Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unyoaji Laini Kabisa

Unyoaji Laini Kabisa

Unyoaji Laini Kabisa

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA AUSTRALIA

IIKIWA mtu hutumia dakika tano kwa siku kunyoa na hufanya hivyo kila siku kwa miaka 50, atakuwa ametumia siku zaidi ya 63 tu maishani mwake kunyoa ndevu zake! Wanaume huhisije kuhusu zoea hili la kila siku?

Ukaguzi usio rasmi wa hivi karibuni ulitoa maoni haya kuhusu kunyoa: “Sipendi kunyoa.” “Nakuchukia.” “Ni mojawapo ya mambo hatari maishani.” “Ni jambo la kuepukwa unapoweza kufanya hivyo.” Ikiwa baadhi ya wanaume huhisi hivyo kuhusu kunyoa ndevu zao, kwa nini wao hunyoa? Acheni tujifunze zaidi kuhusu kunyoa. Labda tutapata jibu.

Kutoka Kaa la Chaza Hadi Nyembe Zinazoweza Kutupwa

Je, unaweza kuwazia kunyoa kwa kutumia kaa la chaza? Jino la papa? Labda kipande chembamba chenye makali cha jiwe gumu sana? Wanadamu wamedhihirisha ubunifu mkubwa sana katika kuteua vifaa vya kunyolea! Katika Misri ya kale, wanaume walinyoa kwa kutumia wembe wa shaba uliofanana na shoka dogo. Hivi karibuni zaidi, katika karne ya 18 na 19, vifaa vilivyojulikana kuwa vyaweza kukata koo vilitengenezwa, hasa katika Sheffield, Uingereza. Nyembe hizo ambazo mara nyingi zilitiwa madoido zilikuwa na ubapa wa feleji uliobonyea ambao ulikunjwa kwa njia salama ndani ya mpini wakati zilipokuwa hazitumiwi. Vifaa hivyo vilihitaji kutumiwa kwa uangalifu sana, na kabla mtu hajazoea kuvitumia bila shaka alijikata mara nyingi na kutokwa damu. Kwa watu ambao hawakuwa na ujuzi sana, lazima wawe walifadhaika sana walipovitumia kwa mara ya kwanza. Hata hivyo, karne ya 20 ilitokeza kitulizo.

Mnamo mwaka wa 1901 mwanamume mmoja huko Marekani aliyeitwa King Camp Gillette alibuni wembe salama wenye ubapa unaoweza kutupwa. Wazo lake lilikubaliwa haraka sana ulimwenguni na hatimaye likaongoza kwenye mbinu za namna mbalimbali, kutia ndani nyembe zenye mipini iliyofunikwa kwa shaba au dhahabu. Maendeleo yaliyofanywa hivi karibuni yanatia ndani nyembe zinazoweza kutupwa kabisa, nyembe zenye bapa mbili au hata tatu, na nyembe zenye vichwa vinavyonyumbulika, na kuzunguka.

Bila shaka, hatupaswi kusahau nyembe za stima, ambazo zilitokea mara ya kwanza mwaka wa 1931. Zimekuwa na matokeo na kupendwa sana, lakini wengi bado hupendelea wembe wenye ncha kali kwa ajili ya unyoaji laini kabisa.

Ndevu Zimekuwa Kwenye Mtindo na Kutoweka Katika Historia Yote

Kutoka nyakati za mapema wanadamu wamekuwa wakiachilia ndevu na kuzinyoa katika historia yote. Wamisri wa kale, chasema kitabu Everyday Life in Ancient Egypt, “hawakuwa na malaika kwenye miili yao nao walijivunia unyoaji laini, na matumizi ya nyembe zilizotengenezwa vizuri ambazo waliziweka ndani ya vibweta nadhifu vya ngozi.” Kwa kuzingatia desturi hiyo twaweza kufahamu sababu iliyomfanya mfungwa Mwebrania Yosefu anyoe ndevu kabla ya kujihudhurisha mbele za Farao.—Mwanzo 41:14.

Waashuri walikuwa jamii ya wanaume wenye ndevu maridadi. Hata walizionea fahari huku wakizitunza sana na kuzipa uangalifu ndevu zao kwa kuzipinda, kuzisonga na kuzipanga kwa uangalifu sana.

Wanaume wa kale wa Israeli walikuwa na ndevu zenye urefu wa kadiri, na walitumia wembe ili kuzikata kwa njia nzuri. Kwa hiyo, Sheria ya Mungu ilimaanisha nini ilipowaamuru wanaume Waisraeli ‘wasinyoe denge pembe za vichwani’ au ‘kuharibu pembe za ndevu zao’? Hiyo haikuwa amri iliyokataza kupunguza nywele au ndevu. Badala yake, ilizuia wanaume Waisraeli wasiige mazoea ya kidini yanayopita kiasi ya mataifa ya kipagani waliyopakana nayo. *Mambo ya Walawi 19:27; Yeremia 9:25, 26; 25:23; 49:32.

Katika jumuiya ya kale ya Kigiriki, kwa kawaida wanaume wote walikuwa na ndevu, isipokuwa makabaila, ambao mara nyingi walinyoa kwa njia laini kabisa. Katika Roma yaelekea zoea la kunyoa lilianza katika karne ya pili K.W.K., na kwa karne kadhaa baada ya hapo, kukawa na desturi ya kunyoa kila siku.

