Tumaini Je, Linaweza Kutusaidia?
Tumaini Je, Linaweza Kutusaidia?
DANIEL alikuwa ameugua kansa kwa mwaka mmoja alipokuwa na umri wa miaka kumi tu. Madaktari na rafiki zake wa karibu walikuwa wamekata tamaa. Hata hivyo, Daniel aliendelea kuwa na tumaini. Aliamini kwamba siku moja angekuwa mkubwa na kuwa mtafiti ambaye angesaidia kupata tiba ya kansa. Alitarajia sana kuja kwa daktari ambaye ni mtaalamu wa kutibu aina ya kansa aliyokuwa nayo. Hata hivyo, siku hiyo ilipofika, daktari huyo alilazimika kuvunja safari yake kwa sababu ya hali mbaya ya hewa. Daniel akakata tamaa. Kwa mara ya kwanza, akafadhaika. Akafa siku chache baadaye.
Kisa cha Daniel kilisimuliwa na mfanyakazi wa afya ambaye alichunguza jinsi kuwa na tumaini au kupoteza tumaini kunavyoathiri afya. Huenda umesikia visa kama hivyo. Kwa mfano, fikiria mzee anayekaribia kufa ambaye anatarajia kwa hamu tukio fulani muhimu ambalo amengojea kwa muda mrefu, labda kutembelewa na mpendwa au sherehe fulani. Tukio hilo linapofika na kupita, mzee huyo hufa baada ya muda mfupi. Ni nini husababisha jambo hilo? Je, ni kukosa tumaini kama wengine wanavyoamini?
Watafiti wengi wa kitiba husema kwamba matazamio mema, tumaini, na maoni mazuri huboresha maisha na afya ya mtu. Lakini si wote wenye maoni hayo. Watafiti fulani hupinga jambo hilo wakisema kwamba halipatani na sayansi. Wao husema kwamba magonjwa hayawezi kusababishwa na hisia.
Bila shaka, maoni hayo yanayopinga umuhimu wa tumaini si mapya. Maelfu ya miaka iliyopita, mwanafalsafa Mgiriki Aristotle alipoulizwa maana ya tumaini, alijibu: “Ni ndoto ya mchana.” Na muda mrefu baadaye, mwanasiasa wa Marekani, Benjamin Franklin, alisema hivi waziwazi: “Anayeishi kwa tumaini atakufa njaa.”
Basi, tumaini ni nini? Je, wakati wote tumaini ni njia ya kujifariji kwa kuota ndoto zisizoweza kutimia? Au, je, tumaini linahusisha mengi zaidi ya ndoto—kitu ambacho sote tunahitaji ili tuwe na afya na furaha, kitu ambacho kina msingi thabiti na manufaa?