Jinsi Wakristo Walivyotunza Waliokumbwa na Mafuriko Msumbiji
Jinsi Wakristo Walivyotunza Waliokumbwa na Mafuriko Msumbiji
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MSUMBIJI
MAPEMA mwaka jana watazamaji wa televisheni walishangazwa na picha kutoka Msumbiji zilizoonyesha watu wakiwa juu ya miti huku maisha yao yakiwa hatarini kwa sababu ya mafuriko. Mwanamke mmoja alijifungua akiwa juu ya mti na alionyeshwa akiondolewa pamoja na mtoto wake kutoka eneo la hatari na ndege ya helikopta. Hata hivyo, maelfu ya watu walidumu katika hali hiyo kwa siku nyingi—baadhi yao walikaa sehemu zenye nyoka—hadi maji yalipopungua au kuokolewa kwa helikopta.
Msiba huo ulianza wakati mvua kubwa iliponyesha katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo. Baada ya saa kadhaa vitongoji vizima-vizima vilifurika maji. Katika maeneo fulani maji yalifika kwenye paa za nyumba. Barabara ziligeuka kuwa mito yenye kwenda kasi. Maji yalichimba makorongo makubwa na nyumba na magari na vitu vingine vingi vikafagiliwa mbali. Lakini msiba mbaya zaidi ulitukia baadaye.
Mvua ilizidi kunyesha, maji yakifunika eneo lote la kusini mwa nchi. Mvua pia ilikuwa ikinyesha
katika nchi jirani za Afrika Kusini, Zimbabwe, na Botswana. Mito ya Incomati, Limpopo, na Zambezi inayopita Msumbiji kutoka nchi hizo ikielekea baharini, ilisababisha hasara kubwa ilipofurika na maji yake kusambaa kwenye maeneo makubwa ya Msumbiji. Jinsi Wakristo walivyotunza wenzao wakati wa msiba huu ni habari yenye kujenga imani sana.Kukadiria Hasara ya Mwanzoni
Mnamo Februari 9 mwaka jana, wawakilishi wawili kutoka ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova huko Maputo walifunga safari kwenda eneo la kaskazini. Mnamo saa tatu asubuhi walifika katika mji wa Xinavane, ambapo Mto Incoluane ulikuwa umefurika sana. Waliamua kuendelea na safari hadi Xai-Xai, mji mkuu wa mkoa wa Gaza. Hata hivyo, waliona kwamba mji wa Chókwè, ambao kwa kawaida hutatizwa na mafuriko ulikuwa shwari. Hivyo wakaamua kurudi Maputo.
Lakini huko njiani walipokaribia mji wa Xinavane walizuiliwa na polisi. Polisi waliwaonya hivi: “Maji kutoka Afrika Kusini yamefurika na kuziba njia kuu. Hakuna basi wala lori zinazopita njia hiyo.” Barabara ambayo walikuwa wameitumia asubuhi hiyo sasa ilikuwa imefunikwa na maji kabisa! Eneo lote lilikuwa bila njia ya kuwasiliana na sehemu nyingine ya nchi kwa sababu mito mingine ya kaskazini ilikuwa inafurika polepole.
Wawakilishi hao wawili waliamua kulala katika mji wa karibu uitwao Macia. Usiku huo hali ilizidi kuwa mbaya. Mji wote wa Xinavane ulifunikwa na maji na watu wakapoteza mali yao yote. Mipango ilifanywa ili Mashahidi wa eneo hilo wahamishwe hadi kwenye Jumba la Ufalme la Macia ambapo kambi ya muda ya kusaidia wakimbizi ilikuwa imefunguliwa. Mashahidi walifanya hima kwenda madukani kununua mahitaji ya msingi kama vile mchele, maharagwe, unga, na mafuta.
