Maua ya Mcheri Yenye Petali Zinazovutia Tangu Zamani
Maua ya Mcheri Yenye Petali Zinazovutia Tangu Zamani
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Japani
TANGU nyakati za kale Wajapani wamesifu sana uzuri wa sakura, yaani, mcheri wa Japani unaochanua. Petali zake zinavutia sana hivi kwamba maua ya mcheri yamekuwa maarufu zaidi kuliko maua mengine, nayo yamekuwa sehemu muhimu katika historia na utamaduni wa Japani. Kwa kweli, katika maeneo fulani, neno “maua” katika Kijapani humaanisha sakura. Kwa zaidi ya miaka elfu moja, Wajapani wameyaona maua ya mcheri kuwa yenye thamani.
Unaweza kuona micheri kotekote katika visiwa vya Japani. Hutalazimika kusafiri mbali ili uone moja kati ya aina 300 hivi zinazokuzwa huku. Kila ua huwa na petali tano zenye mikato kwenye miisho yake, ingawa aina fulani zina petali nyingi zaidi. Maua kadhaa hufanyiza kichala kimoja. Petali hizo huwa na rangi mbalimbali kama vile nyeupe, waridi, na hata nyekundu kutia ndani rangi nyingine zinazokaribiana na hizo. Kwa muda mrefu umbo na rangi ya maua hayo zimehusianishwa na utakato na usahili.
Mtu huvutiwa kutazama mcheri uliochanua maua kabisa. Mcheri unapopigwa na nuru ya jua inayotoka kwenye mawingu, petali zake hung’aa kwa rangi ya waridi-nyeupe. Miti mingi ya cheri huvutia hata zaidi inapokua karibukaribu.
Ni Maridadi Kutazama
Tangu nyakati za kale, Milima ya Yoshino imekuwa maarufu kwa sababu ya micheri inayochanua maua meupe. Eneo hilo lina misitu minne mikubwa yenye micheri zaidi ya 100,000. Sehemu moja ya misitu hiyo inaitwa Hitome Senbon, kumaanisha ‘micheri elfu moja inayoweza kuonekana kwa wakati mmoja.’ Kihalisi maua meupe huangaza pande zote za mlima huo na kufanya uonekane kwamba umefunikwa na theluji. Basi haishangazi kwamba kila mwaka, zaidi ya watu 350,000 hutembelea eneo hilo ili kuona umaridadi huo wenye kutokeza!
Ikitegemea jinsi ambavyo imepandwa, micheri inaweza kutokeza mambo yenye kupendeza. Kwa mfano, micheri inapopandwa katika safu sambamba ambayo matawi yake hugusana, hiyo hufanyiza ‘njia yenye paa ya nusu duara.’ Hebu wazia vichala vingi vya micheri vikiwa juu ya kichwa chako, na kufanyiza mwamvuli wa rangi ya waridi-nyeupe, huku ukikanyaga petali nyingi zilizomwagika chini.
Hata hivyo, maua hayo hayadumu kwani hayo hunyauka baada ya siku mbili au tatu. Yanaweza kunyauka upesi zaidi ikitegemea hali ya hewa.
Hanami—Tafrija Chini ya Micheri
Maua ya kwanza huanza kuchanua kusini mwa kisiwa cha Japani, huko Okinawa mwezi wa Januari, nayo huendelea kuchanua hatua kwa hatua kuelekea kaskazini huko Hokkaido mpaka mwishoni mwa mwezi wa Mei. Kwa ukawaida, televisheni, redio, magazeti, na hata
Intaneti huripoti ni wapi micheri inachanua. Watu wengi wanapopata habari kuhusu mahali ambapo micheri ya Japani imechanua, wao huenda huko ili kuiona.Desturi ya hanami, au “kutazama maua” ni ya zamani sana. Na ua ambalo watu hutazama ni la mcheri. Katika enzi ya Heian (794 hadi 1185), wakuu walifanya karamu ili kufurahia ua hilo. Mnamo 1598, mbabe wa vita aliyeitwa Hideyoshi Toyotomi alifanya karamu ya kutazama maua ya mcheri katika hekalu la Daigoji mjini Kyoto. Watu wote wenye nguvu waliomiliki mashamba pamoja na wageni waheshimiwa walikusanyika chini ya miti iliyochanua na kukariri mashairi yaliyosifu micheri iliyochanua. Wanawake walivaa mavazi yaliyokuwa na michoro yenye kuvutia ya ua hilo linaloitwa sakura.
