Kuvuka Mstari
Kuvuka Mstari
KWA MUDA MREFU MWANADAMU AMETAMANI kurudisha wakati nyuma au kuusogeza mbele ili ajikumbushe yaliyopita au kuona yatakayotokea wakati ujao. Basi haishangazi kwamba kila siku kwa njia fulani watu hurudi nyuma au kusonga mbele kwa habari ya wakati. Fikiria mfanyabiashara huko Tokyo anayesafiri kwa ndege hadi New York ili kuhudhuria mkutano. Iwapo anaanza safari yake wakati wa adhuhuri na kusafiri bila kutua karibu nusu ya dunia, atawasili mahala anapokwenda asubuhi hiyohiyo, kana kwamba ni kabla ya wakati alipoondoka.
Je, unaweza kusafiri mbali na bado ufike kabla ya wakati ulipoanza safari? La, haiwi hivyo kihalisi. Lakini, majiji yaliyo mbali huwa katika kanda tofauti za wakati. Kwa hakika, mtu anapovuka ule mstari wa tarehe wa kimataifa, ambao ni mstari wa kuwaziwa tu, yeye huvuka mpaka uliokubaliwa ambao hutenganisha tarehe. Hilo ni jambo linalovuruga akili sana! Ni kama kupata au kupoteza siku moja ghafula, ikitegemea unaelekea wapi.
Tuseme yule mfanyabiashara anaanza safari ya kutoka New York kurudi Tokyo Jumanne usiku. Ndege yake itakapotua muda wa saa 14 baadaye, tayari itakuwa siku ya Alhamisi nchini Japani. Ni jambo la ajabu kupoteza siku nzima! Mtu mmoja anayesafiri mara nyingi anasema hivi anapokumbuka mara yake ya kwanza kuvuka mstari wa tarehe wa kimataifa: “Sikuweza kuelewa jinsi nilivyopoteza siku moja. Jambo hilo lilinishangaza sana.”
Kwa kuwa mstari huo wa tarehe huwakanganya wasafiri, huenda watu fulani wakajiuliza ni kwa nini mstari huo ulibuniwa.
Mabaharia Wafanya Uvumbuzi
Uhitaji wa mstari huo wa tarehe waonekana wazi tunapokumbuka yaliyotukia mwaka wa 1522, wakati Ferdinand Magellan na kikosi chake cha mabaharia walipozunguka dunia kwa mara ya kwanza. Baada ya kusafiri kwa miaka mitatu baharini, waliwasili nchini Hispania Jumapili, Septemba 7. Hata hivyo, kitabu cha habari zote za safari yao kilionyesha kwamba siku hiyo ilikuwa Jumamosi, Septemba 6. Hitilafu hiyo ilitokea wapi? Tofauti na watu wa Hispania, wao walikosa kuona jua likichomoza siku moja kwani walizunguka dunia wakielekea magharibi.
Mwandishi Jules Verne alitaja yale yanayotukia wakati mtu anaposafiri akielekea mashariki katika kitabu chake Kuizunguka Dunia kwa Siku Themanini. Mhusika mkuu katika kitabu hicho alipaswa kuzunguka dunia yote kwa siku 80 ili apokee fedha nyingi sana. Mwishoni
mwa safari yake, aliwasili nyumbani akiwa amesikitika kwani alichelewa kwa siku moja na hangeweza kupokea zawadi yake. Alidhani amechelewa. Lakini alishangaa kujua kwamba alikuwa amefika wakati barabara. Kama kitabu hicho kinavyoeleza: ‘Pasipo kujua, Phileas Fogg alikuwa na ziada ya siku moja katika safari yake kwa sababu alikuwa anasafiri kuelekea mashariki kila wakati.’Japo yaonekana kwamba hadithi ya Bw. Verne ilimalizika vizuri kwa sababu ya ule mstari wa tarehe wa kimataifa, mstari huo haukuwepo wakati kitabu hicho maarufu kilipochapishwa mwaka wa 1873. Manahodha wa merikebu wa wakati huo walirekebisha ile tofauti ya siku moja kwenye kalenda zao kila mara walipokuwa wakivuka Bahari ya Pasifiki, lakini mstari wa tarehe wa kisasa haukuwa kwenye ramani zao. Walifanya hivyo kabla ya mfumo wa kanda za wakati kuidhinishwa rasmi ulimwenguni pote. Hivyo, Urusi ilipomiliki Alaska, wenyeji wa Alaska walifuata tarehe ileile iliyofuatwa na wakazi wa Moscow. Lakini mnamo mwaka wa 1867, Marekani iliponunua eneo hilo, Alaska ilipatanisha tarehe zake ziwe kama za Marekani.