Hali ya Wakristo wenzao katika Chókwè na miji mingine ya karibu iliwatia wasiwasi. Waangalizi wa makutaniko ya Chókwè walikutana na kufanya mipango ya kuwahamisha Mashahidi wote kwa ujumla. Mbiu hii ilivumishwa: “Ondokeni mara moja, mwelekee Macia!” Ilibainishwa upesi kwamba ndugu wengi wa Xinavane hawakuwa wamefika. Kwa hiyo, Mashahidi walitumwa kwenda kuangalia hali yao. Walipata habari kwamba mzee mmoja Mkristo alikuwa amekufa maji nyumbani mwake. Walimzika na Mashahidi wengine waliopatikana, baadhi yao wakiwa juu ya paa wakasaidiwa kuhamia Macia.
Baada ya mipango hiyo kukamilika, wale wawakilishi wawili wa ofisi ya tawi walienda katika mji mdogo wa pwani uitwao Bilene na kukodi ndege na kusafiri hadi Maputo. Wakiwa hewani, wasafiri hao waliona maji kila mahali. Iliripotiwa kwamba katika mkoa wa Gaza pekee, watu zaidi 600,000 walikuwa wameathiriwa.
Hali Yazorota Zaidi
Mnamo siku mbili zilizofuata, mvua iliongezeka na kuharibu maeneo yaliyoko katikati mwa Msumbiji. Kisha kimbunga cha kitropiki kiitwacho Eline kikazuka. Mnamo Februari 20, kimbunga hicho kikamimina mvua kwenye mikoa ya Inhambane, Sofala, na Manica. Matokeo yalikuwa ongezeko la mafuriko, maafa na uharibifu.
Kisha kuelekea mwisho wa mwezi wa Februari, mji wa Chókwè na maeneo yote yanayozunguka yalifurika maji kwa namna ambayo haikuwahi kuonekana. Kuelekea usiku wa manane hivi Jumamosi, Februari 26 maji yalifika yakiwa kama mto mkubwa na kufagilia mbali kila kitu. “Tuliamshwa na jirani aliyekuwa akipiga kelele dirishani,” asimulia Luis Chitlango, Shahidi mwenye umri wa miaka 32.
Chitlango alieleza hivi: “Tulipokuwa tukitoka haraka-haraka kitandani, tuliweza kusikia mngurumo wa maji. Tulipokuwa tukikimbia tuliona nyoka wengi njiani. Tulifika kwenye sehemu kavu saa 12 asubuhi, lakini baadaye asubuhi hiyo maji yalizidi kuwa mengi
kila upande na ikatubidi kupanda juu ya miti. Tulikuwa kundi la watu 20.“Wanaume walitangulia kupanda mitini. Kisha wanawake wakawapokeza watoto na wakafungwa kwenye matawi. Hatimaye wanawake walipanda juu ya miti pamoja na watoto wachanga. Mara kwa mara tuliteremka chini na kupekua udongo ndani ya maji kutafuta njugu kwa sababu tulifahamu kwamba zao hilo hukuzwa eneo hilo.
“Baada ya kuwa pale kwa siku tatu iliamuliwa kwamba watu wote watembee hadi Chókwè. Maji yalifika kifuani na tulikabili mikondo ya maji yenye nguvu. Njiani tuliwaona watu wengi wakiwa juu ya miti na juu ya paa. Siku iliyofuata maji yalikuwa yamepungua kiasi cha kuruhusu malori kufika mjini na kubeba watu hadi mji wa Macia.”
Kambi ya Wakimbizi ya Mashahidi
Mnamo Machi 4, ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ilikodi ndege na kuwapeleka wawakilishi kwenye eneo lililokumbwa na msiba. Idadi kubwa ya watu ilikuwa imekimbilia Macia, na kuugeuza mji huo kuwa kambi kubwa sana ya wakimbizi. Wakimbizi wengi walisumbuliwa na homa, utapiamlo, malaria, na maradhi mengine.
