Maharamia wa Skandinavia Washindi na Wakoloni
Maharamia wa Skandinavia Washindi na Wakoloni
ILIKUWA siku moja ya mwezi wa Juni mwaka wa 793 W.K. Watawa wa kiume katika kisiwa kidogo cha Lindisfarne, kinachoitwa pia Holy, kilicho kwenye ufuo wa mwambao wa Northumberland, Uingereza, walikuwa kwenye shughuli zao za kawaida, bila kujua kwamba mashua maridadi na fupi zilikuwa zikija kasi mawimbini. Mashua hizo zilifika upesi ufuoni, na wanaume wenye ndevu na sura za kuogofya waliobeba panga na mashoka mikononi wakashuka hima na kukimbia wakielekea kwenye makao ya watawa wa kiume. Wakashambulia watawa hao waliokuwa na hofu nyingi na kuwaua wengi. Wavamizi hao walipora dhahabu, fedha, vito, na hazina nyingine kutoka makao hayo ya watawa. Kisha wakarejea katika Bahari ya Kaskazini na kutoweka.
Waporaji hao walikuwa Maharamia wa Skandinavia, na mbinu zao katili za kushambulia na kukimbia zilivuma sana katika Ulaya na zikaja kuashiria mwanzo wa muhula wa Maharamia wa Skandinavia. Punde si punde hofu ya Maharamia hao wa Skandinavia ikawa kuu sana hivi kwamba kotekote Uingereza sala hii ikawa ya kawaida: “Tuokoe na hasira ya Watu wa kaskazini, Ee Bwana.” *
Maharamia hao wa Skandinavia walikuwa nani? Mbona waliibuka ghafula tu na kuandikwa kwenye historia, wakawa mashuhuri kwa karne tatu, kisha kutokomea?
Wakulima na Waporaji
Mababu wa Maharamia wa Skandinavia walikuwa watu wa makabila ya Kijerumani, ambao miaka 2,000 kabla ya muhula wa Maharamia wa Skandinavia, walianza kuhama kaskazini-magharibi mwa Ulaya na kuingia Denmark, Norway, na Sweden—Skandinavia. Kama ilivyokuwa na mababu zao, Maharamia wa Skandinavia walikuwa wakulima, hata wale walioenda kuvamia. Katika maeneo baridi zaidi ya Skandinavia, walitegemea zaidi kuwinda, kuvua samaki, na kuvua nyangumi. Maharamia wa Skandinavia waliokuwa wanabiashara waliishi katika vijiji vikubwa zaidi, na kutoka huko walisafiri kwenye njia kuu za biashara za Ulaya wakitumia mashua zao imara. Ni nini basi, kilichofanya watu walioonekana
wasioweza kudhuru wageuke na kuwa wabaya sana katika kizazi kimoja tu?Mojawapo ya sababu ni kuongezeka kwa watu kupita kiasi, lakini wanahistoria wengi huhisi kwamba hilo lingekuwa tatizo tu huko magharibi mwa Norway ambako mashamba yalikuwa haba. Kichapo The Oxford Illustrated History of the Vikings chasema hivi: “Maharamia wengi wa Skandinavia wa mapema walitafuta utajiri, wala si mashamba.” Jambo hilo lilikuwa muhimu zaidi kwa wafalme na wakuu waliohitaji mali nyingi ili kudumisha utawala wao. Maharamia wengine wa Skandinavia waliondoka huko ili kuepuka mizozo ya kifamilia na vita vya kijamii.
Sababu nyingine huenda ilikuwa ni zoea la Maharamia wa Skandinavia matajiri kuwa na zaidi ya mke mmoja. Kwa sababu hiyo, wakaja kuwa na watoto wengi. Hata hivyo, kwa kawaida ni mwana wa kwanza tu aliyepewa urithi wote wa familia, hivyo iliwabidi watoto wengine wadogo wajikimu. Kulingana na kitabu The Birth of Europe, wana ambao hawakurithi mali “walifanyiza kikundi kikubwa na chenye wapiganaji hatari waliolazimika kujikimu kwa njia yoyote ile, iwe ni kwa kuwanyang’anya mali watu wa nchi yao au kupitia uharamia katika nchi za kigeni.”
Maharamia wa Skandinavia walikuwa na chombo cha usafiri kilichofaa katika kushambulia na kukimbia—mashua ndefu. Wanahistoria husifu mashua hiyo ndefu kuwa mojawapo ya vyombo bora vya kiufundi vya mapema katika Enzi za Kati. Vikiwa na kina cha kadiri na kuendeshwa kwa tanga au makasia, vyombo hivyo maridadi vilisaidia Maharamia wa Skandinavia kuwa weledi wa kila bahari, kila ziwa, na kila mto katika eneo lote.
