Kiwanda cha Kutengeneza Divai cha Moldova
Kiwanda cha Kutengeneza Divai cha Moldova
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MOLDOVA
KATIKA kitongoji cha Cricova, nje ya Chişinău, jiji kuu la Moldova, kuna vijia mbalimbali meta 80 hivi chini ya ardhi, vyote pamoja vikiwa na urefu wa kilometa 120. Zamani chokaa ilichimbwa kwenye mapango hayo yenye giza.
Hata hivyo, kwa miaka 50 iliyopita, mapango hayo baridi yametumiwa kuhifadhi divai bora ya Ulaya. Mapipa na chupa zimepangwa kwenye sehemu yenye urefu wa zaidi ya kilometa 60 katika mapango hayo. Mapango hayo yanaweza kuhifadhi lita milioni 350 za divai, na inasemekana ndiyo hifadhi kubwa zaidi ya divai kusini-mashariki mwa Ulaya.
Kuendeleza Utamaduni wa Kale
Moldova ni nchi inayofaa zao la zabibu. Iko kwenye mstari uleule wa latitudo na mkoa wa Burgundy wa Ufaransa ambao ni maarufu kwa utengenezaji wa divai na ina hali ya hewa ya wastani na udongo wenye rutuba. Utengenezaji wa divai ulianza huko Moldova katika mwaka wa 300 K.W.K., wakati wafanyabiashara Wagiriki walipoleta mizabibu kwa mara ya kwanza katika eneo hilo. Karne zilizofuata, utengenezaji wa divai uliendelea hata ingawa nchi hiyo ilitekwa na Wagothi, Wahuni, na watawala mbalimbali.
Miliki ya Ottoman ilimiliki eneo hilo kati ya karne ya 16 na 18 na kupiga marufuku utengenezaji wa divai kwa sababu za kidini. Hata hivyo, katika karne ya 19, watawala Warusi waliimiliki nchi hiyo na kuwahimiza watu wafanye biashara ya divai. Walileta mizabibu mbalimbali kutoka Ufaransa na ilisitawi. Baada ya Vita vya Pili vya Ulimwengu, serikali ya Muungano wa Sovieti, iliyotawala Moldova, ilitumia mbinu za kisasa kutengeneza divai. Hata ilifanya Moldova kuwa eneo kuu linalotokeza divai katika Muungano wote wa Sovieti. Wasovieti ndio waliogundua kwamba mapango hayo ni hifadhi nzuri ya divai. Andamana nasi tunapotembelea hifadhi hiyo ili ujifunze mambo fulani kuihusu.
Kusafiri Katika Mji Ulio Chini ya Ardhi
Tunapoingia ndani ya kiwanda hicho cha divai kwa gari, tunaona mnara langoni ambao ni sehemu ya jengo lililochongwa kwenye jiwe la chokaa. Jengo hilo linafanana na vibanda vya eneo la mashambani la Ufaransa. Hata hivyo, huwezi kuwazia kwamba kuna majengo makubwa chini yake. Mwendo mfupi kutoka langoni, tunaona njia ya kuingia pangoni na tunastaajabishwa na ukubwa wake. Hata malori mawili yanaweza kupitana bila wasiwasi.
Tunaingia kwa gari katika pango hilo, na baada ya dakika chache tunajiunga na yule anayetutembeza. Kuna njia nyingi zinazopindapinda hivi kwamba tungepotea kama hatungekuwa na mtu wa kutuelekeza.
Mmoja wetu anauliza, “Mawe ya chokaa yaliyokuwa yakichimbwa hapa yalienda wapi?”
Anayetutembeza anajibu hivi: “Yalitumiwa kujenga huko Chişinău. Chokaa ni nzuri kwa ujenzi kwa kuwa inaweza kuzuia umeme na sauti zisipenye.”
Tunapoteremka meta 70 hivi chini ya ardhi giza linaongezeka na kutuogopesha. Tunasimama katika makutano ya barabara nyingi zilizo na mapipa makubwa ya divai pande zote. Tunaona kwamba barabara zimeitwa majina ya aina tofauti za divai. Baadhi ya majina ambayo yanatufurahisha ni kama vile Pinot, Feteasca, na Cabernet.
Yule anayetutembeza anatueleza kwamba mapipa ya mialoni hutumiwa hasa kutengeneza divai ambayo haitoi povu hali mapipa madogo ya chuma hutumiwa kutengeneza divai yenye povu. Tunawaona wafanyakazi wachache sana na tunauliza ni watu wangapi wanaofanya kazi huku. Anajibu hivi: “Kuna wafanyakazi 300 hivi. Wote huvalia nguo nzito mwaka mzima kwa sababu ya baridi. Wanaamini kwamba hali hiyo ya hewa ni nzuri kwa divai na inawafanya watu waendelee kuwa vijana, kwa hiyo hawajali baridi.”