Eneo hilo lilifanana na uwanja wa vita. Ndege za helikopta, za nchi mbalimbali, zilizagaa hewani na kutua kwenye viwanja vilivyotengenezwa haraka-haraka ili kuteremsha mizigo. Kundi la msaada la Mashahidi lilipofika Macia, mipango ya kulisha wahasiriwa na kufungua hospitali ndogo ilifanywa. Lakini kwanza waliomba kibali cha wenye mamlaka wa mji ambao walisifu sana mpango huo.
Katika kambi yenye watu takriban 700 waliotia ndani Mashahidi na watu wengine, andiko la Biblia lilisomwa kila asubuhi saa 12:30. Dada Wakristo walipomaliza kupika chakula, majina ya vichwa vya familia yaliitwa. Kila mmoja wao alionyesha kwa ishara ya vidole kiasi cha sahani alizohitaji, na chakula kilipelekwa mahali alipo.
Kila jambo kambini lilifanywa kwa utaratibu. Watu fulani walipewa daraka la kununua chakula, wengine kutunza usafi na maji ya kunywa, wengine kuosha vyoo na kadhalika. Maofisa wa serikali walipoona utaratibu huo walisifu hivi: ‘Hapa ni mahali pafaapo sana. Hakuna mtu anayelala njaa, wala hapana ugomvi.’ Mtu mmoja mwenye mamlaka alisema hivi: ‘Ingefaa kila mtu azuru kambi ya Mashahidi ili ajionee jinsi mambo yanavyopasa kuendeshwa.’
Siku moja halmashauri ya kutoa msaada ilikutana na wazee Wakristo na kuwaarifu kwamba ofisi ya tawi ilikuwa imefanya mipango ya kujenga upya nyumba na Majumba ya Ufalme pamoja na kuwapa wahasiriwa vitu vingine muhimu wanavyohitaji. Mpango huo ulitangazwa wakati wa kusoma andiko la Biblia asubuhi iliyofuata. Ndugu walishangilia sana.
Ingawa wenye mamlaka walikuwa wameleta hema mbili kubwa bado wengi walikuwa wakilala nje. Kwa hiyo, kikundi kutoka miongoni mwa wakimbizi kilipangwa ili kujenga Jumba kubwa la Ufalme kwenye uwanja wa kutaniko la hapo. Jumba hilo lilijengwa kwa matete na mabati—aina ya ujenzi wa Msumbiji—likiwa na nafasi ya watu 200. Ujenzi ulikamilika kwa siku mbili tu!
Kutafuta Wengine
Wakati huohuo, mnamo Machi 5, baada ya maji kupungua kwa kiasi fulani, kikundi cha kutoa msaada kilitumwa hadi mji wa Aldeia da Barragem ulio kwenye eneo lililokuwa limekumbwa na maji mapema. Katika mji huo kulikuwa na kutaniko la Mashahidi 90 na hawakujulikana waliko.
Wakiwa njiani, walipitia kwenye kambi kubwa ya wakimbizi iitwayo Chihaquelane iliyokuwa na watu 100,000 hivi. Maji yalikuwa yamefunika pande zote za barabara iliyokuwa imeharibiwa vibaya sana na maji. Mshiriki mmoja wa kikundi hicho alisema: “Tulipofika tulipata mji wa Chókwè ulikuwa ukiwa. Nyumba nyingi zilizokuwa kwenye mwingilio wa mji bado zilikuwa zimefunikwa na maji hadi kwenye paa. Nyumba nyingine nyingi zilikuwa zimefunikwa kabisa na maji. Usiku ulikuwa wakaribia na bado ilisalia safari ya kilometa 25 kufika Aldeia da Barragem.”
