Jinsi Unavyoweza Kutunza Meno Yako
Jinsi Unavyoweza Kutunza Meno Yako
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KANADA
UNAPOJIANGALIA kwenye kioo, wewe hutazama nini? Labda wewe hutazama nywele zako au sehemu nyingine ya uso wako. Lakini namna gani meno yako? Je, umetambua kwamba jinsi ambavyo wewe hutabasamu hutegemea hasa meno yako? Naam, ikiwa unajali tabasamu yako, utatunza meno yako. Meno ya mtu mzima yanapaswa kudumu muda wote wa maisha yake. Yanapaswa kutunzwa vizuri. Mbali na kutafuna chakula na kukusaidia kuzungumza kwa njia nzuri, meno yako hutegemeza midomo na mashavu yako na hivyo kuboresha tabasamu yako na kuifanya ivutie. Kwa kweli, meno yako ni muhimu sana!
Unaweza Kutunzaje Meno Yako?
Meno yenye afya hutegemea chakula unachokula. Lishe bora yenye kalisi na vitamini A, C, na D husaidia meno yakue tangu wakati mtu anapokuwa tumboni hadi meno yanapokomaa. * Kula chakula kinachofaa kutakusaidia uwe na meno yenye afya, lakini jihadhari na vyakula vyenye sukari nyingi! Vitafanya iwe rahisi zaidi meno kuoza. Licha ya maonyo mengi yanayotolewa kuhusu jinsi vyakula vyenye sukari vinavyochangia kuoza kwa meno, inasemekana kwamba mkaaji wa Amerika Kaskazini hula kilo 50 hadi 60 za sukari kila mwaka! Kwa nini sukari inaweza kuharibu meno yetu?
Kuoza kwa meno husababishwa na aina mbili za bakteria, yaani, “streptococci na lactobocilli” ambazo hutokeza ukoga, ambao ni utando mwembamba wa bakteria na mabaki ya chakula ambayo hukwama kwenye meno. Bakteria hizo hula sukari na kuigeuza kuwa asidi zinazodhuru ambazo hufanya meno yaoze. Aina fulani za sukari hugeuzwa haraka kuwa asidi au hukwama kwenye meno kwa urahisi, na hivyo kuzipa bakteria hizo muda wa kufanya meno yaoze. * Ukoga ambao hauondolewi unaweza kuwa mgumu kuzunguka fizi.
Kudhibiti ukoga na hasa bakteria za streptococci ni muhimu ili kuzuia meno yasioze. Kwa hiyo, ikiwa ungependa kutunza meno yako, ni lazima usafishe kinywa chako kila siku. Chuo Kikuu cha Upasuaji wa Meno na Kinywa huko Columbia kinasema hivi: “Kuondoa uchafu katikati ya meno kwa kutumia uzi mwembamba
pamoja na [kupiga mswaki] ndiyo njia muhimu zaidi ya kudumisha afya ya meno yako na sehemu nyingine zinazoyashikilia.” Picha kwenye ukurasa huu na unaofuata inaonyesha njia moja inayofaa ya kupiga mswaki na kuondoa uchafu katikati ya meno. Daktari wa meno anaweza kupendekeza vifaa na mbinu nyingine ambazo zitakusaidia kusafisha na hivyo kutunza meno yako ifaavyo.Jino linaposhambuliwa mara nyingi na asidi, madini huondolewa na kunakuwa na matundu madogo sana kwenye tabaka ngumu ya juu ya meno. Hata hivyo, kila siku madini hayo hurudishwa tena. Jinsi gani? Imethibitishwa kwamba floraidi hutumika kuzuia kuoza kwa meno kwa kusaidia kurudisha madini yaliyoondolewa. Kwa hiyo, ingawa kuoza kunaweza kuenea katika sehemu nyingine za meno, jambo hilo linaweza kuzuiwa na vitu, kama vile floraidi. Naam, meno yanaweza kujiponya!
Utazamie Nini Unapoenda kwa Daktari wa Meno?
Katika uchunguzi ambao watu waliulizwa wao huogopa nini zaidi, woga wa kwenda kwa daktari wa meno ulichukua nafasi ya pili baada ya woga wa kuzungumza mbele ya umati. Je, inafaa kuwa na woga huo? Katika nchi tajiri, kekee, au mashini ndogo inayozunguka kwa kasi, na dawa za kutia ganzi za kujipaka na za sindano huwasaidia madaktari wa meno kufanya kazi nyingi bila kumfanya mgonjwa ahisi uchungu mwingi. Kufahamu kinachohusika katika kila hatua ya matibabu kunaweza kupunguza woga wako.
Unapoenda kwa daktari wa meno, huenda akasafisha au kukwangua meno yako. Anapofanya hivyo, ukoga huondolewa kwenye sehemu zisizoweza kufikika kwa mswaki na nyuzi. Meno husafishwa na kung’arishwa ili kuzuia ukoga na kuondoa madoa ambayo huharibu tabasamu yako.
Imegunduliwa kwamba madini ya floraidi hupunguza hatari ya kuoza kwa meno, na katika nchi nyingi, mara nyingi madaktari wa meno hupaka madini hayo kwenye meno ya watoto. Katika nchi nyingi pia, madini ya floraidi hutiwa katika maji, na mara nyingi dawa za meno huongezwa floraidi ili kuzuia meno yasioze.
Daktari wa Meno Anaweza Kufanya Nini?
