Huwafaidi Sana Wakulima wa Sertão
Huwafaidi Sana Wakulima wa Sertão
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI
INAKADIRIWA kwamba kuna mbuzi milioni kumi katika sertão *, ambalo ni eneo kame lenye ukubwa wa kilometa 1,100,000 za mraba, kaskazini-mashariki mwa Brazili. Kila mwaka kwa kipindi cha miezi tisa, anga la eneo hilo hukosa mawingu, kunakuwa na joto jingi, hewa huwa nzito, na mchanga huwa mgumu kama jiwe. Mito yake hukauka, majani ya miti hupukutika, kunakuwa na upepo mkavu wenye joto, nayo mifugo hurandaranda ikitafuta mimea yoyote inayoweza kula.
Hata hivyo, inaonekana kwamba mbuzi wa Brazili hawaathiriwi na ukame huo. Wakati hali mbaya ya ukame inapokumba eneo hilo, idadi ya ng’ombe na kondoo hupungua, lakini idadi ya mbuzi huongezeka. Ni nini huwawezesha mbuzi kustahimili hali hiyo ngumu?
Vinywa Vilivyobuniwa Ili Kukabiliana na Magumu
Watu wengi wanaoishi huko sertão husema kwamba mbuzi wanaweza kula chochote, kutia ndani viatu, sapatu, hata nguo. Profesa João Ambrósio, ambaye ni mtafiti katika Kituo cha Kitaifa cha Utafiti Kuhusu Mbuzi cha Sobral, huko kaskazini-mashariki mwa Brazili, anasema kwamba mbuzi wanaweza kuendelea kuishi kwa kula vitu visivyoweza kumeng’enywa kama vile mizizi, majani makavu, na maganda ya zaidi ya aina 60 za mimea. Mifugo mingine kama vile ng’ombe hula hasa nyasi.
Ni kweli kwamba mbuzi hufanikiwa kustahimili hali kwa sababu ya kula vyakula vyovyote bila kubagua. Wao hufanikiwa hasa kwa sababu ya midomo yao. Ambrósio anasema kwamba ng’ombe hutumia ulimi kuchukua chakula na hivyo hawawezi kuuma jani moja au ganda la mmea. Hata hivyo, mbuzi hutumia vinywa vyao vidogo, midomo inayonyumbulika, na meno makali kuuma na kula sehemu zenye lishe zaidi za mmea. Kwa kuwa mbuzi wanaweza kutafuta, kuuma, na kula mimea yoyote inayopatikana, watu husema kwamba mbuzi huharibu mimea. Ambrósio anasema hivi: “Mwanadamu ndiye aliyesababisha hali mbaya zinazomlazimu mbuzi kutenda hivyo. Mbuzi anajaribu tu kuokoa uhai wake.”
Ufugaji wa Mbuzi Huleta Faida
Haishangazi kwamba wakulima wa sertão huona kuwa ni muhimu sana kwao kufuga mbuzi wa asili ambao wanaweza kustahimili magumu. Mbuzi hao huwa chanzo muhimu cha chakula chenye protini kwa familia nyingi. Kwa kuwa nyama ya ng’ombe yaweza kuwa bei ghali, watu wengi hula nyama ya mbuzi iliyokaangwa au kuchemshwa na buxada (matumbo ya mbuzi yaliyojazwa nyama ya utumbo
na wali). Watu wanaweza kuuza ngozi ya mbuzi kwenye viwanda vya ngozi ili wapate pesa za ziada. Kwa hiyo, wakati wa dharura mbuzi wanaweza kuuzwa ili kupata pesa za kununua dawa au vitu vingine vya lazima.Faida nyingine ya mbuzi ni kwamba wao hujitafutia chakula. Wakati wa mchana, mbuzi hula pamoja wakiwa katika maeneo yasiyo na ua ya misitu ya miiba inayoitwa caatinga. Giza linapoingia, mbuzi hutambua sauti ya mchungaji wao, nao hurudi kwenye mazizi yao. Mkulima hujishughulisha nao wakati wa kuzalisha unapofika, kwa kuwa wakati huo yeye huchagua mbuzi atakaochinja, huwatibu walio wagonjwa, na kuwatia alama mbuzi wachanga. Kwa kuwa ni rahisi kufuga mbuzi, wakaaji wa mjini hufuga mbuzi wachache nyumbani kwao, au wanawaacha warande-rande mjini hata ikiwa sheria za eneo haziruhusu jambo hilo. Si ajabu kuona mbuzi akila katikati ya mji.
