Kalipso Muziki wa Kitamaduni wa Trinidad
Kalipso Muziki wa Kitamaduni wa Trinidad
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI TRINIDAD
UNAPOSIKIA kuhusu Jamhuri ya Trinidad na Tobago, unafikiria nini? Wengi watafikiri kuhusu bendi za mapipa na muziki wenye kuvutia wa kalipso. Kwa kweli, midundo na mtindo wenye kuvutia wa kalipso unapendwa na watu wengi katika nchi nyingi mbali na mahali ulipoanzia, kusini katika Bahari ya Karibea. *
Kulingana na kitabu Calypso Calaloo, jina kalipso linaweza kumaanisha “wimbo wowote ambao baada ya mwaka wa 1898 uliimbwa wakati wa sherehe huko Trinidad, iwe unaimbwa mtaani na watu wanaosherehekea kwa kelele au katika majukwaa na waimbaji chipukizi na maarufu.” Huenda muziki wa kalipso ulichochewa na utamaduni wa Kiafrika wa kusimulia hadithi ulioingizwa Trinidad na watumwa Waafrika. Vivyo hivyo, mambo ambayo yalipendwa sana katika nyimbo, dansi, na upigaji ngoma za Kiafrika, pamoja na uvutano wa kitamaduni wa Wafaransa, Wahispania, Waingereza, na utamaduni mwingine, ulikuwa msingi wa kalipso.
Haijulikani mahali ambapo jina kalipso lilitoka. Wengine wanafikiri kwamba linatokana na neno kaiso la Afrika Magharibi, ambalo lilitumiwa kumsifu mtu alipofanya jambo vizuri. Hata kabla ya utumwa kuisha huko Trinidad na Tobago katika miaka ya 1830, umati ulikusanyika wakati wa sherehe za kila mwaka kusikiliza chantuelles (waimbaji) wakijitukuza na kudhihakiana wanapoimba. Ili kujitofautisha na waimbaji wengine, kila mwimbaji wa kalipso alikuwa na jina la utani la jukwaani na mtindo wake mwenyewe.
Mtindo na Uvutano Wake
Waimbaji wa kalipso wameheshimiwa sikuzote kwa sababu ya werevu wao. Isitoshe, waimbaji wengi wa kalipso wamesitawisha uwezo wa ajabu wa kutokeza mistari kadhaa ya muziki unaopatana bila kujitayarisha, mara nyingi wakiiunganisha na ufafanuzi unaopatana kabisa na
wimbo. Mwanzoni, waimbaji wa kalipso hasa walikuwa wakaaji wa Trinidad wenye asili ya Kiafrika na watu wa jamii maskini, lakini leo waimbaji wanatoka katika jamii, rangi, na tabaka zote.Dakt. Hollis Liverpool, aliyekuwa msimamizi wa utamaduni huko Trinidad na Tobago, ni mwanahistoria na mwimbaji wa kalipso. Alimwambia hivi mwandishi wa Amkeni! kuhusu waimbaji wa mapema wa kalipso: “Jambo zuri kuwahusu ni kwamba walipenda ucheshi, kwani watu walihudhuria maonyesho [ya kalipso] hasa ili watumbuizwe, wasikie uvumi, na wathibitishe mambo waliyokuwa wamesikia. Watu wa tabaka la juu walikuja kusikia mambo ambayo watu wa matabaka ya chini walikuwa wakifanya, naye gavana na watu wengine wenye mamlaka walikuja ili wajue uvutano wao wa kisiasa ulikuwa mkubwa kadiri gani.”
Mara nyingi, waimbaji wa kalipso waliwadhihaki watu wenye mamlaka na wa tabaka la juu katika jamii. Kwa sababu hiyo, waimbaji wa kalipso walionwa kuwa mashujaa na watetezi wa watu wa kawaida, lakini wenye mamlaka waliwaona kuwa watu wanaozusha ghasia. Nyakati nyingine waimbaji wa kalipso walitunga nyimbo zenye kuchambua sana hivi kwamba serikali ya kikoloni ikachochewa kutunga sheria zilizokusudiwa kuwadhibiti. Waimbaji walianza kutunga nyimbo zenye maana mbili, nao wakaboresha sana ujuzi huo. Hadi leo, nyimbo zenye maana mbili ni alama ya muziki wa kalipso.
Waimbaji wa kalipso hawakutumia tu lugha bali waliibuni. Kwa kweli, wamechangia sana kuongezwa kwa maneno katika lugha ya kienyeji ya West Indies. Haishangazi basi kwamba watu wengi, kutia ndani wanasiasa, huwanukuu mara nyingi waimbaji wa kalipso ili kukazia jambo fulani.
Kalipso ya Kisasa
Katika nyakati za karibuni, mitindo tofauti ya kalipso imebuniwa ambayo huwavutia watu walio na mapendezi mbalimbali ya muziki. Kama tu miziki mingi, maneno ya nyimbo fulani za kalipso hazipatani na kanuni za juu za maadili. Kwa wazi, ni jambo la hekima kuchagua ni maneno ya aina gani tutasikiliza. (Waefeso 5:3, 4) Huenda tukajiuliza, ‘Je, ninaweza kuogopa kuelezea watoto wangu au msikilizaji mwingine maneno fulani katika nyimbo zenye maana mbili?’
Bila shaka, ukitembelea Trinidad na Tobago, utafurahia fuo na matumbawe maridadi na mchanganyiko wa jamii na utamaduni mbalimbali wa visiwa hivyo. Na huenda pia ukafurahia bendi za mapipa na muziki wa kalipso, muziki wenye kusisimua na kuvutia ambao umenasa fikira za vijana kwa wazee ulimwenguni pote.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Mara nyingi bendi za mapipa hucheza muziki wa kalipso, lakini kawaida mwimbaji wa kalipso huandamanisha muziki wake kwa vifaa kama vile gitaa, tarumbeta, saksafoni, na ngoma.
[Picha katika ukurasa wa 25]
Ngoma za mapipa