Dubu wa Kermode Wenye Rangi Mbalimbali
Dubu wa Kermode Wenye Rangi Mbalimbali
Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Kanada
“Wao husimama kwa miguu yao ya nyuma, wao huketi kwa makalio yao . . . , wao hata hukoroma wanapolala. . . . Ni werevu, ni wadadisi, wao hujifunza haraka na kubadilikana vyema na hali, na ni kana kwamba wana hisia kama zetu.”
MWANABIOLOJIA wa mambo ya wanyama-pori Wayne McCrory alisema yaliyo juu kuhusu mmojawapo wa dubu adimu sana ulimwenguni—yule dubu mweupe-mweusi wa pwani iliyo kaskazini-magharibi mwa Kanada. Fani ya sayansi ilipata kumchunguza dubu huyo kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 1900 kupitia William Hornaday, mshiriki wa Sosaiti ya Elimu ya Wanyama ya New York. Alikuwa akiainisha ngozi za dubu kutoka kwenye jiji la Victoria, British Columbia, alipoona ngozi isiyo ya kawaida. Ilikuwa nyeupe na yenye rangi hafifu ya dhahabu na umbo lake lilifanana na lile la ngozi ya dubu mweusi.
Hornaday alipendezwa sana na uchunguzi huo hivi kwamba alimwuliza Francis Kermode, mkurugenzi wa Jumba la Makumbusho la Mkoa wa British Columbia, amsaidie kupata habari zaidi juu ya jamii hiyo ya dubu ambayo Hornaday alifikiri kuwa ni mpya. Mnamo mwaka wa 1905, Hornaday alimwita dubu huyo Ursus kermodei, yaani, dubu wa Kermode, ili kumthawabisha Kermode kwa ajili ya jitihada zake za kupata habari na vitu vilivyotumiwa katika majaribio.
Dubu wa Kermode ni wa jamii ya dubu weusi. Hata hivyo, si wote walio weusi. Wahindi wanaozungumza lugha ya Tsimshian, wanaoishi kwenye eneo lenye dubu wa Kermode humwita dubu huyo Moksgm’ol, au dubu mweupe. Vilevile, dubu wa rangi ya machungwa, wa kahawia-nyekundu, wa dhahabu, wa manjano nyang’avu, wa kijivu-samawati, na dubu weupe wenye madoadoa ya rangi ya kahawia-nyeusi wameonekana.
Wanabiolojia hawana uhakika kwa nini kuna dubu weupe wa Kermode. Sababu moja iliyodokezwa ni kwamba huenda mabadiliko yasiyo na utaratibu ya chembe za urithi yalitokeza rangi hiyo tofauti. Kwa kweli, dubu mmoja kati ya kila dubu kumi wa Kermode waliopata kuonekana ni mweupe. Kwa hakika, dubu wa Kermode wa pwani ya kaskazini-magharibi ya Pasifiki ya Kanada hawana kifani na wanavutia sana.
Kuzuru Makao ya Dubu wa Kermode
Waweza kuwaona dubu wa Kermode kwenye eneo la kilometa zipatazo 75,000 za mraba. Eneo hilo liko kwenye pwani ya kaskazini ya British Columbia. Ukisafiri umbali wa kilometa 600 kutoka Vancouver kuelekea upande wa kaskazini-magharibi, utafika kwenye Kisiwa cha Princess Royal na eneo la Mlango-bahari wa Douglas karibu na Kitimat. Kilometa 150 hivi kutoka baharini, upande wa kaskazini-mashariki, kuna jamii ya wakataji-miti wa Terrace, karibu na Mto Skeena. Dubu wa Kermode wanapatikana hasa katika eneo hilo. Eneo hilo limesemwa kuwa jangwa lenye wanyama-pori wengi zaidi na mali asili nyingi zaidi katika eneo la Magharibi la Kanada.
Ili upate kumwona mnyama huyo mweupe mzururaji, wahitaji kuwa na kiongozi wa watalii mwenye ujuzi anayefahamu tabia za dubu wa Kermode. Mwezi wa Oktoba ndio wakati mzuri kabisa wa kumwona mnyama huyo, wakati maelfu ya samaki wa samoni wanapotaga mayai mengi kwenye vijito vya British Columbia. Kwenye pindi hiyo inayotukia mara moja kwa mwaka tu, dubu wa Kermode huteremka kutoka kwenye nyanda za juu ili kusherehekea mlo wa samoni. Mtu mmoja aliyejionea jambo hilo, alisema hivi alipofafanua desturi hiyo ya dubu hao: “Wao huteua samaki wanayetaka, wanaweka wayo mmoja juu ya kichwa chake, kisha wanambambua ngozi kuanzia kwenye matamvua hadi chini, na kufunua nyama wanayokula.”
Tabia Zao
Dubu wa Kermode huonekana kuwa wenye urafiki, wanaopenda watu, na wenye kucheza-cheza. Lakini, kwa kweli, kama dubu wengine, waweza kubadilika wakati wowote na kuwa hatari. Yasemekana kwamba hawaoni vizuri. Pua yao ndogo nyembamba na matundu marefu ya pua yameundwa hivi kwamba huwawezesha kunusia harufu za mbali. Ingawa ni kana kwamba wao hutembea kwa kujivuta, wao ni chapuchapu sana. Uchunguzi uliofanywa umeonyesha kwamba wengine wametembea umbali mfupi kwa mwendo unaozidi kilometa 50 kwa saa moja!
Kermode wa kike waliokomaa wana urefu wa kati ya sentimeta 130 hadi 190 na uzani wa kati ya kilogramu 50 hadi 180. Kermode wa kiume ni wakubwa zaidi na wakati mwingine wao huzidi uzani wa kilogramu 200. Kermode hufikia kimo cha sentimeta 250 hadi 275 wanaposimama kwa miguu yao ya nyuma. Pia, wao ni waogeleaji stadi. Afisa mmoja wa doria kwenye eneo la uvuvi, alimwona dubu mmoja wa Kermode akiogelea kutoka kwenye kisiwa cha karibu hadi bara. Aliposogeza mashua yake karibu na dubu huyo, alipigwa na bumbuazi dubu huyo alipopiga mbizi chini ya maji, akirudi juu ili kupata hewa tu.
Wanapokutana na Wanadamu
Dubu wanapotambua kwamba wanadamu huwa na chakula, mara nyingi wao huacha kuwaogopa wanadamu na waweza kuwa wachokozi sana au kuwa hatari. Mara nyingi, dubu wa aina hiyo huuawa. Basi umwonapo dubu msituni kisha akuombe chakula, kumbuka kwamba ukimlisha, mbali na kujihatarisha utakuwa unasababisha dubu huyo afe mapema.
Kwa kumchunguza dubu huyo wa kustaajabisha, twavutiwa na unamna-namna uliopo katika jamii ya dubu. Jinsi kazi za Mungu za uumbaji zilivyo za ajabu na zenye kupendeza! Na mwanadamu ana daraka la pekee kama nini la kuwatunza viumbe hao wanaovutia!
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 27]
Howie Garber/www.wanderlustimages.com