Ubaguzi
Ubaguzi
“Hata jitihada za aina gani zikifanywa ili kumaliza ubaguzi, bado utarudi.”—Frederick Mkuu, Mfalme wa Prussia.
RAJESH huishi katika kijiji cha Paliyad huko India. Sawa na watu wengine wanaobaguliwa na kuonwa kuwa wachafu, yeye hutembea dakika 15 ili kuteka maji kwa ajili ya familia yake. Anasema hivi: “Katika kijiji chetu, haturuhusiwi kuteka maji katika mifereji inayotumiwa na watu wa matabaka ya juu.” Alipokuwa shuleni, Rajesh na rafiki zake hata hawakuruhusiwa kuugusa mpira ambao watoto wengine waliuchezea. Anasema: “Badala yake, tulichezea mawe.”
“Mimi huona kwamba watu wananichukia, lakini sijui sababu,” asema Christina, kijana kutoka Asia anayeishi Ulaya. Anaongeza hivi: “Inafadhaisha sana. Kwa kawaida, mimi hujitenga na wengine, lakini hilo pia halisaidii.”
“Nilianza kuona ubaguzi nikiwa na umri wa miaka 16,” asema Stanley, wa Afrika Magharibi. “Watu nisiowajua hata kidogo waliniambia niondoke mjini. Nyumba za watu fulani wa kabila letu ziliteketezwa. Akaunti ya benki ya baba yangu ilifungwa. Hivyo, nilianza kulichukia kabila lililotubagua.”
Rajesh, Christina, na Stanley ni baadhi tu ya watu waliobaguliwa. “Mamia ya mamilioni ya watu wanaendelea kuumia kutokana na ubaguzi wa rangi, upendeleo, chuki dhidi ya wageni, na kutengwa na jamii,” asema Koichiro Matsuura, mkurugenzi-mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO). “Matendo hayo ya kinyama yanayochochewa na ujinga na maoni ya chuki, yamesababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi nyingi na mateso mengi kwa wanadamu.”
Ikiwa hujawahi kubaguliwa, huenda ikawa vigumu kwako kuelewa jinsi hali hiyo inavyofadhaisha sana. Kitabu Face to Face Against Prejudice kinasema kwamba “watu fulani huvumilia ubaguzi bila kulalamika. Wengine hulipiza kisasi wanapobaguliwa.” Ubaguzi huathirije maisha ya watu?
Ikiwa wewe ni mtu wa jamii ndogo, huenda watu wakakuepuka, wakakutazama vibaya, au wakasema kwa madharau kuhusu utamaduni wenu. Usipokubali kazi za hali ya chini zinazoepukwa na wengi, huenda isiwe rahisi kupata kazi nyingine. Huenda ikawa vigumu kupata makao mazuri. Watoto wako wanaweza kutengwa na kukataliwa na wanafunzi wenzao shuleni.
Isitoshe, ubaguzi unaweza kuwachochea watu kuwa wajeuri au hata kuua. Kwa kweli, historia ina mifano mingi yenye kuogopesha kuhusu jeuri ambayo imesababishwa na ubaguzi, kama vile mauaji ya kinyama ya watu wengi na mauaji ya jamii nzima-nzima.
Ubaguzi Umekuwapo kwa Karne Nyingi
Wakati mmoja, Wakristo hasa ndio waliobaguliwa. Kwa mfano, muda mfupi baada ya kifo cha Yesu, Wakristo walinyanyaswa kwa ukatili sana. (Matendo 8:3; 9:1, 2; 26:10, 11) Karne mbili baadaye, watu waliodai kuwa Wakristo walidhulumiwa kwa ukatili mara nyingi. Tertullian, mwandishi wa karne ya tatu, aliandika hivi: “Janga linapotokea, mara moja watu hupiga kelele hivi, ‘Wapelekeni Wakristo Wakaliwe na Simba.’”
Hata hivyo, kuanzia karne ya 11, wakati wa vile Vita Vitakatifu, jamii ndogo ya Wayahudi ilianza kuchukiwa sana huko Ulaya. Tauni ya majipu ilipokumba Bara hilo na kusababisha vifo vya karibu robo ya watu katika muda wa miaka michache tu, ilikuwa rahisi kuwalaumu Wayahudi kwani tayari walichukiwa na wengi. Katika kitabu chake Invisible Enemies, Jeanette Farrell anaandika hivi: ‘Chuki hiyo iliwafanya watu ambao waliogopa tauni hiyo kudai kwamba ilisababishwa na Wayahudi.’
