Matatu—Gari Maridadi la Usafiri Nchini Kenya
Matatu—Gari Maridadi la Usafiri Nchini Kenya
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA
MGENI yeyote anayetembelea Kenya hakosi kusema mambo mazuri kuhusu safari yake. Hatasahau kamwe mambo aliyoona kama vile ndovu jike akiongoza kundi lake, simba mwenye fahari, na machweo mekundu ya jua. Kuna mambo mengi mbalimbali yanayopendeza. Hata hivyo, katika barabara nyingi za eneo hili, kuna kitu fulani tofauti cha kuvutia—matatu inayobadilika-badilika. Jina hilo larejezea magari fulani ya usafiri wa umma. Kwa kuwa magari hayo yanapendeza, yanatumiwa sana kwa usafiri nchini Kenya.
Kama vile biashara ya matatu inavyostaajabisha, ndivyo na mwanzo wake. Matatu ya kwanza ilikuwa gari zee aina ya Ford Thames. Gari hilo lilikuwa mojawapo ya magari yaliyotumiwa na wanajeshi wa Uingereza nchini Ethiopia wakati wa vita ya pili ya ulimwengu. Katika miaka ya mapema ya 1960, mkazi mmoja wa Nairobi alitumia gari hilo zee kuwapeleka watu jijini na kuwalipisha abiria mapeni matatu tu kwa ajili ya mafuta. * Punde baadaye, wengine wakatambua kumbe magari hayo mazee yangetumiwa kuchuma pesa. Hivyo, magari mengi kama hayo yalitumiwa kubeba abiria 21. Abiria walikaa kwenye mabenchi matatu yaliyokuwa sambamba. Mabenchi hayo yalipangwa kama yale ya malori mazee ya bolekaja ya Nigeria. Kila abiria alilipa nauli ya mapeni matatu kila aliposafiri. Huenda hiyo ndiyo sababu magari hayo yaliitwa matatu—kutokana na neno “tatu.” Tangu wakati huo, magari hayo yamebadilika kabisa, huku miundo ya siku hizi ikiwa tofauti kabisa na yale magari ya zamani yaliyolia kama mikebe. Naam, matatu ya siku hizi ni gari maridadi sana. Gazeti moja la kila siku la Kenya lilisema matatu ni gari ambalo ‘limeundwa kama ndege ya jeti na lina rangi nyingi.’ Gari hilo ni tofauti kabisa na magari yaliyotengenezwa katika vile viwanda vidogo vya miaka ya 1960!
Kusafiri kwa matatu kwaweza kusisimua, hasa dereva anapokata njia ili kuepuka msongamano
wa magari jijini! Acheni tuzunguke kifupi jijini Nairobi kwa matatu, ili tupate msisimuko huo.Umaridadi Unaovutia
Safari yetu yaanza kwenye kituo cha magari hayo. Magari mengi yameegeshwa yakingoja kuanza safari kuelekea sehemu mbalimbali. Ni saa saba mchana na kuna umayamaya wa watu, kila mtu akijaribu kupata matatu itakayompeleka mahala anapoenda. Abiria wengine wanaelekea mashambani, safari ya saa kadhaa. Wengine wanakwenda kilometa chache kutoka katikati ya jiji, labda kupata mlo wa haraka. Naam, matatu zina faida sana.
Je, umeona kwamba matatu nyingi zina rangi kadhaa maridadi? Rangi hizo hazirembeshi tu gari lenyewe. Kuna abiria wanaopenda kusafiri kwa matatu maridadi zaidi. Ukitazama magari hayo kwa makini utagundua kwamba yana majina kadhaa yaliyoandikwa ubavuni. Baadhi ya majina hayo hueleza matukio ya hivi karibuni—kama vile, “El Nino” (Mvua ya El Nino), “Millennium” (Milenia), “The Website,” “Internet,” na “Dot Com.” Majina mengine kama “Meek” (Mpole) na “Missionary” (Mishonari) hueleza sifa nzuri au mafanikio ya wanadamu. Gari jingine linalopendeza kama matatu ni gari la usafiri nchini Ufilipino linaloitwa jeepney. Kwa kupendeza, gari la jeepney lilitumiwa pia katika vita ya pili ya ulimwengu.
Abiria huitwa kwa njia ya kustaajabisha. Makondakta hupiga kelele na madereva hupiga honi zenye sauti tamu hata ingawa kuna vibao kwenye vioo vya mbele vinavyoonyesha wazi mahala magari hayo yanakoelekea. Usishangae kuona vibao vyenye majina “Jerusalem” au “Jericho” katika matatu nyingine. Ukipanda matatu hizo, hutapelekwa Mashariki ya Kati, bali utajikuta katika vitongoji vilivyo mashariki mwa jiji la Nairobi ambavyo huitwa majina hayo ya Biblia. Haishangazi kwamba abiria huwa na kibarua kigumu wanapochagua matatu watakayopanda, kwani makondakta hung’ang’ania abiria, kila mmoja akitaka abiria wapande gari lake!
