Akina Mama Walio na UKIMWI Watatanika
Akina Mama Walio na UKIMWI Watatanika
CYNTHIA, * mwanamke anayeishi West Indies, alikabiliwa na suala la kumnyonyesha mtoto wake aliyetoka tu kuzaliwa ama kumnyonyesha maziwa kupitia chupa. Huenda uamuzi huo ukaonekana kuwa sahili. Hata hivyo, kwa miongo mingi wataalamu wa afya wamekuwa wakipendekeza maziwa ya mama kuwa “chakula bora zaidi” kwa watoto. Mbali na hilo, watoto wanaonyonyeshwa maziwa kwa chupa katika jumuiya zilizo maskini hupatwa na kifo karibu mara 15 zaidi kutokana na maradhi ya kuharisha kuliko wale wanaonyonyeshwa. Kwa kweli, Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa (UNICEF) yaripoti kwamba karibu watoto 4,000 hufa kila siku kwa sababu ya hatari zinazohusiana na vibadala vya maziwa ya mama.
Hata hivyo, katika kisa cha Cynthia, uamuzi kuhusu kunyonyesha ulihusu hatari nyingine kabisa. Mume wake alikuwa amemwambukiza HIV, ambavyo husababisha UKIMWI. Baada ya kuzaa, Cynthia aligundua kwamba mtoto wa mama aliye na HIV huwa katika hatari ya kuwa mmoja kati ya watoto saba anayeambukizwa kupitia maziwa ya mama. * Hivyo, alilazimika kufanya uchaguzi wenye kuhuzunisha sana: kumtia mtoto wake kwenye hatari za kunyonyesha au katika hatari zinazohusu maziwa ya chupa.
Katika sehemu kadhaa za ulimwengu ambazo kuna visa vingi sana vya UKIMWI, wanawake 2 au 3 kati ya wanawake 10 wenye mimba wana HIV. Katika nchi moja, zaidi ya nusu ya wanawake wajawazito waliopimwa walikuwa wameambukizwa. “Idadi hiyo yenye kushtua,” ikaripoti Redio ya UM, “imelazimu wanasayansi wajitahidi kutafuta dawa.” Ili kuitikia tisho hilo, mashirika sita ya UM yamechangia uzoefu wao, jitihada zao, na mali ili kuunda programu iitwayo Joint United Nations Programme inayohusu HIV/UKIMWI, ijulikanayo kuwa UNAIDS. * Lakini UNAIDS imeona kwamba utatuzi wa tatizo la UKIMWI si rahisi.
Vizuizi Vigumu Vinavyozuia Utatuzi Sahili
Kulingana na Edith White, mtaalamu wa unyonyeshaji na kuambukiza HIV kutoka kwa mama hadi kwa mtoto, wafanyakazi wa afya wanashauri wanawake walio na HIV katika nchi zilizositawi wasiwanyonyeshe watoto wao, kwa kuwa hilo huongeza maradufu hatari ya mtoto
kuambukizwa. Kutumia mchanganyiko wa lishe ya maziwa huonekana kuwa jambo la kiakili. Lakini katika nchi zinazositawi—ambapo mawazo ya kudhania tu hushindwa upesi na kuwa mambo halisi—utatuzi huu sahili huwa mgumu kuutekeleza.Mojawapo ya vizuizi ni kile cha kijamii. Katika nchi ambamo kunyonyesha ni jambo la kawaida, wanawake wanaonyonyesha watoto wao kwa chupa huenda wakawa wanajulisha kwamba wameambukizwa HIV. Huenda mwanamke akaogopa kwamba atalaumiwa, kuachwa, au hata kupigwa hali yake ijulikanapo. Wanawake fulani walio katika hali hii huhisi kwamba hawana jingine ila kunyonyesha mtoto wao ili kuendelea kuficha kwamba wameambukizwa HIV.
