Dunia Inaharibiwa
Dunia Inaharibiwa
KATIKA mwaka wa 1805, wavumbuzi mashuhuri Meriwether Lewis na William Clark walifika kwenye Mto Columbia ambao sasa uko katika Jimbo la Washington, Marekani. * Zaidi ya kuvutiwa na mto wenyewe, walivutiwa hasa na wingi wa samaki wa samoni waliokuwemo. Waliandika hivi katika kitabu chao cha safari: “Samaki hawa ni wengi ajabu. Wao huelea kwa wingi kupatana na mkondo wa mto, na husukumwa ufuoni, hivi kwamba Wahindi huhitaji tu kuwaokota, kuwapasua, na kuwakausha kwenye majukwaa ya mbao.” Ama kweli, samoni hao walikuwa wengi sana hivi kwamba Wahindi waliwakausha na kuwatumia kama kuni!
Sasa mambo yamebadilika. Gazeti Newsweek linaripoti hivi: “Kwa zaidi ya miaka kumi, wanasayansi wamefahamu kwamba idadi ya samaki wanaovuliwa ni kubwa kuliko ya wanaozaliwa.” Kwa mfano, inakadiriwa kwamba samoni walio katika Bahari ya Atlantiki Kaskazini wamepungua kwa asilimia 90.
Lakini si samaki tu wanaoendelea kupungua. Mali za asili, kama vile makaa ya mawe, mafuta, madini, na misitu, zinatumiwa kupita kiasi. Hazina ya Wanyama wa Pori Ulimwenguni inaripoti kwamba kati ya mwaka wa 1970 na 1995, mali za asili za dunia zilipungua kwa asilimia 30. Matumizi ya mali za asili za dunia yameleta faida na hasara, kwa kuwa mbinu zinazotumiwa kukusanya mali hizo zinaweza kuharibu mazingira.
Watu fulani husema kwamba kwa kuwa wanadamu ndio waliosababisha matatizo hayo, basi wanaweza kuyatatua. Kwa mfano, hivi karibuni uchafuzi wa hewa umepungua katika majiji mengi yenye viwanda. Je, hilo linaonyesha kwamba wanadamu wanatatua matatizo hayo?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Lewis na Clark walikuwa wametumwa kuchunguza na kuchora ramani ya eneo ambalo lilikuwa limenunuliwa karibuni huko magharibi ya Mto Mississippi.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
© Kevin Schafer/CORBIS