Jinsi Mstari Huo Ulivyobuniwa
Mnamo mwaka wa 1884, wakati ambapo kulikuwa na mvurugo huo kuhusu wakati, wawakilishi wa mataifa 25 walikutana mjini Washington, D.C., kwa ajili ya Kongamano la Kimataifa la Meridiani Kuu. Walianza kutumia mfumo wa kanda 24 za wakati duniani pote na wakakubaliana kutumia meridiani kuu, yaani, mstari wa longitudo unaopita huko Greenwich, Uingereza. * Mstari huo ulianza kutumiwa kuonyesha mahala maeneo mbalimbali ulimwenguni yalipokuwa kuelekea mashariki na magharibi.
Ilionekana kwamba ingekuwa vizuri kabisa kuweka ule mstari wa tarehe wa kimataifa katikati ya dunia kutoka Greenwich, yaani, kuhesabu kanda 12 za wakati, mashariki au magharibi. Japo haukukubaliwa rasmi kwenye kongamano hilo la 1884, watu wengi walikubali kwamba mstari wa longitudo wa digrii 180 ulikuwa mahala pazuri kabisa kwani hiyo ingemaanisha kwamba mstari wa tarehe wa kimataifa haungepita katikati ya bara lolote. Hebu wazia jinsi watu wangevurugika iwapo ingekuwa siku ya Jumapili katika sehemu moja ya nchi yenu hali katika sehemu nyingine ya nchi yenu ingekuwa siku ya Jumatatu?
Ukichunguza ramani ya dunia, utaona kwamba mstari wa longitudo wa digrii 180 upo magharibi ya Hawaii. Utagundua mara moja kwamba ule mstari wa tarehe wa kimataifa haufuati longitudo hiyo kabisa. Mstari huo huepuka nchi kavu kabisa kwa kujipinda-pinda kwenye Bahari ya Pasifiki. Na kwa kuwa mstari huo wa tarehe ulikubaliwa bila kufanya mkataba wa kimataifa, unaweza kubadilishwa na nchi yoyote. Kwa mfano, katika mwaka wa 1995, serikali ya Kiribati ilitangaza kwamba mstari wa tarehe wa kimataifa, ambao ulikuwa ukipita katikati ya visiwa hivyo, utapita kando ya kisiwa kilichoko mashariki zaidi ya visiwa hivyo. Hivyo, ramani za kisasa huonyesha visiwa vyote vya Kiribati vikiwa upande mmoja wa mstari huo. Kwa hiyo, visiwa hivyo vina tarehe moja.
Maana ya Mstari Huo
Ili kuonyesha ni kwa nini mtu hupoteza au kupata siku moja anapovuka mstari huo wa tarehe, hebu wazia unazunguka dunia kwa merikebu. Na tuseme unaelekea mashariki. Pasipo kujua, unaendelea kupata saa moja unapovuka kila ukanda wa wakati. Ukimaliza safari yako ya kuzunguka dunia, utakuwa umevuka kanda 24 za wakati. Kama hakungekuwa na mstari wa tarehe wa kimataifa, ni kana kwamba ungefika siku moja mbele ya saa za mahala hapo. Mstari wa tarehe wa kimataifa huondoa tatizo hilo. Ni vigumu kidogo kuelewa jambo hilo, sivyo? Ndiyo sababu yule jamaa Phileas Fogg anayetajwa katika hadithi, na Magellan na kikosi chake walikosea kuhusu siku waliyomaliza safari zao za kuzunguka dunia!
Wale ambao wamevuka mstari huo wanaelewa kabisa hali hiyo ya kiajabu ya kupoteza au kupata siku kwa ghafula. Lakini, kama ule mstari wa tarehe wa kimataifa haungekuwepo, watu wangevurugika akili hata zaidi wanaposafiri.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 11 Kwa habari zaidi kuhusu kanda za wakati na mistari ya longitudo, ona makala yenye kichwa “Hiyo Mistari Yenye Manufaa ya Kuwaziwa” katika gazeti la Amkeni! la Machi 8, 1995.
[Mchoro/Ramani katika ukurasa wa 13]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Machi | Machi
2 | 1
[Picha katika ukurasa wa 14]
Juu: Jengo la Uchunguzi la Greenwich Royal
Kulia: Mstari huu wa jiwe-mango unaonyesha mahala ile meridiani kuu inapopita