Hatimaye, Myahudi mmoja kusini mwa Ufaransa alipokuwa akiteswa sana, “aliungama” kwamba Wayahudi ndio waliosababisha tauni hiyo kwa kutia sumu ndani ya visima. Bila shaka, alisema uwongo, lakini habari hizo zilienezwa kuwa habari za kweli. Muda si muda, jumuiya nzima-nzima za Wayahudi zilichinjwa huko Hispania, Ufaransa, na Ujerumani. Ni kana kwamba hakuna mtu awaye yote aliyezingatia kisababishi kikuu cha tauni hiyo, yaani, panya. Na ni watu wachache tu waliotambua kwamba Wayahudi pia walikufa kutokana na tauni hiyo!
Ubaguzi ukiisha kuanza, unaweza kuendelea kichinichini kwa karne nyingi. Katikati ya karne ya 20, Adolf Hitler alichochea chuki dhidi ya Wayahudi kwa kuwalaumu kwamba walifanya
Ujerumani ishindwe katika Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. Mwishoni mwa Vita vya Pili vya Ulimwengu, Rudolf Hoess, kamanda wa Nazi katika kambi ya mateso ya Auschwitz, alikubali hivi: “Mafunzo ya kijeshi na dhana zetu zilitufanya tuamini kwamba tulihitaji kuilinda Ujerumani dhidi ya Wayahudi.” Ili “kuilinda Ujerumani,” Hoess alisimamia mauaji ya watu 2,000,000 hivi, wengi wao wakiwa Wayahudi.Ijapokuwa miaka mingi imepita tangu wakati huo, inasikitisha kwamba ukatili haujakwisha. Kwa mfano, katika mwaka wa 1994, chuki ya kikabila ilizuka katika Afrika Mashariki kati ya Watutsi na Wahutu, na kusababisha vifo vya watu wapatao nusu milioni. “Hakukuwa na sehemu za kukimbilia,” laripoti gazeti Time. “Watu wengi waliuawa ndani ya makanisa ambamo walijificha. . . . Vita hivyo vilipiganwa ana kwa ana, vilichochewa na sababu za kibinafsi, na viliogopesha sana, kwani watu walikuwa na hamu kubwa ya kumwaga damu hivi kwamba wale waliofaulu kutoroka walichanganyikiwa kihisia na kushindwa kuongea kwa sababu ya woga.” Hata watoto hawakuepuka jeuri hiyo yenye kutisha. “Rwanda ni nchi ndogo,” alieleza raia mmoja. “Lakini sisi ndio wenye chuki zaidi ulimwenguni.”
Mapigano yaliyotokana na kuvunjika kwa Yugoslavia, yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 200,000. Majirani waliokuwa wameishi kwa amani kwa miaka mingi waliuana. Maelfu ya wanawake walinajisiwa, na mamilioni ya watu wakafukuzwa makwao kwa sababu ya mauaji ya kikatili ya jamii nzima-nzima.
Ijapokuwa mara nyingi ubaguzi hausababishi mauaji, kwa kawaida unawagawanya watu na kuchochea chuki. Licha ya kuongezeka kwa ushirikiano kati ya mataifa, inaonekana ubaguzi wa rangi na wa kijamii “unazidi katika sehemu nyingi ulimwenguni,” yasema ripoti moja ya karibuni ya shirika la UNESCO.
Je, inawezekana kukomesha ubaguzi? Ili kujibu swali hilo, tunapaswa kufahamu jinsi ubaguzi unavyoingizwa katika akili na mioyo ya watu.
[Sanduku katika ukurasa wa 5]
Jinsi Ubaguzi Unavyoonyeshwa
Katika kitabu chake The Nature of Prejudice, Gordon W. Allport anataja mambo matano yanayosababishwa na ubaguzi. Kwa kawaida, mtu mwenye ubaguzi hufanya jambo moja au zaidi kati ya haya.
1. Kusema mambo yasiyofaa. Mtu huongea kwa madharau kuhusu jamii anayochukia.
2. Kuwaepuka wengine. Yeye humwepuka mtu yeyote wa jamii anayochukia.
3. Kuwa mwenye upendeleo. Yeye huwatenga watu wa jamii hiyo inayobaguliwa kwa kuwazuia wasipate kazi za aina fulani, wasiishi katika maeneo fulani, au wasipate huduma fulani za jamii.
4. Kuwashambulia wengine. Yeye hushiriki katika matendo ya jeuri ili kuwatisha watu anaochukia.
5. Kuua. Yeye hujihusisha katika visa vya mauaji na uchinjaji wa jamii nzima-nzima.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Kambi ya wakimbizi ya Benaco, huko Tanzania, mnamo Mei 11, 1994
Mwanamke anapumzika kando ya vyombo vya kevya kutekea maji. Zaidi ya wakimbizi 300,000, hasa Wahutu kutoka Rwanda waliingia Tanzania
[Hisani]
Photo by Paula Bronstein/Liaison