Wahasiriwa Wanaobadilika wa Vita
Wahasiriwa Wanaobadilika wa Vita
“VITA vya siku hizi ni tofauti na vile vya zamani . . . Ni raia wa kawaida, badala ya wanajeshi,” ambao wanahasiriwa zaidi, ikaripoti programu ya utangazaji ya Redio ya UM iitwayo “Perspective.” Mathalani, wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, ni asilimia 5 tu ya watu waliouawa vitani ambao walikuwa raia. Hata hivyo, wakati wa vita ya ulimwengu ya pili, idadi ya raia waliouawa iliongezeka hadi asilimia 48. Na leo, ikasema Redio ya UM, “karibu watu wote wanaouawa kwenye vita ni raia—asilimia 90—na wengi wao ni wanawake, watoto na wazee-wazee.”
Kulingana na Olara Otunnu ambaye ni katibu mkuu Mwakilishi wa Pekee wa UM kwa ajili ya Watoto na Mapambano ya Kivita, “watoto wakadiriwao kuwa milioni mbili wameuawa katika hali za mapambano ya kivita tangu 1987.” Hiyo yajumlika kuwa zaidi ya watoto wahasiriwa wa vita 450 kwa siku katika miaka zaidi ya 12 iliyopita! Kwa kuongezea, wakati huohuo, zaidi ya watoto milioni sita wameumizwa vibaya au kulemazwa kabisa.
Njia moja ambayo UM ungeweza kupunguza idadi inayoongezeka ya watoto wanaouawa vitani, akadokeza Bw. Otunnu, ni kukuza maeneo ya amani. “Mahali ambapo watoto huwa wengi, kama vile shuleni, hospitalini, na viwanjani, panapasa kuonwa kuwa maeneo yasiyo ya vita.” Hata hivyo Redio ya UM iliongezea kusema, “kuzuia mapambano kwanza” ndiyo njia yenye matokeo zaidi ya UM kuhakikisha kwamba raia wa kawaida hawauawi wakati wa vita. Kwa kweli, ili kuzuia kabisa watu wasiuawe vitani jambo hilo lataka vita yenyewe iondoshwe. Hilo litapata kutokea?
Kwa sababu ya rekodi ndefu ya binadamu ya vita, watu wengi kwa kufaa huhisi kwamba binadamu hawataleta amani kamwe duniani. Hata hivyo, Neno la Mungu, Biblia, huahidi kwamba Yehova Mungu atafanya hivyo: “Avikomesha vita hata mwisho wa dunia.” (Zaburi 46:9) Hilo litatokea lini? Na kwa nini unaweza kuwa na hakika kwamba ahadi ya Mungu ya kuleta amani ulimwenguni pote itatimia? Ukitaka kupata jibu la maswali haya, tafadhali andikia wachapishaji wa gazeti hili, ukitumia anwani ya karibu zaidi nawe iliyoorodheshwa kwenye ukurasa wa 5, au uwasiliane na Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova lililo karibu nawe. Hakuna wajibu wala malipo—utapata majibu moja kwa moja.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
UN PHOTO 156450/J. Isaac