Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Hasara za Kufanya Kazi Baada ya Shule
Idadi kubwa ya vijana Wajerumani hufanya kazi wakati wa likizo na pia baada ya shule. Gazeti la Der Spiegel laripoti kwamba “angalau thuluthi moja ya watoto wenye umri wa kuanzia miaka 13 na zaidi kote nchini, hufanya kazi kwa wastani wa saa tatu kila juma.” Katika jimbo la Hesse nchini Ujerumani, kati ya asilimia 50 na 80 ya wanafunzi wa madarasa ya juu katika shule za upili hufanya kazi za pembeni. Mara nyingi vijana hao hawahitaji kusaidia familia zao kupata mahitaji ya lazima. Badala yake, wanataka vitu vya kisasa kama vile simu za mkononi, mavazi ya kimtindo, na magari ya kisasa, na hata kujitegemea. Lakini kuna hasara. Mwalimu Thomas Müller asema kwamba “si ajabu kumwona mwanafunzi akilala darasani kwa sababu alifanya kazi kwa muda mrefu siku iliyotangulia au hata mapema asubuhi. Wanataka raha sasa badala ya elimu itakayowasaidia wakati ujao.” Mwalimu mwenzake Knud Dittman aongezea: “Mara tu watoto wanapokuwa na tabia ya kununua-nunua vitu, hawajali hata kutofanya vizuri shuleni au hata kurudia mwaka mmoja.”
Sokwe Wamo Hatarini
“Misitu ambamo sokwe huishi itatoweka baada ya miaka 30 ikiwa wanadamu hawatachukua hatua madhubuti,” laripoti shirika la habari la Reuters. Maafisa wa Umoja wa Mataifa walisema hivi kwenye Mkutano Kuhusu Mazingira ya Dunia uliofanywa karibuni huko Johannesburg, Afrika Kusini: “Ni asilimia isiyozidi 10 ya makao ya sokwe wa Afrika yatakayobaki kufikia mwaka wa 2030 ikiwa ujenzi wa barabara, uchimbaji wa migodi na miradi mingine itaendelea.” Tayari idadi ya sokwe imepungua sana kwa sababu ya kupungua kwa misitu wanamoishi. Idadi ya sokwe waliopo sasa inakadiriwa kuwa 200,000 ikilinganishwa na 2,000,000 karne iliyopita, na sokwe wanaoishi kwenye nyanda za chini wamebaki elfu kadhaa tu hali sokwe wa milimani wamebaki mamia kadhaa tu. Shirika la Reuters linasema kwamba “shirika la U.M. linashirikiana na watafiti, wahifadhi wa mazingira, serikali na wenyeji kupanga mikakati ya kuwaokoa sokwe katika nchi 24 hivi zenye sokwe wengi.”
Televisheni Huathiri Maoni ya Watu Kuhusu Historia
Gazeti The Times la London linaripoti kwamba “Waingereza wanaona kifo cha Malkia Diana wa Wales kuwa tukio kuu zaidi katika historia ya nchi hiyo katika muda wa miaka 100 iliyopita. Ni tukio kuu kuliko kuzuka kwa Vita vya Pili vya Ulimwengu au haki ya wanawake ya kupiga kura.” Katika uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Vipindi vya Historia, zaidi ya watu 1,000 waliombwa wachague matukio 10 ambayo waliona kuwa makuu katika historia ya Uingereza katika muda wa miaka 100 iliyopita. Asilimia 22 walichagua kifo cha malkia huyo kuwa tukio kuu zaidi, asilimia 21 walichagua kuzuka kwa vita vya pili vya ulimwengu, na asilimia 15 walichagua haki ya wanawake ya kupiga kura. Walipoulizwa kuhusu matukio ya ulimwengu, asilimia 41 walichagua mashambulizi ya Septemba 11, asilimia 19 walichagua kutupwa kwa bomu la atomiki huko Hiroshima, na asilimia 11 walichagua kubomolewa kwa Ukuta wa Berlin. Gazeti The Times linasema kwamba watu wengi “wanafikiri mambo ya kihistoria ni yale waliyoona karibuni zaidi katika televisheni.”
Je, Talaka Huathiri Masomo Shuleni?
Utafiti uliofanywa karibuni na Taasisi ya Kuchunguza Idadi ya Watu ya Ufaransa unaonyesha kwamba watoto wa wazazi waliotalikiana hawafanyi vyema shuleni kama watoto wa wazazi wanaoishi pamoja, laripoti gazeti Le Monde la Ufaransa. Wazazi wanapotengana watoto wakiwa wadogo, wao huacha shule miezi 6 au mwaka mmoja mapema ikilinganishwa na wale ambao wazazi hawatengani, na wala haitegemei jamii na utamaduni. Watoto wengi kutoka familia tajiri hupita mitihani yao ya mwisho, lakini kuna uwezekano mkubwa kwa wale wanaotoka kwenye familia zilizovunjika kutofanya vizuri shuleni. Asilimia 40 ya ndoa nchini Ufaransa huishia kwenye talaka.