Usiku huo kikundi hicho kiliwasili Aldeia da Barragem. Mshiriki mmoja wa kikundi hicho akumbuka hivi: “Tuliduwaa tusijue la kufanya.” Kisha watu wakatokea, wakipaaza sauti: “Ndugu!” na kikazuka kicheko kikubwa cha furaha. Watu walipoona taa za magari mawili, Mashahidi waliwaza mara moja kwamba huenda ikawa ni ndugu zao, na wakajulisha wengine jambo hilo. Watu walioshuhudia walistaajabu na kusema hivi: ‘Watu hawa wanapendana kikweli. Wameleta chakula na hata wamezuru!’
Kutoa Msaada Mfululizo
Hao Mashahidi wa Aldeia da Barragem walisafirishwa hadi kambi ya Macia ambako walipewa chakula, makao na matibabu. Wakati huo hali katika Macia ilizidi kuzorota. Chakula, dawa, na fueli ziliadimika kwa sababu zililetwa humo kwa ndege. Kulikuwa na uhitaji mkubwa wa kufungua barabara kati ya Macia na Maputo. Jambo hilo lilifanyika mnamo Machi 8.
Mji mkubwa wa Xai-Xai ulikuwa umekumbwa kabisa na mafuriko. Maji yalikuwa na kina cha meta tatu katika sehemu fulani-fulani katikati mwa mji! Mashahidi waliunda halmashauri ya kutoa msaada ili ishughulikie mahitaji ya ndugu waliokuwa huko. Halmashauri nyingine ziliundwa ili kufanya kazi hiyo katika mikoa ya Sofala na Manica.
Mashahidi kutoka nchi nyingine walituma msaada. Kwa mfano, ofisi ya tawi ya Afrika Kusini ilipanga kusafirishwa kwa tani nyingi za nguo, blanketi, na vitu vingine. Na makao makuu ya Mashahidi wa Yehova huko Brooklyn, New York, yalituma pesa za kutunza wale walioathiriwa na msiba huo.
Baada ya maji kupungua na idadi ya Mashahidi ambao nyumba zao ziliharibiwa kujulikana, kazi ya kujenga upya nyumba zao na Majumba ya Ufalme ilianza. Halmashauri ya ujenzi iliundwa na kazi hiyo ikaanza mara moja kwa msaada wa wajitoleaji wengi. Tangu wakati huo, zaidi ya nyumba 270 na angalau Majumba matano ya Ufalme yamejengwa upya.
Nyumba za kwanza kujengwa na Mashahidi zilipoanza kukamilika watu walivutiwa. Jirani mmoja alisema hivi: ‘Mnaabudu Mungu aliye hai. Viongozi wa dini yetu hawajali kondoo wao wenye kuteseka. Lakini nyinyi mmejengewa nyumba hizi nzuri.’ Kwenye maeneo hayo, watu wengi wamekubali ujumbe wa Ufalme unaotangazwa na Mashahidi wa Yehova, na mafunzo kadhaa ya Biblia yameanzishwa.—Mathayo 24:14; Ufunuo 21:3, 4.
Ijapokuwa Mashahidi wengi walipoteza mali zao zote za kimwili hakuna aliyepoteza imani yake. Badala yake, imani yao kwa Yehova Mungu na kwa ushirika wa ulimwenguni pote wa waamini wenzao ilitiwa nguvu. Wana shukrani nyingi kwa udugu wa kimataifa wenye upendo ambao ulitenda haraka wakati wa msiba huo mbaya sana. Wameona kibinafsi utunzaji mwororo na ulinzi wa Yehova. Nao watakumbuka daima maneno haya ya Biblia: “Mwenyezi-Mungu ni mkuu,”—Zaburi 48:1, BHN.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mji wa Xai-Xai ulifurika maji ya tope
[Picha katika ukurasa wa 25]
Bidhaa za msaada zililetwa kwa ndege
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kundi la msaada la Mashahidi lilifungua hospitali ndogo
[Picha katika ukurasa wa 26]
Ujenzi wa nyumba waendelea
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kambi kubwa zaidi ilikuwa na wakimbizi 100,000