Katika enzi ya Edo (1603 hadi 1867), watu wa kawaida walianza kuiga tafrija hizo zilizofanywa chini ya micheri iliyochanua. Walikula, wakanywa, wakaimba, na kucheza dansi huku wakitazama maua hayo yaliyochanua wakiwa pamoja na familia zao na marafiki wao. Watu wanaendelea kufuata desturi maarufu ya hanami hadi leo, wengi wao wakienda mahali pasipo na watu wengi ili wafurahie kutazama petali za micheri zenye kuvutia.
Mtindo Wenye Kujirudia-rudia
Kwa muda mrefu, sakura imekuwa sehemu muhimu ya historia na utamaduni wa Japani. Hiyo hupatikana
sana katika fasihi, mashairi, maigizo, na muziki wa Japani. Kwa karne nyingi, wasanii wamechora maua ya micheri juu ya vyombo vya udongo na kwenye visitiri vya kukunjwa.Mashujaa wa vita Wajapani wanaoitwa samurai, pia walianza kufuata desturi ya sakura. Kwa kuwa walijitoa kabisa kwa bwana wao, walitazamiwa kutoa uhai wao wakati wowote. Samurai waliona jinsi maisha yalivyo mafupi walipotazama maua ya mcheri. Kitabu Kodansha Encyclopedia of Japan kinasema hivi kuhusu jambo hilo: “Kwa kuwa maua ya mcheri huchanua kwa muda mfupi sana kisha yanatawanyika, yamekuwa pia mfano unaofaa wa urembo unaopendwa na Wajapani, yaani, umaridadi usiodumu kwa muda mrefu.”
Leo bado watu hupendezwa na maua ya micheri nchini kote. Mara nyingi, vazi la kimono lenye kupendeza lina michoro ya maua ya micheri. Umbo hilo la sakura linaweza kuonekana pia katika vyombo vya nyumbani, skafu, na mavazi mengine. Ua hilo linapendwa sana hivi kwamba wazazi hujivunia kuwaita mabinti zao warembo Sakura, kutokana na maua ya mcheri.
Ingawa ni rahisi kuharibika, ua la mcheri lina uwezo wa kuathiri utamaduni wa nchi nzima, nalo ni mfano bora wa vitu vyenye kupendeza ambavyo Muumba wetu ametokeza.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]
Micheri Iliyokomaa
Mbao nzuri za micheri zinaweza kutumiwa kutengeneza vinyago, fanicha, na kuchapisha. Lakini si mambo hayo tu ambayo yamefanya mcheri uwe mti wa pekee nchini Japani. Wala haijawa maarufu kwa sababu ya matunda yake. Tofauti na micheri inayokua katika sehemu nyingine za ulimwengu, mti wa cheri wa Japani hukuzwa hasa kwa sababu ya maua yake ambayo yanapendwa na watu wengi sana.
Micheri inaweza kupandwa kwa urahisi kwa kutumia mbegu zake. Hivyo, micheri imepandwa kando ya mito na barabara kuu na vilevile katika bustani nyingi kotekote nchini.
[Sanduku katika ukurasa wa 15]
Kupukutika kwa Maua ya Mcheri
Wakati petali za micheri zinapopukutika, kunakuwa na mandhari yenye kuvutia ya rangi ya waridi. Bila kutarajia, petali huanguka kutoka kwenye matawi. Upepo wenye nguvu unaweza kupukutisha petali hizo na kuzitawanya. Wajapani huita jambo hilo sakura fubuki, au kupukutika kwa maua ya mcheri. Ni kama ardhi hufunikwa na mkeka mzuri wa rangi ya waridi. Ni mandhari chache tu zinazoweza kuwa zenye kuvutia kama petali hizo zilizopukutika.
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
“Hanami”—tafrija chini ya micheri iliyochanua
[Picha katika ukurasa wa 17]
‘Njia yenye paa ya nusu duara ya micheri’