Baada ya kufuga mbuzi kwa karne kadhaa, imeonekana kwamba hilo huleta faida hasa kwa wakulima wadogo. Kazi ambayo mtu anahitaji kufanya na ardhi inayohitajiwa ili kufuga ng’ombe mmoja, ni sawa na ile inayohitajiwa ili kufuga mbuzi wanane. Kwa mfano, ikiwa mkulima ana ng’ombe watano, na mmoja afe, mkulima huyo atakuwa amepoteza asilimia 20 ya mifugo yake. Lakini vipi ikiwa angefuga mbuzi 40 badala ya ng’ombe 5? Angehitaji kuwa na kiasi kilekile cha ardhi na kufanya kiasi kilekile cha kazi. Ikiwa mbuzi mmoja angekufa, hiyo ingekuwa hasara ya asilimia 2.5 tu. Hiyo ndiyo sababu inayofanya familia milioni moja hivi nchini Brazili zifuge mbuzi ili kujitegemeza wakati wa ukame.
Sababu ya Kufanya Kazi kwa Bidii
Baadhi ya makundi makubwa zaidi ya mbuzi hupatikana katika Jimbo la Bahia, na mengine huwa na maelfu ya mbuzi. Inasemekana kwamba huko Uauá, ambao ni mji mdogo ulio kilometa 800 hivi kutoka kwenye jiji kuu, idadi ya mbuzi imezidi ile ya wakaaji kwa mara tano. Jamii nzima hutegemea ufugaji wa mbuzi na kazi nyingine zinazohusiana na ufugaji huo. Wakaaji hupenda kusema hivi kwa mzaha: “Huku Uauá mbuzi ndio wanaowafuga watu, wala si watu wanaowafuga mbuzi.”
Mbuzi huanza kuzaliwa katika mwezi wa Mei, miezi mitano hivi baada ya kipindi cha kuzalisha kuanza. Wachungaji wa mbuzi wenye bidii hufanya kazi kuanzia saa kumi usiku hadi saa moja jioni, wakiwakusanya, kuwanywesha, kuwatafuta, na kuwaokoa mbuzi wachanga waliopotea na walio hatarini. Wachungaji wenye ustadi hufunga na kukamua mamia ya mbuzi-jike kila siku ili mbuzi wachanga wasinywe maziwa kupita kiasi na kufa. Pia mbuzi hutibiwa majeraha na jitihada hufanywa kuzuia uvamizi wa wadudu wanaoitwa pange ambao hutoboa mashimo madogo kwenye ngozi ya mbuzi na hivyo kupunguza thamani ya ngozi yake.
Wachungaji hawatunzi mbuzi kwa njia hiyo kwa sababu tu wanawapenda, bali pia
kwa sababu wanapata faida fulani. Njia ya kawaida inayotumiwa huko Uauá na maeneo mengine ya mashambani kuwalipa wachungaji huitwa quarteação (robo), nayo huwafaidi wachungaji wenye bidii. Wachungaji hupewa mbuzi mmoja kwa kila mbuzi wanne wanaozaliwa katika kipindi cha kuzalisha. Mwenye mbuzi akiwa mkarimu yeye huwapa wachungaji wake mbuzi mmoja kwa kila mbuzi watatu wanaozaliwa. Kila mbuzi mchanga hupewa namba, kisha namba hizo hutiwa katika kikombe na wachungaji huruhusiwa kuchukua namba fulani kati ya namba hizo. Kwa kuwa kuna uwezekano wa kuchukua namba inayowakilisha mnyama yeyote, awe ni mlemavu, mwenye afya, mwembamba, au aliyenona, mchungaji huwachunga mbuzi wote vizuri kana kwamba ni mali yake.Kufaidika Zaidi Kutokana na Mbuzi wa Asili
Mbuzi wa Brazili wamezalishwa kutokana na mbuzi walioletwa na Wazungu mapema katika miaka ya 1500. Hata hivyo, kawaida mbuzi wa Brazili ni wadogo zaidi na hutoa kiasi kidogo sana cha maziwa kwa kulinganishwa na mbuzi walioletwa kutoka Ulaya.