Kusambaa kwa Maharamia wa Skandinavia
Wanahistoria fulani husema kwamba muhula wa Maharamia wa Skandinavia ulianza katikati ya karne ya nane, kabla tu ya Maharamia hao kuvamia Lindisfarne. Vyovyote vile, kuvamiwa kwa Lindisfarne kulihamasisha watu juu ya Maharamia wa Skandinavia. Baada ya kushambulia Uingereza, waligeukia Ireland na kwa mara nyingine shabaha yao ikiwa makao ya watawa yenye mali nyingi. Mashua zao ndefu zikiwa zimejazwa shehena waliyopora na watumwa, Maharamia hao walifunga safari ili kuwa nyumbani wakati wa majira ya baridi kali. Hata hivyo, katika mwaka wa 840 W.K., Maharamia hao waliacha mtindo huo wakawa wanakaa katika eneo walilokuwa wamepora ikiwa majira ya baridi kali yangewapata huko. Mji wa Dublin katika Ireland hasa ulianzishwa na Maharamia hao ukiwa makao yao ya kwanza ya kigeni. Katika mwaka wa 850 W.K., walianza pia kuishi Uingereza katika majira ya baridi kali, kituo chao cha kwanza kikiwa Kisiwa cha Thanet katika mlango wa Mto Thames.
Punde si punde Maharamia kutoka Denmark na Norway wakafika kwenye Visiwa vya Uingereza, sasa wakiwa si vikundi vya kushambulia na kukimbia, bali wakiwa vikosi kwenye misafara ya mashua ndefu za kivita. Yawezekana baadhi ya mashua hizo zilikuwa na urefu wa meta 30, na huenda zilibeba takriban wapiganaji 100. Katika miaka iliyofuata, Maharamia wa Skandinavia wakatiisha eneo la kaskazini-mashariki la Uingereza, eneo lililokuja kujulikana kama Danelaw, kwa sababu utamaduni na sheria ya Denmark ilienea sana huko. Hata hivyo, kusini mwa Uingereza katika Wessex, Mfalme Alfred Msaksoni na wafalme warithi waliwakomesha Maharamia wa Skandinavia. Lakini hata hivyo, baada ya vita kubwa huko Ashington katika mwaka wa 1016, na kifo cha Mfalme Edmund wa Wessex mwaka huohuo, Canute, kiongozi wa Maharamia wa Skandinavia—aliyedai kuwa Mkristo—akawa mfalme pekee wa Uingereza.
Kotekote Ulaya na Kwingineko
Katika mwaka wa 799 W.K., Maharamia wa Skandinavia wa asili ya Denmark walianza kuvamia eneo lililojulikana wakati huo kama Frisia—eneo la mwambao la Ulaya ambalo lilienea kutoka Denmark hadi Uholanzi. Kutoka huko walipiga makasia yao katika mito kama ya Loire na Seine na kuvamia miji na vijiji iliyokuwa katikati ya Ulaya. Katika mwaka wa 845 W.K., Maharamia hao hata waliupora mji wa Paris. Mfalme Mfranka Charles the Bald aliwapatia pauni 7,000 za fedha ili waondoke mji
huo. Lakini walirudi na kuvamia si Paris tu bali pia Troyes, Verdun, na Toul.Maharamia wa Skandinavia walisafiri hadi Hispania na Ureno, ambapo shambulio lao la kwanza lenye kujulikana lilitukia mwaka wa 844 W.K. Walipora miji kadhaa midogo na hata walimiliki mji wa Seville kwa muda. “Hata hivyo,” chasema kichapo Cultural Atlas of the Viking World, “walinzi Waarabu walikinza mashambulizi kwa bidii sana na kuwakomesha upesi Maharamia hao, nusura majeshi yao yaangamizwe.” Ingawa hivyo, walirudi tena katika mwaka wa 859 W.K.—wakati huo wakiwa na msafara wa meli 62. Baada ya kuvamia sehemu fulani-fulani za Hispania, walivamia Afrika Kaskazini; na ingawa meli zao zilikuwa zimejaa pomoni shehena waliyokuwa wameiba, walisafiri hadi Italia na kuvamia Pisa na Lina (awali uliitwa Luna).
Maharamia wa Skandinavia kutoka Sweden walisafiri mashariki kuvuka Bahari ya Baltiki na kuingia kwenye baadhi ya njia za majini zilizo kuu katika Ulaya Mashariki—mito ya Volkhov, Lovat’, Dnieper, na Volga. Hatimaye njia hizo ziliwapeleka hadi Bahari Nyeusi na kwenye nchi zenye utajiri za milki ya Byzantium. Maharamia fulani wafanya-biashara hata walifika Baghdad kupitia Mto Volga na Bahari ya Kaspiani. Hatimaye, wakuu wa Maharamia hao kutoka Sweden wakaja kuwa watawala wa nchi kubwa za Kislavu za Dnieper na Volga. Wavamizi hao waliitwa Rus, neno ambalo watu fulani hudai kuwa asili ya neno “Urusi”—“Nchi ya Rus.”