Pia kuna vizuizi vingine. Kwa mfano, mfikirie Margaret mwenye umri wa miaka 20. Yeye, kama vile asilimia 95 hivi ya wanawake wa Uganda wanaoishi vijijini, hajapata kupimwa kama ana HIV. Lakini Margaret ana sababu ya kuhangaika. Mtoto wake wa kwanza alikufa, na mtoto wake wa pili ni mdhaifu na mgonjwa-mgonjwa. Margaret ananyonyesha mtoto wake wa tatu mara kumi kwa siku, ijapokuwa huenda akawa na HIV. “Siwezi kamwe kumlisha mtoto wangu mchanganyiko wa lishe ya maziwa,” yeye asema. Kwa nini? Gharama ya kumlisha mtoto mmoja mchanga mchanganyiko wa lishe ya maziwa, Margaret asema, ni mara moja na nusu zaidi kuliko jumla ya mapato ya mwaka mzima ya familia moja katika kijiji chake. Hata kama mchanganyiko ungepatikana bila malipo, bado kungekuwa na tatizo la kupata maji safi ya kuutengeneza mchanganyiko huo kuwa chakula safi cha mtoto. *
Baadhi ya vizuizi hivyo vyaweza kupunguzwa ikiwa akina mama walio na maambukizo ya HIV wanaandaliwa usafi wa kutunza afya, vibadala vya kutosha vya maziwa ya mama, na maji safi. Ni ghali? Labda. Hata hivyo, kwa kushangaza, kutoa maandalizi hayo kwaonekana kuwa jambo la kuweka mambo ya kutangulizwa kuliko kutafuta fedha. Kwa kweli, shirika la UM laripoti kwamba baadhi ya nchi zilizo maskini zaidi ulimwenguni hutumia fedha maradufu kwa ajili ya wanajeshi kuliko zinavyotumia kwa ajili ya afya na elimu.
Vipi Dawa za Kuzuia UKIMWI?
Wanasayansi wa UM wameripoti kwamba dawa sahili na isiyo ghali sana iitwayo AZT yaweza kupunguza kwa njia yenye kutokeza maambukizo ya HIV kutoka kwa mama hadi kwa mtoto. Kwa msaada wa UNAIDS, gharama ya tiba hiyo imepunguzwa hadi dola 50 za Marekani. Isitoshe, wachunguzi wa UKIMWI walitangaza katika Julai 1999 kwamba kutibu akina mama walio na HIV na watoto wao waliotoka kuzaliwa kwa kutumia dawa nevirapine ya dola tatu tu kwaonekana kuwa na matokeo hata zaidi kuliko AZT katika kuzuia maambukizo ya HIV. Wataalamu wa afya wanasema kwamba nevirapine ingeweza kusaidia watoto 400,000 wanaozaliwa kwa mwaka kuanza maisha yao bila maambukizo ya HIV.
Hata hivyo, wengine huchambua tiba hizo za dawa, wakidai kwamba kwa kuwa zinaweza tu kuzuia maambukizo ya HIV kutoka kwa mama hadi kwa mtoto, hatimaye mama atashikwa na UKIMWI na kumwacha mtoto wake akiwa yatima. Shirika la UM latoa sababu kwamba uchaguzi mwingine wenye kuhuzunisha ni kuacha watoto waambukizwe HIV, hivyo kuwaacha wahasiriwa hao wasio na hatia kufa polepole kwa huzuni. Pia wanadai kwamba akina mama walioambukizwa HIV waweza kuishi kwa miaka mingi. Mfikirie Cynthia, aliyetajwa mapema. Aligundua kwamba alikuwa na HIV mwaka 1985 mtoto wake alipozaliwa lakini hakuwa mgonjwa mpaka ilipotimia miaka minane baadaye. Na hata ingawa mtoto wake alikuwa na HIV alipozaliwa, alipofikia umri wa miaka miwili hakuwa na maambukizo hayo tena.
Uhakikisho wa Biblia wenye kufariji ni kwamba mazingira yenye usalama kikweli na utatuzi wenye kudumu wa mapigo ya ugonjwa kama vile UKIMWI uko karibu. (Ufunuo 21:1-4) Yehova Mungu anaahidi ulimwengu mpya ambamo “hakuna mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24) Mashahidi wa Yehova wangependa kukuambia juu ya utatuzi huo wenye kudumu. Ili upate habari zaidi, tafadhali wasiliana na wachapishaji wa gazeti hili au Mashahidi wa Yehova katika jumuiya yako.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 2 Si jina lake halisi.
^ fu. 3 Kulingana na UNICEF, karibu vitoto vichanga 500 hadi 700 kwa siku wanaambukizwa na maziwa ya mama zao walio na HIV.
^ fu. 4 Mashirika hayo sita ni UNICEF, Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo, Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa, Shirika la Afya Ulimwenguni, Benki ya Dunia, na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni. Shirika la UNAIDS lilianzishwa mwaka wa 1995.
^ fu. 8 Uchunguzi wa karibuni wadokeza kwamba mchanganyiko wa lishe ya maziwa na unyonyeshaji huenda ukaongeza hatari ya maambukizo ya HIV na kwamba maziwa ya mama huenda yakawa na vizuia-virusi ambavyo husaidia kuzimua virusi. Ikiwa ni kweli, kunyonyesha peke yake—hata kukiwa na hatari zake—kwaweza kuwa chaguo salama zaidi. Hata hivyo, utafiti wa uchunguzi huo haujathibitishwa bado.
[Picha katika ukurasa wa 20]
WHO/E. Hooper