Hata hivyo, baada ya kuanguka kwa Milki ya Roma, watu wakaanza kuachilia ndevu tena, zoea hilo liliendelea kwa miaka 1,000 hadi kufikia nusu ya pili ya karne ya 17, ambapo unyoaji ukawa ndio mtindo. Watu waliendelea kunyoa kwa njia laini kabisa katika karne yote ya 18. Lakini, ndipo kufikia katikati hadi mwishoni mwa karne ya 19, kuachilia ndevu kukawa mtindo. Ndiyo sababu, picha za C. T. Russell, msimamizi wa kwanza wa Watch Tower Society, na Mkristo mwenzake W. E. Van Amburgh huonyesha wanaume hao wawili wakiwa na ndevu za kimtindo zilizokatwa vizuri ambazo wakati huo zilionwa kuwa adhama na zenye kufaa. Hata hivyo, mapema katika karne ya 20, watu walianza kunyoa tena na wamependelea mtindo huo katika nchi nyingi hadi siku ya leo.

Je, wewe ni mmojawapo wa mamilioni ya wanaume wanaotumia wembe kunyoa kila siku kwa kutumia kioo? Ikiwa ndivyo, bila shaka unataka unyoaji usio na maumivu, bila damu, na wenye matokeo kadiri iwezekanavyo. Ili kutimiza jambo hilo, huenda ukataka kufikiria madokezo kwenye sanduku “Madokezo ya Kunyoa kwa Kutumia Wembe.” Yawezekana kwamba tayari unatumia baadhi ya madokezo hayo. Vyovyote iwavyo,—furahia unyoaji safi na laini kabisa!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 Ona kitabu Insight on the Scriptures, Buku la Kwanza, ukurasa wa 266 na 1021, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Madokezo ya Kunyoa kwa Kutumia Wembe

Kitabu cha Men’s Hair chatoa madokezo yafuatayo ya kunyoa kwa njia yenye matokeo kwa kutumia wembe. *

1. Kulainisha sharafa zako: Njia pekee ya kulainisha vizuri kabisa ndevu zako ni kwa kutumia maji moto kwa wingi. Ikiwezekana, nyoa baada ya kuoga, kwa kuwa hilo hutokeza muda zaidi ili maji yalainishe sharafa.

2. Kutumia sabuni za kunyolea: Sabuni zote za namna mbalimbali, povu, hamira, na jeli hutimiza mambo matatu ya msingi. (1) Huziba unyevu kwenye sharafa, (2) huzifanya zikae wima, na (3) hulainisha ngozi ili wembe uteleze juu yake kwa urahisi zaidi. Teua ile inayokufaa zaidi. Aha! je, umejaribu mafuta ya kulegeza nywele? Yamekusudiwa pia kulainisha nywele.

3. Kutumia wembe unaofaa kwa njia inayofaa: Wembe wenye makali ndio unaofaa. Nyembe zilizo butu zaweza kuharibu ngozi yako. Nyoa kwa kufuatisha uelekeo wa ukuzi wa nywele. Kunyoa kinyume na uelekeo wa jinsi nywele inavyokua kwaweza kutokeza unyoaji laini, lakini kwaweza kukata sharafa chini ya ngozi na kuzifanya zikue kwenye tishu zilizo karibu badala ya kukua kwenye vitundu vidogo vya ngozi. Kwa mujibu wa vichapo fulani, mazoea mabaya ya unyoaji—ya wanaume na wanawake—yanaweza kusababisha maambukizo ya virusi ambavyo hutokeza chunjua.

4. Krimu za kujipaka baada ya kunyoa za kulinda ngozi: Kila mara unaponyoa, unatoa tabaka la ngozi lisiloonekana, na kufanya ngozi yako iweze kuathiriwa kwa urahisi. Kwa hiyo, ni jambo la maana kusuuza uso wako kwa maji safi—maji moto kwanza, kisha baridi ili kuziba vitundu vidogo na kuziba unyevu. Ukipenda, unaweza kutumia losheni ya kulainisha ngozi ili kulinda na kufanya upya ngozi yako.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 20 Makala hii yazungumzia unyoaji wa wanaume. Katika nchi nyingi wanawake pia hunyoa sehemu fulani za miili yao, kwa hiyo wao vilevile waweza kunufaika na baadhi ya hoja zilizotajwa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]

Sharafa Ni Nini?

Sharafa ni nywele ambazo hukua kwenye uso. Zimefanyizwa kwa keratini na protini zinazohusiana nayo. Keratini ni protini ya nyuzinyuzi yenye salfa ambayo hutengenezwa na mwili wa binadamu na wa mnyama na ndio kitu cha msingi cha kufanyiza nywele, kucha, manyoya, kwato, na pembe. Kati ya nywele zote zilizo kwenye mwili wa binadamu, sharafa ndizo ngumu na thabiti zaidi, huwa ngumu kuzikata kama vile kukata waya ya shaba yenye unene sawa. Mwanamume wa kawaida ana sharafa zipatazo 25,000 kwenye uso wake, nazo hukua kwa kiwango cha takriban nusu milimeta kila saa 24.

[Hisani]

Wanaume: A Pictorial Archive from Nineteenth-Century Sources/

Dover Publications, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kunyoa kumekuwa kwenye mtindo na kutoweka katika historia yote

Mmisri

Mwashuri

Mroma

[Hisani]

Museo Egizio di Torino

Photographs taken by courtesy of the British Museum