Kwa mfano, mbuzi wa Brazili anayeitwa canindé hutoa chini ya lita moja ya maziwa kwa siku, na kwa upande mwingine mbuzi wa jamii hiyo huko Ulaya hutoa lita 3.8 za maziwa. Kwa miaka mingi, wakulima wengi na wataalamu wa mimea wametaka sana kuzalisha mbuzi anayeweza kustahimili magumu kama yule wa Brazili na vilevile kutoa maziwa mengi kama yule wa Ulaya. Hivyo, mbuzi huyo ambaye hufafanuliwa kuwa “ng’ombe wa maskini” atakuwa kama dhahabu kwa mkulima wa sertão.
Mbuzi wakubwa wanaotoa maziwa mengi wamezalishwa kwa kuchanganya mbegu za mbuzi wa Brazili na za yule wa Ulaya. Shirika fulani la utafiti wa kilimo katika Jimbo la Paraíba lililo kaskazini-mashariki mwa Brazili, lilizalisha mbuzi kwa kuchanganya mbegu za mbuzi wa Brazili na mbegu za mbuzi wa Italia, Ujerumani, na Uingereza. Mbuzi waliozalishwa walikuwa wakubwa zaidi, waliweza kustahimili hali katika maeneo makavu, na kutoa maziwa mengi zaidi. Mbuzi waliozalishwa kutokana na wale waliokuwa wakitokeza chini ya lita moja ya maziwa kwa siku, hutokeza kati ya lita 2.2 na 3.8.
Kituo cha utafiti huko Sobral kimefanya uvumbuzi ambao haugharimu pesa nyingi. Watafiti waligundua kwamba mbuzi hupenda kula majani ya miti fulani. Hata hivyo, mbuzi wangeweza tu kula majani hayo wakati ambapo miti ingeacha kukua na majani kupukutika. Ili kuwawezesha mbuzi kupata majani mengi, matawi ya juu ya miti fulani yalikatwa. Hilo lilifanya miti itokeze matawi katika sehemu za chini, ambapo mbuzi wangeweza kufikia. Ikawaje? Uzito wa mbuzi waliolisha katika sehemu iliyokuwa na miti hiyo uliongezeka mara nne.
Licha ya mavumbuzi hayo, huenda watu wanaofuga mbuzi wachache wakakabili tatizo lingine ambalo haliwezi kusuluhishwa na sayansi. Tatizo gani? Mkulima mmoja anaeleza hivi: “Mbuzi huzoeana na watu wanaowatunza, na hivyo wanakuwa wanyama-vipenzi. Kwa hiyo ni vigumu kumchinja hata mbuzi mmoja.” Wafugaji wa mbuzi hawataki kutenganishwa na wanyama wao wapendwa! Huenda hiyo ikawa sababu nyingine inayowafanya mbuzi wastahimili hali ngumu!
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Wareno wa kwanza kufika katika eneo hilo waliliita desertão, au jangwa kubwa, kwa sababu liliwakumbusha kuhusu majangwa na maeneo ya savana ya Afrika Kaskazini.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]
Ukweli Kuhusu Maziwa ya Mbuzi
Watu wengi husema kwamba ni vigumu kumeng’enya maziwa ya mbuzi, na wengine husema kwamba yananuka vibaya. Lakini usiamini maoni hayo yasiyo ya kweli kuhusu maziwa ya mbuzi. Ikiwa wewe hupata matatizo ya kumeng’enya maziwa ya ng’ombe, huenda daktari au mtaalamu wa lishe akapendekeza utumie vyakula vilivyotengenezwa kwa maziwa ya mbuzi. Ingawa maziwa ya mbuzi yana mafuta na protini nyingi, vidonge vyake vya mafuta ni vidogo na rahisi zaidi kumeng’enya. Vipi harufu yake?
Maziwa ya mbuzi hayana harufu. Ukihisi maziwa ya mbuzi yana harufu mbaya huenda ikawa kwamba mbuzi huyo alikamwa mahali pachafu au alikuwa karibu na mbuzi-dume. Tezi za harufu zilizo nyuma ya pembe za mbuzi-dume hutokeza homoni ambayo huvutia mbuzi-jike. Homoni hiyo huchafua kitu chochote ambacho huguswa na mbuzi-dume.
[Hisani]
CNPC–Centro Nacional de Pesquisa de Caprinos (Sobral, CE, Brasil)
[Ramani katika ukurasa wa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
“Sertão”
[Picha katika ukurasa wa 26]
Mbuzi hutumia kinywa chake kilichobuniwa kwa njia ya pekee kuchagua sehemu bora za mmea
[Hisani]
Dr. João Ambrósio–EMBRAPA (CNPC)
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Map: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.; goats: CNPC–Centro Nacional de Pesquisa de Caprinos (Sobral, CE, Brasil)