Mivinje—Jamii ya Miti Yenye Matumizi Mengi
Mivinje—Jamii ya Miti Yenye Matumizi Mengi
NA MWANDISHI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA CHEKI
MMOJA ni mwembamba na umenyooka na unaonekana mrefu sana. Ule mwingine umeinama na kichwa chake kimenyong’onyea. Ijapokuwa ina maumbile mbalimbali, yote ni ya jamii moja. Ni nini hiyo? Ni miti—mwerebi na mti unaoitwa weeping willow. Miti hiyo ni ya jamii ya mvinje.
Kwa kawaida, mivinje hupatikana kando ya mito na vijito. Katika Jamhuri ya Cheki, miti hiyo inanawiri kwenye maeneo yenye majimaji, ambako huchipuka haraka kutoka kwenye vitawi vidogo. Mivinje inaweza kufikia kimo cha zaidi ya mita 30. Inaweza kuwa na majani membamba yanayoning’inia kwenye matawi marefu yaliyonyooka. Au, inaweza kuwa na majani mapana kama ya shining willows na pussy willows.
Ingawa kuna spishi zaidi ya 350 za willow na mierebi, kuna spishi moja inayovutia sana inayoitwa weeping willow. Spishi nyingine inayoitwa goat willow, inajulikana kwa vishada vya maua vyenye manyoya-manyoya ambavyo huota kabla ya majani kutokea. Inasemekana kwamba vishada hivyo vinapotokea, majira ya kuchipua yatafuata.
Aina Nyingine za Mvinje
Mierebi hupatikana sana Bohemia, eneo ambapo Prague, jiji kuu la Jamhuri ya Cheki lipo. Kuna angalau spishi 35 za mierebi, na zote ni za jamii ya mvinje. Spishi inayopatikana sana ni ile inayoitwa black poplar, nayo hupatikana kandokando ya vijito na misitu yenye majimaji ya Bohemia. Aina moja ya spishi hiyo ni Lombardy au Italian poplar ambao una shina jembamba na matawi yanayoelekea juu ambayo hukua karibu sana na shina lenyewe. Mti huu maridadi unaweza kufikia kimo cha mita 35, urefu unaolingana na jengo lenye ghorofa 11! Mierebi hiyo inaweza pia kupatikana kandokando ya barabara nyingi, nayo hufanya mandhari ya vijijini ipendeze hasa wakati wa majira ya kupukutika majani yake yanapogeuka rangi na kuwa manjano nyangavu.
Pia aina nyingine ya mwerebi ni Aspen. Miti hiyo si mirefu sana na matawi yake ya juu ni myembamba. Mierebi hiyo ina sifa nyingine ya kipekee—majani yake hutetemeka yanapopulizwa hata na upepo mdogo.
Je, Mivinje Inatajwa Katika Biblia?
Huenda ukadhani kwamba mierebi haiwezi kukua sehemu za mbali sana za kusini kama Mashariki ya Kati. Hata hivyo, Biblia inasema kwamba Waisraeli walitundika vinubi vyao juu ya mierebi wakiwa huko Babiloni. (Zaburi 137:2) Kwa nini walifanya hivyo? Hata ingawa vinubi vilitumiwa kumsifu Mungu, Waisraeli wenye huzuni hawakufurahia kupiga vinubi vyao wakati huo wa taabu. (Isaya 24:8, 9) Neno la Mungu pia linataja mierebi kati ya miti ambayo matawi yake yalitumiwa kujenga vibanda wakati wa Sherehe ya Kukusanya. (Mambo ya Walawi 23:40) Kitabu cha Ayubu kinasema kwamba kiboko ambaye ni mnyama jasiri huishi kwenye vijito na “mierebi ya bonde la mto humzunguka.”—Ayubu 40:22.
Leo, willow na mierebi hutumiwa kutengenezea vifaa mbalimbali. Mierebi hutumiwa kutengenezea vinia, mbao laini, kreti, katoni na bidhaa mbalimbali za karatasi. Pia mti wa willow unathaminiwa kwa sababu ya matumizi yake mbalimbali. Mafundi stadi hutumia matawi yake yanayoweza kupindwa kwa urahisi kutengenezea vikapu na fanicha. Kwa kweli, mvinje ni jamii ya miti yenye matumizi mengi!
[Picha katika ukurasa wa 10]
Majani ya “aspen”
[Picha katika ukurasa wa 10]
“Weeping willow”
[Picha katika ukurasa wa 10]
“Lombardy poplar”
[Picha katika ukurasa wa 10]
“Goat willow”
[Picha katika ukurasa wa 10]
“Black poplar”