaweza kuyasema kwa urahisi. “Mimi huchanganya lugha hizo mbili,” anasema Michael, aliye na umri wa miaka 13, ambaye wazazi wake walihamia Uingereza kutoka China. Ornelle mwenye umri wa miaka 15 ambaye alihamia London kutoka Congo (Kinshasa), anasema: “Mimi hujaribu kumwambia mama yangu jambo kwa lugha ya Lingala, lakini siwezi kwa kuwa nimezoea kuzungumza Kiingereza.” Lee, ambaye wazazi wake ni Wakambodia na alizaliwa Australia, anajuta kwa sababu hawezi kuzungumza lugha ya wazazi wake kwa ufasaha. Anaeleza: “Ninapotaka kuwafafanulia wazazi wangu maoni yangu kuhusu jambo fulani, siwezi kujieleza vizuri katika lugha yao.”

Sababu za Kukabiliana na Tatizo Hilo

Ikiwa umeanza kusahau lugha ya mama, usikate tamaa. Unaweza kuboresha uwezo wako wa kuizungumza. Lakini kwanza unapaswa kuona umuhimu wa kufanya hivyo. Je, kuna faida zozote? “Nilijifunza lugha ya mama kwa kuwa nilitaka kuwakaribia wazazi wangu kihisia, lakini hasa kiroho,” anasema Giosuè, aliyetajwa awali. “Kujifunza lugha yao kumeniwezesha kuelewa hisia zao. Na kumewasaidia kunielewa.”

Vijana wengi Wakristo wanajifunza lugha ya wazazi kwa kuwa wanataka kuwahubiria wahamiaji wengine habari njema ya Ufalme wa Mungu. (Mathayo 24:14; 28:19, 20) Salomão, ambaye alihamia London alipokuwa na umri wa miaka mitano anasema: “Kuna faida kubwa ya kuweza kueleza Maandiko katika lugha mbili! Nilikuwa karibu kusahau lugha ya mama, lakini kwa kuwa sasa niko katika kutaniko la Kireno, ninaweza kuzungumza Kiingereza na Kireno kwa ufasaha.” Oleg, mwenye umri wa miaka 15, ambaye sasa anaishi Ufaransa anasema: “Ninafurahia kuwasaidia wengine. Ninaweza kuwaeleza watu wanaozungumza Kirusi, Kifaransa, au Kimoldova kuhusu Biblia.” Noor, aliona kwamba kuna uhitaji wa wahubiri katika eneo la watu wanaozungumza Kiarabu. Anasema: “Sasa nimeanza kujifunza Kiarabu na ninajaribu kukumbuka maneno niliyosahau. Mtazamo wangu umebadilika. Sasa ninataka kusahihishwa ninapokosea. Ninataka kujifunza.”

Unaweza kufanya nini ili uweze kuzungumza tena lugha ya mama kwa ufasaha? Familia fulani zimeona kwamba wakizungumza lugha ya mama peke yake wakiwa nyumbani, watoto wao hujifunza lugha zote mbili vizuri. * Huenda pia ukawaomba wazazi wako wakusaidie kujifunza kuandika lugha hiyo. Stelios, ambaye amelelewa Ujerumani lakini lugha yake ya mama ni Kigiriki, anasema: “Wazazi wangu walizungumzia pamoja nami andiko la Biblia kila siku. Wangesoma andiko hilo kwa sauti, kisha ningeliandika. Sasa ninaweza kusoma na kuandika Kigiriki na Kijerumani.”

Kwa kweli, kuna faida kubwa ikiwa unafahamu tamaduni mbili na unaweza kuzungumza lugha mbili au zaidi. Kujua kwako tamaduni mbili huongeza uwezo wako wa kuelewa hisia za watu na kujibu maswali yao kuhusu Mungu. Biblia inasema: “Mtu hushangilia jibu la kinywa chake, nalo neno linalosemwa wakati unaofaa ni jema kama nini!” (Methali 15:23) Preeti, aliyezaliwa Uingereza na wazazi Wahindi, anaeleza: “Kwa kuwa ninaelewa tamaduni mbili, mimi hujihisi nikiwa na uhakika katika huduma. Ninawaelewa watu kutoka tamaduni zote mbili, yaani ninaelewa imani na mitazamo yao.”

“Mungu Hana Ubaguzi”

Ukihisi kwamba umevurugika kwa sababu ya kuishi katika tamaduni mbili, usivunjike moyo. Hali yako ni sawa na ya watu fulani wanaotajwa katika Biblia. Kwa mfano, Yosefu alihamishwa alipokuwa mvulana kutoka utamaduni wa Waebrania aliokuwa ameuzoea na kuishi Misri maisha yake yote. Lakini ni wazi kwamba hakusahau lugha ya mama. (Mwanzo 45:1-4) Kwa sababu hiyo, aliisaidia familia yake.—Mwanzo 39:1; 45:5.

Timotheo, ambaye aliandamana na mtume Paulo katika safari zake nyingi, alikuwa na baba Mgiriki na mama Myahudi. (Matendo 16:1-3) Badala ya kuruhusu malezi yake yawe kizuizi, alitumia ujuzi wake wa utamaduni mbalimbali kuwasaidia watu alipokuwa katika kazi yake ya umishonari.—Wafilipi 2:19-22.

Je, wewe pia unaweza kuona hali zako kuwa faida badala ya kizuizi? Kumbuka, “Mungu hana ubaguzi, bali katika kila taifa mtu ambaye anamwogopa na kutenda uadilifu anakubalika kwake.” (Matendo 10:34, 35) Yehova anakupenda jinsi ulivyo, bila kujali unatoka wapi. Je, wewe, kama vijana wengine waliotajwa kwenye makala hii, unaweza kutumia ujuzi na uzoefu wako kuwasaidia wengine walio na malezi kama yako kujifunza kuhusu Yehova, Mungu wetu mwenye upendo ambaye hana ubaguzi? Kufanya hivyo kunaweza kukuletea furaha nyingi!—Matendo 20:35.

Ili upate makala nyingine za “Vijana Huuliza . . .” unaweza kutembelea tovuti yetu ya mafundisho-biblia/matineja/uliza/

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 21 Kwa mapendekezo ya ziada, ona makala yenye kichwa “Kuwalea Watoto Katika Nchi ya Kigeni—Magumu na Thawabu,” iliyochapishwa katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Oktoba 15, 2002 (15/10/2002).

MAMBO YA KUFIKIRIA

▪ Ni vizuizi gani vya kitamaduni na lugha unavyokabiliana navyo?

▪ Unaweza kushindaje baadhi ya vizuizi hivyo?

[Picha katika ukurasa wa 20]

Kuzungumza lugha ya wazazi wako kunaweza kuimarisha kifungo cha familia