Je, Ni Mnyama-Kipenzi au Ni Muuaji Hatari?
Je, Ni Mnyama-Kipenzi au Ni Muuaji Hatari?
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI POLAND
MTU mmoja anayefanya mazoezi ya kukimbia avuja damu na kufa baada ya kushambuliwa na mbwa mkali sana. Msichana mmoja auawa na mbwa wake aina ya Rottweiler. Mbwa mzururaji aina ya German shepherd amshambulia mvulana mwenye umri wa miaka tisa na kumuua mbele ya wazazi wake. Hiyo ni baadhi tu ya misiba ambayo imesababishwa na mbwa wanaozaliwa na jamii moja ya mbwa nchini Poland.
Ili kuepuka misiba kama hiyo, serikali fulani huwaruhusu watu wafuge mbwa fulani baada tu ya kupata cheti. Barbara Zaleska, mwanachama wa Chama cha Wamiliki wa Mbwa Nchini Poland, asema kwamba wamiliki wa mbwa ndio wanaopaswa kupewa cheti wala si mbwa “kwa sababu ni mmiliki atakayeamua ikiwa mbwa wake aina ya mastiff, Rottweiler, na bullterrier watakuwa hatari sana kwa wanadamu au watakuwa rafiki zao.”
Nyakati nyingine, mbwa huzoezwa kimakusudi kuwa wauaji. Inadaiwa kwamba walimu wa mbwa huwapiga, huwanyima chakula, na hata hutumia “mazoezi ya kuua,” ambayo yanatia ndani kumzoeza mbwa kushambulia na kurarua-rarua wanasesere. Kisha, mbwa huzoezwa kuwashambulia mbwa wengine wanyonge na kuwaua. Baada ya kuzoezwa kikamili, mbwa huwa tayari kushiriki mapigano ya mbwa ambayo yanapendwa sana na wachezaji wa kamari na mashabiki wanaopenda kuona mbwa wakiangamizana.
Biblia inaeleza waziwazi maoni ya Mungu kuhusu kuwatendea wanyama kwa ukatili. Inasema hivi: “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake; bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.” (Mithali 12:10) Watu wanaotaka kumpendeza Mungu hawawatendei wanyama kwa ukatili. Tunafurahi kujua kwamba katika ulimwengu mpya wa Mungu, tabia ya kuwazoeza wanyama ili wawe wauaji—iwe ni katika michezo ama kwa sababu nyingine yoyote—itakoma.—Zaburi 37:9-11.