Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Hisi Zenye Kustaajabisha Nina umri wa miaka 15 na nimesoma magazeti yenu tangu nilipojua kusoma. Asanteni kwa mfululizo wenye kichwa “Hisi Zenye Kustaajabisha—Je, Unazithamini?” (Machi 8, 2003) Makala hizo zilipendeza. Asanteni kwa kazi yenu ngumu na utafiti mnaofanya mnapoandika Amkeni! Nina hamu kubwa ya kusoma gazeti linalofuata!
H. S., Marekani
Mfululizo huo ulinisaidia kuelewa kwamba sisi ni viumbe tata. Nilistaajabu kufahamu kwamba kidole cha mwanadamu kinaweza kutambua alama ndogo sana ya kituo yenye ukubwa wa mikroni tatu! Ama kweli, Yehova anawajali viumbe wake hata katika mambo madogo hivyo.
E. R., Australia
Mhispania Aliyefia Imani Nawashukuru kwa dhati kwa ajili ya makala “Mwanamume Aliyeamua Kumtii Mungu.” (Machi 8, 2003) Niliguswa moyo niliposoma jinsi Antonio Gargallo alivyodumisha uaminifu wake alipokabili uamuzi mzito kwa ghafula hata ingawa alikuwa na umri wa miaka 19 tu na alikuwa amebatizwa karibuni. Makala hiyo ilinionyesha jinsi Yehova anavyotuimarisha na kutupa amani ya moyoni tukiazimia kufanya mapenzi yake.
M. T., Italia
Asanteni sana kwa simulizi hilo fupi lenye kuchochea. Machozi yalinidondoka nilipolisoma. Niliguswa moyo hasa na barua ambayo Antonio Gargallo alimwandikia mama yake na dada yake kabla ya kuuawa. Tafadhali endeleeni kuandika kuhusu Wakristo ambao wamebaki waaminifu kwa Yehova licha ya kukabili kifo ili imani yetu iimarishwe.
R. O., Nigeria
Viatu Asanteni kwa makala “Je, Viatu Vyako Vinakutoshea Vizuri?” (Machi 8, 2003) Nimekuwa na matatizo ya miguu kwa miaka mingi na hata nimefanyiwa upasuaji mdogo mara kadhaa. Hatimaye niligundua kwamba mguu mmoja ni mkubwa kuliko mwingine. Sasa inanibidi nivae viatu maalumu vya watu wenye matatizo ya mifupa kwa kuwa nilivaa viatu visivyonitoshea kwa miaka mingi.
R. G., Marekani
Ilikuwa makala nzuri sana. Hata hivyo, hamkutaja kwamba ni vizuri zaidi kununua viatu jioni wakati ambapo kwa kawaida miguu huwa imefura.
A. W., Kanada
“Amkeni!” linajibu: Asante kwa maoni yako. Tafadhali soma sehemu yenye kichwa “Matatizo ya Kiafya Yahusishwa na Viatu” katika makala ya “Kuutazama Ulimwengu” katika toleo la Agosti 8, 1999.
Kuiba Mtihani Ninashukuru kwa makala “Vijana Huuliza . . . Kuna Ubaya Gani Kuiba Mtihani?” (Januari 22, 2003) Mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu na nimekuwa na tabia ya kuiba mtihani tangu nilipokuwa katika darasa la tano. Sikuzote nilijiuliza kama kuiba mtihani ni sawa, lakini sikupata jibu. Kwa hiyo, makala hiyo ilinisaidia sana. Nimeamua kubadili tabia yangu kuanzia mtihani unaokuja ambao ninasomea hivi sasa.
S. Y., Ukrainia
Ukahaba wa Watoto Asanteni kwa mfululizo “Ukahaba wa Watoto—Ni Hali Inayosikitisha.” (Februari 8, 2003) Ingawa tatizo hilo linasikitisha sana, nilichochewa hasa na jinsi ambavyo wahasiriwa walifarijiwa. Mifano mliyotoa inafanana na hali iliyonipata. Ilionyesha kwamba hata katika mfumo huu mbovu, athari za tukio lenye kuhuzunisha zinaweza kukomeshwa kwa kiasi kikubwa—kwa msaada wa Yehova.
P. R., Ujerumani