Baadaye tunatembelea kiwanda cha kutengeneza divai yenye povu. Tunaona mamia ya chupa zikiwa zimeinamishwa juu-chini kwa digrii 30. Tunaambiwa hivi: “Chupa zinapoinamishwa hivyo, machicha hukusanyika kwenye kifuniko. Baadaye kifuniko hugandishwa. Sasa kinaweza kutolewa kwa urahisi pamoja na machicha, halafu chupa hufunikwa tena.”
Muda si muda tunafika kwenye hifadhi ya divai ya msimu. Yule anayetutembeza anasema hivi: “Zaidi ya chupa milioni moja za divai ya msimu huhifadhiwa humu. Karibu nchi zote za Ulaya huhifadhi divai nzuri katika mapango yetu. Divai ya kale zaidi ni ya mwaka wa 1902 na ilitengenezwa kwa ajili ya Pasaka ya Wayahudi huko Yerusalemu. Miaka kadhaa iliyopita, mtu mmoja alitaka kununua divai hiyo kwa dola 100,000 lakini hakuruhusiwa. Chupa hiyo ilionwa kuwa yenye thamani sana.”
Pia tunaambiwa kwamba hifadhi hiyo ya divai huwa na giza zito wakati wote ila tu kwa dakika chache ambapo watalii wanatembezwa. Tunapochunguza vibandiko vya chupa hizo zenye vumbi, tunagundua kwamba divai nyingi ni nzee kuliko sisi!
Matembezi yetu yanaishia kwenye chumba cha kuonjea divai. Chumba kikubwa zaidi kinaitwa Chumba cha Karamu cha Rais. Kina meza ndefu ya mwaloni na viti vinavyofanana nayo, vinavyoweza kukaliwa na watu 65. Chumba hicho kilitumiwa kwa ajili ya karamu za serikali wakati wa Muungano wa Sovieti. Leo chumba hicho maridadi chenye mwangaza wa kutosha bado kinatumiwa kwa ajili ya shughuli za serikali.
Chumba cha Sala Casa Mare (Chumba cha Wageni) huketi watu 15 na kina fanicha za kitamaduni za Moldova, na watu 10 wanaweza kufurahia mlo kwenye meza ya duara katika Sehemu ya Chini ya Chumba cha Karamu cha Sarmatic. Jambo la kupendeza zaidi kwenye chumba hicho ni dari lake. Mwanzoni chumba hicho kilikuwa pango la chini ya maji, na kuna mabaki ya samaki-gamba na ya wanyama wa majini. Tunakumbushwa na yule anayetutembeza kwamba wakati mmoja jiji la Moldova lilikuwa “chini ya Bahari ya Sarmatic.”
Mialoni ya hapa hutumiwa kutengeneza fanicha zilizo katika vyumba hivyo, kutia ndani zile zilizo katika Chumba cha Karamu cha Yury Gagarin. Mtalaamu huyo wa angani anayejulikana, alitembelea Cricova mnamo Oktoba 8-9, 1966. Aliandika barua ya shukrani na kusema kwamba ‘hata mtaalamu stadi wa kuonja atapata divai anayopenda hapa.’
Yule anayetutembeza anatuambia hivi: “Tangu hifadhi hii ijengwe miaka 50 iliyopita, tumetembelewa na watu kutoka zaidi ya nchi mia moja. Wakati wa Muungano wa Sovieti, divai yetu yenye povu iliitwa shampeni ya Sovieti. Ni wachache sana waliojua kwamba ilitoka Moldova. Leo tunauza divai yenye povu inayoitwa Cricova, na tuna divai nyekundu na nyeupe.” Tunathamini mambo yote ambayo yule anayetutembeza ametueleza na tunamshukuru kwa kututembeza.
Tunapotoka mapangoni, tunahisi kana kwamba tumetoka ulimwengu mwingine. Nje kuna jua na joto kali. Hakuna mawingu hata kidogo. Tunaporudi Chişinău, tunaona bustani nzuri kubwa zilizotunzwa vizuri zenye mizabibu ambayo inakaribia kuvunwa.
[Ramani katika ukurasa wa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
UKRAINIA
MOLDOVA
RUMANIA
Chişinău
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kiwanda cha kutengeneza divai cha Cricova na mnara wake langoni
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mojawapo ya majina ya barabara za chini ya ardhi zenye urefu wa kilometa 120
[Picha katika ukurasa wa 24]
Njia ya gari ya kuingia kwenye hifadhi ya divai
[Picha katika ukurasa wa 24]
Zaidi ya chupa milioni moja za divai huhifadhiwa hapa