Madhara Mengine ya Dawa za Kulevya
Gazeti la El Comercio la Lima linaripoti kwamba katika miezi ya karibuni, watu watano wamekufa huko Peru baada ya kunywa maji yanayotoka msituni ambayo yalichafuliwa na ukuzaji wa koka na utengenezaji wa kokeini. Mafuta ya taa, asidi ya salfuriki, amonia na kemikali nyingine zenye sumu hutumiwa kutengeneza kokeini. “Watu hao walikufa baada ya kunywa maji kutoka chemchemi au vijito ambamo walanguzi wa dawa za kulevya hutupa takataka zenye kemikali yenye sumu kali,” yasema ripoti hiyo. Hata polisi wanaopambana na ulanguzi wa dawa za kulevya ambao hugundua na kuharibu viwanda vilivyofichwa vya kutengeneza dawa hizo wameathiriwa sana na takataka hizo zenye sumu. Watu wengine wengi wanaoishi kwenye misitu hiyo wamepata pia “madhara yasiyotibika ya viungo vya mwili” kwa sababu ya kunywa maji yenye sumu. Jonathan Jacobson wa Ofisi ya Kupambana na Ulanguzi wa Dawa za Kulevya iliyo katika Ubalozi wa Marekani huko Lima anasema “inahuzunisha kwamba idadi kubwa ya watu hao hata hawajui hatari inayowakabili. Bila shaka watu hao hawakuzi koka wala kutengeneza kokeini.”
Wamexico Hunywa Soda Sana
Nchi ya Mexico ndiyo ya pili katika unywaji wa soda ulimwenguni baada ya Marekani, na soda ni miongoni mwa vitu kumi vinavyopendwa sana nchini Mexico. Asilimia 60 ya familia hunywa soda, laripoti gazeti la Reforma. Hilo linawahangaisha wataalamu wa afya kwa sababu badala ya kununua maziwa, matunda, mboga, na vyakula vingine vilivyo muhimu kwa ukuzi wa watoto, familia hutumia pesa nyingi kununua bidhaa ambazo “hazijengi mwili lakini zina kiwango kikubwa cha wanga ambacho mwishowe kinawafanya wanenepe kupita kiasi,” laripoti gazeti la Reforma. Madhara mengine ya kunywa soda sana hasa soda za cola, ni meno kuoza na kudhoofika kwa mifupa, yasema ripoti hiyo.
Vidonge Vyaweza Kuzidisha Maumivu ya Kichwa
“Daktari wa neva Michael Anthony anakadiria kwamba asilimia 10 ya watu wenye kuumwa na kichwa ‘hutumia isivyofaa dawa za kutuliza maumivu,’ lasema gazeti The Daily Telegraph la Sydney, Australia. “Mtu anaweza kuumwa na kichwa kila siku badala ya mara moja kwa juma kwa sababu ya kutegemea sana dawa zinazonunuliwa dukani.” Profesa Anthony wa Chuo Kikuu cha New South Wales, aligundua kwamba “wagonjwa wanaotumia isivyofaa vidonge vya kutuliza maumivu ya kichwa wana upungufu wa serotonin,” homoni inayozuia mishipa ya damu kupanuka. Anasema, “kiasi kidogo cha serotonin hufanya mishipa ipanuke, na hilo husababisha maumivu ya kichwa.” Anthony anapendekeza watu wanaosumbuliwa na kipandauso watumie dawa wanazopewa na daktari badala ya kununua vidonge dukani, kisha aongezea: “Ikiwa [wagonjwa] watameza vidonge [vya kutuliza maumivu] zaidi ya mara tatu kwa juma au hata dozi moja mara tatu kwa juma, basi maumivu yao ya kichwa yatazidi baada ya miezi michache.”
Kupunguza Kichefuchefu cha Wajawazito
“Inakadiriwa kwamba kati ya asilimia 70 na 80 ya wajawazito hushikwa na kichefuchefu wakati wa asubuhi,” lasema gazeti la Sun-Herald la Australia. Wanawake hao wenye mimba changa hushikwa na kichefuchefu na mara nyingi hutapika wanapoamka asubuhi. Miongoni mwa mambo yanayokisiwa yanasababisha tatizo hilo ni kuongezeka kwa homoni ya projesteroni wakati wa ujauzito, ambayo inaweza kuzidisha asidi za tumboni. Zaidi ya hilo, “uwezo bora wa kunusa unaweza kuwafanya wajawazito wahisi kichefuchefu.” Ijapokuwa hakuna dawa ya kutibu kichefuchefu, gazeti hilo linapendekeza wajawazito waepuke sehemu zenye joto, kwa kuwa joto linasababisha kichefuchefu, walale kidogo mchana na wapate usingizi wa kutosha, na wanuse ndimu iliyokatwa. “Jaribu kula biskuti kavu au nafaka kavu kabla ya kutoka kitandani. Kila siku toka kitandani polepole,” laongezea gazeti hilo. “Mara kwa mara kula vyakula vyepesi vyenye protini.” Gazeti hilo lasema kwamba “kichefuchefu cha wajawazito kina faida pia. Uchunguzi wa karibuni unaonyesha kwamba yaelekea mara nyingi mimba za wajawazito wanaoshikwa na kichefuchefu haziharibiki.”