Madaktari wa meno wanazidi kuzoezwa mbinu za kuzuia kuharibika kwa meno madini yanapoondolewa. Mara nyingi kuoza kwa meno kunaweza kuzuiwa kwa kuziba matundu yanapokuwa bado madogo sana. Kwa hiyo, unapoenda kwa daktari wa meno mapema, unaweza kufurahia matibabu ya meno.
Hata hivyo, asidi inayotokezwa na ukoga ikibaki kwenye meno, meno huanza kuoza. Meno hayo yasipotibiwa, huenda yakawa na matundu. Jino lililo na tundu litahitaji kutibiwa. Ikiwa halijaoza hadi sehemu zenye neva, basi kwa kawaida sehemu iliyooza huondolewa na tundu kuzibwa.
Daktari hutumia kekee kuondoa sehemu iliyooza na kusafisha tundu hilo kisha huliziba. Mchanganyiko wa madini ya zebaki, fedha, na bati unaotumiwa kuziba matundu ya meno huwa mgumu haraka na hushindiliwa ili uenee kwenye tundu lote. Michanganyiko mingine hufanywa iwe migumu kwa kutumia mashini ndogo inayotoa nuru ya buluu. Matundu yasipotibiwa na sehemu zenye neva zianze kuoza, huenda mizizi ikahitaji kuondolewa au hata jino kung’olewa. Kuondolewa kwa mizizi kunaweza kuzuia jino lising’olewe, kwani matibabu hayo huhusisha kujaza na kuziba sehemu ya ndani ya jino. Sehemu ya juu ya meno yaliyoharibika sana hufunikwa kwa vifuniko, au meno bandia yanaweza kutumiwa jino linapong’olewa. *
Kwa Nini Inafaa Kumwona Daktari wa Meno?
Labda bado unaogopa kumwona daktari wa meno. Ikiwa ndivyo, mweleze daktari wa meno wasiwasi wako. Kabla ya matibabu kuanza, kubalianeni ishara utakayotoa (kama vile kuinua mkono) unapohisi uchungu. Mwombe akueleze kinachohusika katika kila hatua ya matibabu. Unaweza kumsaidia mtoto wako awe na meno yenye afya kwa kuwasifu madaktari wa meno na anapokosea, usitishe kumwadhibu kwa kumpeleka kwa daktari wa meno.
Dakt. Daniel Kandelman, profesa wa Idara ya Afya ya Kinywa katika Chuo Kikuu cha Montreal, anasema hivi: “Siku hizi inawezekana kufikia mradi huu wa afya ya meno: tunza meno yako ya asili, utakuwa na tabasamu yenye kuvutia maisha yako yote.” Kufanya hivyo kuna manufaa!
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Jino lililokomaa kabisa huonyesha chakula ambacho mama alikuwa akila alipokuwa mjamzito na wakati mtoto alipokuwa mchanga meno yakikua ndani ya fizi. Hatua ya ukuzi hukoma mtoto anapokuwa tineja au anapofikia umri wa miaka ishirini na kitu.
^ fu. 6 Wataalamu wa meno wamegundua kwamba sukari ya asili inayoitwa xylitol, imesaidia kudhibiti ukoga unaofanya meno yaoze. Chingamu fulani zina sukari hiyo ya xylitol.
^ fu. 16 Kwa habari zaidi kuhusu meno bandia, ona makala yenye kichwa “Je, Wewe Wahitaji Meno Bandia?” katika gazeti la Amkeni! la Februari 22, 1993, ukurasa wa 18-20.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 12]
Kupiga Mswaki
Kuna njia mbalimbali za kupiga mswaki lakini uwe mwangalifu, tumia tu kiasi kidogo cha dawa ya meno. Dawa ya meno hukwaruza na inaweza kuwa “ngumu mara nyingi zaidi kuliko jino.”
1 Pinda mswaki kidogo kutoka kwenye mwisho wa fizi. Kwa utaratibu, piga mswaki kutoka kwenye fizi kwenda chini. Hakikisha kwamba umepiga mswaki sehemu zote za meno, ndani na nje.
2 Piga mswaki polepole kwenye sehemu za meno za kutafunia.
3 Ili usafishe sehemu ya ndani ya meno ya mbele, shikilia mswaki wima. Piga mswaki kutoka kwenye fizi hadi kwenye sehemu ya kutafunia.
4 Piga ulimi mswaki na sehemu ya juu ya kinywa.
[Hisani]
Steps 1-4: Courtesy www.OralB.com
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]
Kutoa Uchafu Katikati ya Meno kwa Uzi Mwembamba
Madaktari wa meno hupendekeza kwamba mtu atoe uchafu katikati ya meno kwa kutumia uzi kila siku na apige mswaki kila baada ya kula.
1 Zungusha uzi kwenye kidole cha katikati cha kila mkono, na uache sehemu ndogo ya uzi katikati ya vidole hivyo.
2 Kwa kutumia kidole cha gumba cha mkono mmoja na kidole cha shahada cha mkono ule mwingine, shikilia uzi kwa nguvu. Fanya ni kana kwamba unausugua uzi huo katikati ya meno ili uweze kupita.
3 Pinda uzi huo katika umbo la C, na kuuvuta juu na chini ili usafishe pande za kila jino. Pitisha uzi taratibu chini ya fizi, lakini usifinye uzi wenyewe kwenye fizi wala usiuvute karibu na fizi.
[Hisani]
Chanzo: The Columbia University School of Dental and Oral Surgery’s Guide to Family Dental Care
Steps 1-3: Courtesy www.OralB.com