Karibu ndani ya matatu inayoitwa Strawberry (Stroberi)! Huenda safari hiyo itafurahisha kama vile tunda hilo linavyofurahisha. Yaonekana matatu hiyo inapendwa na wengi kwani imejaa baada ya dakika chache
tu. Abiria wanaburudishwa na muziki mtamu unaotoka kwenye vipaza-sauti vidogo vilivyowekwa juu. Hata hivyo, usifikiri matatu zote ziko hivyo. Nyingine huwa na vipaza-sauti vikubwa sana chini ya viti, vinavyotoa mdundo unaoweza kupasua masikio. Naam, dakika kumi zimepita tangu watu wajaze viti. Lakini, matatu yetu haijasonga hata kidogo. Kwa nini? Ni lazima kijia kilicho katikati ya viti kijazwe na abiria watakaosimama. Punde si punde, gari limeshonana hakuna hata nafasi ya kugeuka. Isitoshe, huenda matatu hiyo itasimama mara kadhaa njiani ili kubeba abiria zaidi.Hatimaye, twaanza safari. Watu wasiojuana hata kidogo wanazungumza kwa shauku, hasa kuhusu matukio ya siku hiyo. Ni kama soko. Lakini, kaa chonjo usije ukasikiliza hadithi hizo kwa makini mno. Wengine huzubaishwa na mazungumzo hayo hata wakajikuta wamepita mahala walipopaswa kushuka.
Tulisema kwamba matatu hubadilika-badilika. Haitumii njia moja maalumu. Dereva anapotaka kufika haraka mahala anapoenda, atatumia njia yoyote ya mkato anayopata. Hata anaweza kutumia njia ya watu wanaotembea kwa miguu—nyakati nyingine wakiponea chupuchupu tu kugongwa. Kazi ya kondakta pia si rahisi. Anajaribu kukusanya nauli kutoka kwa abiria wenye kelele nyingi, wengine wenye vichwa vigumu. Hata hivyo, hana saa za kubishana na abiria ovyoovyo. Ama abiria alipe au matatu isimame mara moja kisha alazimishwe kushuka—nyakati nyingine kwa fujo! Kondakta humfahamisha dereva iwapo kuna abiria wanaotaka kushuka, huku akiwa chonjo kuona wengine wanaotaka kupanda. Yeye humfahamisha dereva kwa kupiga mbinja, kupiga paa la gari, au kupiga kengele iliyo karibu na mlango. Japo kuna vituo maalumu kwa ajili ya magari yote ya usafiri wa umma, matatu yaweza kusimama mahala popote wakati wowote, ili kuwabeba au kuwashusha abiria.
Baada ya kutoka katikati ya jiji, sasa tumefika katika kitongoji kidogo, ambapo abiria wengi wanashuka. Sasa matatu itarudi tena kwenye kile kituo, mahala safari ilipoanzia. Itabeba abiria wengine njiani. Hao pia watahisi kama sisi. Pasipo shaka, tulifurahia kusafiri katika Strawberry, japo kwa msukosuko.
Zitaendelea Kutumiwa
Huku ikikadiriwa kwamba kuna matatu 30,000, biashara hiyo ya usafiri nchini Kenya imebadilika toka zama za lile gari lililotumiwa vitani na kuwa biashara kubwa inayoleta mapato sana. Hata hivyo, kubadilika-badilika kwake kumetokeza matatizo fulani. Kwa mfano, madereva wameshtakiwa kwa kutofuata sheria za barabarani zinazowaongoza madereva wote, na wenye mamlaka wametunga sheria nyingi ili kuwekea biashara hiyo mipaka. Kutokana na hatua hizo, pindi kwa pindi wenye matatu wamegoma, na hivyo kuwataabisha maelfu ya watu wanaotegemea matatu kila siku. Ingawa si watu wote wanaofurahia namna ambavyo matatu hutoa huduma zake, magari hayo huandaa njia nyingine ya usafiri wa haraka kwa watu wa eneo hili wanaopata mshahara mdogo.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Shilingi, sarafu ya fedha inayotumiwa nchini Kenya, ina thamani ya senti 100 za Kenya. Dola moja ya Marekani ina thamani ya shilingi 78 hivi za Kenya.
[Picha katika ukurasa wa 22]
Gari aina ya Ford Thames
[Hisani]
Noor Khamis/The People Daily