Kuelekea Iceland, Greenland, na Newfoundland
Maharamia wa kutoka Norway walikazia fikira visiwa vingi vya mbali. Kwa mfano, walimiliki visiwa vya Orkney na vya Shetland katika karne ya nane na katika karne ya tisa wakamiliki visiwa vya Faeroe, vya Hebride na mashariki mwa Ireland. Maharamia hao walimiliki hata Iceland. Huko walianzisha bunge iliyoitwa Althing. Bunge hiyo ya Althing ambayo ingali inatawala huko Iceland, ndiyo bunge ya awali zaidi katika nchi za Magharibi.
Katika mwaka wa 985 W.K., Haramia aliyeitwa Erik the Red alianzisha koloni katika Greenland. Baadaye mwaka huohuo, Haramia mwenzake Mnoweji aliyeitwa Bjarni Herjolfsson aliondoka Iceland ili kujiunga na wazazi wake huko Greenland. Lakini alipeperushwa na upepo na kupelekwa mbali zaidi ya Greenland. “Bjarni huenda akawa Mnoweji wa kwanza kuliona bara la Amerika Kaskazini,” chasema kichapo Cultural Atlas of the Viking World.
Kwa msingi wa ripoti ya Bjarni, na labda baada ya mwaka wa 1000, Leif Eriksson, mwana wa Erik the Red, alisafiri kwa mashua kutoka Greenland kuelekea magharibi hadi Kisiwa cha Baffin na kuteremka pwani ya Labrador. Alifika kwenye rasi aliyoipa jina la Vinland, kutokana na zabibu au matunda-mwitu yaliyokuwa yakikua mahali hapo. * Leif alikaa hapo wakati wa majira ya baridi kali kabla ya kurudi zake Greenland. Mwaka uliofuata, kaka yake Leif aitwaye Thorwald aliongoza kikundi cha uvumbuzi hadi Vinland, lakini aliuawa walipokuwa wakipigana na wenyeji. Hata hivyo, miaka michache baadaye, kati ya Maharamia 60 na 160 walianzisha makazi katika Vinland, lakini kwa sababu ya uhasama na wenyeji, walikaa pale kwa miaka mitatu hivi, na hawakuwahi kurudi huko tena. Ilipita takriban miaka 500, kabla ya mvumbuzi mmoja Mwitalia John Cabot, kulitangaza bara la Amerika Kaskazini kuwa koloni ya Uingereza.
Mwisho wa Muhula wa Maharamia wa Skandinavia
Kufikia mwisho wa muhula wao, Maharamia wa Skandinavia walikuwa wameanzisha nchi kadhaa zenye kutawaliwa na wafalme wa Skandinavia. Lakini hawakubaki wakiwa wageni daima, kwa sababu hatimaye Waskandinavia wengi walifuata tamaduni na hata dini za wenyeji. Kwa mfano, Rollo, mtawala Mskandinavia, aliyenyakua sehemu ya eneo la mwambao wa Ufaransa linaloitwa Normandy (maana yake “Nchi ya Northmen,” au Normans), aligeuza imani akawa Mkatoliki. Mmoja wa wazao wake alikuwa William, Dyuki wa Normandy. Baada ya vita ya Hastings ya wenyewe kwa wenyewe ya mwaka wa 1066, iliyopiganwa kati ya wazao wa Norman na Maharamia wa Skandinavia wenyeji wa Uingereza, Dyuki William aliyekuwa mshindi alitawazwa kuwa mfalme wa Uingereza.
William alizuia kwa hima uvutano wowote wa Waskandinavia kuingia Uingereza na akaanzisha muhula mpya wa jamii ya kikabaila uliotia ndani mfumo wa kutawala, umilikaji-mashamba, mfumo wa kibiashara wa Ufaransa ya enzi za kati. Kwa hiyo, “ikiwa tarehe fulani ingechaguliwa ili kutia alama mwisho wa Muhula wa Maharamia wa Skandinavia,” chasema kitabu The Vikings, cha Else Roesdahl, “basi ungekuwa mwaka wa 1066.” Katika karne ya 11 falme za awali za Waskandinavia zilibadilika kuwa nchi huru.
Karne tatu za historia ya Maharamia wa Skandinavia zimejaa matukio mengi. Na bado, wazo la kwamba Maharamia wa Skandinavia walikuwa tu washambuliaji wakatili wenye kubeba panga na shoka si kamili. Walithibitika pia kuwa wenye kubadilikana kwa kufanya nchi za mbali kuwa koloni hatimaye na hata kufuata tamaduni za wenyeji. Wakiwa wakulima waliishi kwenye makazi ya kudumu, na wakiwa watawala walitawala nchi za kigeni. Naam, Maharamia wa Skandinavia, walithibitika kuwa si weledi tu wa kuabiri na wa upanga, bali pia weledi wa plau na wa mambo ya kisiasa pia.
