Si Balaa, Bali Ni Chakula Kitamu
Si Balaa, Bali Ni Chakula Kitamu
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO
Mkulima atavuna mahindi mengi. Ndiyo sababu anatabasamu huku anapochunguza mahindi shambani mwake. Anang’oa hindi na anaona mara moja doa jeusi. Anapotazama hindi hilo kwa makini anaona kwamba lina punje kubwa sana laini za rangi nyeusi zenye umbo na mpangilio tofauti. Anapozitoboa, kitu hicho cheusi chatoa harufu ya uyoga. Hindi hilo limeathiriwa na kuvu! Je, limeharibika? La. Mkulima anatabasamu kwa furaha. Anatazamia kuvuna uyoga mwingi zaidi!
TANGU hapo kale, wenyeji wa Mexico wamefurahia ladha tamu ya uyoga ambao huathiri mahindi unaoitwa huitlacoche, au ugonjwa wa kuvu ya mahindi. Katika nchi nyingine chakula hicho huonwa kuwa cha kipekee sana.
Uyoga wa huitlacoche hutokana na kuvu inayoitwa ustilago maydis. Kuvu hiyo huathiri karibu kila zao la mahindi ya Zea mays kwa kiwango kikubwa, hasa katika maeneo yenye joto na ukame wa wastani. Watafiti wamepata “asidi tatu kati ya zile asidi nne za amino zinazotokeza ladha ya umami.” * (Journal of Agricultural and Food Chemistry) Uyoga wa huitlacoche ni mtamu kwa sababu una kiasi kikubwa cha wanga zaidi ya viyoga vingine vinavyoliwa. Uyoga huo una viungo vinavyonukia vizuri. Mojawapo ya viungo hivyo ni vanillin. Na ijapokuwa watu hupenda huitlacoche hasa kwa sababu ya ladha yake, uyoga huo unanufaisha mwili pia kwani una vitamini C, fosforasi, kalisi, na virutubishi vingine.
Basi, haishangazi kwamba Waazteki walipenda uyoga huo. Waliuita cuitlacochin, yaani, “uvimbe usio wa kawaida.” Baadaye, jina lake likabadilishwa na kuwa huitlacoche. Huko Mexico, uyoga huo hutiwa katika chapati inayoitwa quesadilla, yaani, chapati iliyokunjwa ya tortilla. Hata hivyo, uyoga huo huwekwa katika vyakula vingine pia, kama vile chapati nyembamba ya maji na mchuzi. Hivi majuzi, watafiti wa chembe za urithi walianza kuchunguza uyoga huo katika maabara ili kutafuta mbinu za kufanya mazao yatokeze uyoga mwingi kama huo kwa ajili ya biashara.
Iwapo uyoga wa huitlacoche unapatikana mahala unapoishi, basi jaribu kutumia maelezo haya ya mapishi. * Utashangaa kuona jinsi uyoga huo ulivyo mtamu sana!
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 5 Neno Umami linatumiwa huko Japani kueleza kile ambacho watu wengine hufikiri ndiyo ladha ya tano, kuongezea zile ladha nne kuu—ladha tamu, yenye chumvi, ya chachu, na kali.
^ fu. 7 Wakati mwingine uyoga wa huitlacoche huuzwa katika mikebe. Huenda uyoga huo wa mkebe uwe umekwisha kutayarishwa. Uyoga huo unapohifadhiwa katika friji, unaweza kubaki bila kuharibika kwa siku 8 hadi 15.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]
Kupika Uyoga wa Huitlacoche
Gramu 500 (au mikebe miwili ya gramu 200) za uyoga wa huitlacoche uliokatwa-katwa vizuri
Kitunguu 1 cha ukubwa wa wastani (karibu kikombe kimoja)
Vidole vya vitunguu-saumu 2-4 vilivyokatwa-katwa vizuri
Vijiko 2 vikubwa vya viungo vya epazote (chenopodium ambrosioides) au giligilani
Vijiko 3 vikubwa vya mafuta ya kupikia
Kijiko 1 kikubwa cha siagi
Chumvi ya kutosha
Kaanga kitunguu na vitunguu-saumu katika mafuta bila kuvibadilisha rangi. Ongeza kiungo cha epazote na uyoga wa huitlacoche. Ongeza siagi na chumvi. Koroga vya kutosha. Funika chakula hicho na ukichemshe kwa dakika 15 hivi, huku ukikoroga mara kwa mara.
Tumia mchanganyiko huo ama ukiwa peke yake au pamoja na nyama na jibini unapotaka kuuingiza katika chapati za tortilla au chapati nyembamba za maji. Pia, unaweza kuongeza supu katika mchanganyiko huo. Au unaweza kusaga mchanganyiko huo ili kufanyiza rojo nzito ambayo italiwa kwa nyama.