[Maelezo ya chini
^ fu. 3 Nje ya Skandinavia Maharamia hao walipewa majina kama vile makafiri, Wadenmark, Watu wa kaskazini, au Wanoweji. Na kwa sababu wanahistoria wengi wa kisasa wanatumia mtajo “Maharamia wa Skandinavia” kuwahusu wakazi wote wa nchi za Skandinavia walioishi muhula wa Maharamia hao, tumetumia mtajo huo katika makala hii. Asili ya mtajo “Maharamia wa Skandinavia” haijulikani.
^ fu. 20 Katika L’Anse aux Meadows kaskazini kabisa ya Newfoundland, majengo ya Waskandinavia yaliyofunikwa na majani yamerekebishwa upya, ujenzi huo ulitegemea uthibitisho wa kiakiolojia uliopatikana mahali hapo mapema miaka ya 1960. Uthibitisho huo waonyesha kwamba Maharamia wa Skandinavia waliishi mahali hapo yapata miaka 1,000 awali, lakini kuna tashwishi kama makazi hayo yalikuwa sehemu ya nchi ya kihekaya ya Vinland.—Ona Amkeni!, la Julai 8, 1999.
[Sanduku katika ukurasa wa 27]
DINI YA MAHARAMIA WA SKANDINAVIA
Maharamia wa Skandinavia waliabudu miungu wengi wa kihekaya, kutia ndani Odin, Thor, Frey, Freya, na Hel. Odin mungu wa hekima na vita, ndiye aliyekuwa mungu mkuu. Mke wake alikuwa Frigga. Thor alikuwa muua-majitu na mtawala wa upepo na mvua. Frey alikuwa mungu asiye na adili wa amani na uzazi. Freya, dada yake alikuwa mungu wa kike wa mapenzi na uzazi. Hel alikuwa mungu-mke wa ulimwengu wa wafu.
Hekaya za Waskandinavia ndiyo msingi wa majina ya baadhi ya siku za juma katika Kiingereza na katika baadhi ya lugha nyinginezo. Jumanne (Tuesday) ni siku ya Tyr, mwana wa Odin (anayeitwa pia Woden); Jumatano (Wednesday) ni siku ya Woden, Alhamisi (Thursday), siku ya Thor, na Ijumaa (Friday) ni siku ya Frigga.
Sawa na watu wenye kuiabudu, ilidhaniwa kwamba miungu ya Maharamia wa Skandinavia ilipata utajiri wao kupitia wizi, uhodari, na hila. Odin aliahidi kwamba watu waliokufa kishujaa vitani wangeingia katika makao ya kimbingu ya Asgard (makao ya miungu), katika ukumbi mkuu wa Valhalla. Huko wangeweza kula na kupigana wapendavyo. Wakuu wa Maharamia wa Skandinavia walizikwa pamoja na mashua au na mawe yaliyopangwa kushabihi mashua. Chakula, silaha, mapambo, mizoga ya wanyama, na labda mtumwa aliyetolewa kafara alizikwa pia. Malkia alizikwa pamoja na mjakazi wake.
Kofia ya chuma yenye pembe inayohusianishwa na Maharamia wa Skandinavia ni ya awali kuliko muhula wa Maharamia hao kwa zaidi ya miaka 1,000 na ilivaliwa tu wakati wa sherehe. Maharamia wapiganaji walivaa kofia sahili ya chuma au ya ngozi yenye umbo la pia iwapo walipendelea kuvaa kofia.
[Ramani katika ukurasa wa 26]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
KUSAMBAA KWA MAHARAMIA WA SKANDINAVIA
NORWAY
↓
ICELAND
GREENLAND
Kisiwa cha Baffin
Labrador
Newfoundland
DENMARK
↓
UINGEREZA
IRELAND
UHOLANZI
UFARANSA
URENO
HISPANIA
AFRIKA
ITALIA
SWEDEN
↓
URUSI
Bahari ya Kaspiani
Baghdad
UKRAINIA
Bahari Nyeusi
Istanbul
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mfano wa Mashua ndefu ya Maharamia wa Skandinavia
[Hisani]
Ukurasa wa 2 na wa 24: Antonion Otto Rabasca, Courtesy of Gunnar Eggertson
[Picha katika ukurasa wa 25]
Silaha za Maharamia wa Skandinavia
Kofia ya chuma ya Maharamia wa Skandinavia
[Hisani]
Silaha na kofia ya chuma: Artifacts on display at the Museum of National Antiquities, Stockholm, Sweden
[Picha katika ukurasa wa 27]
Leif Eriksson