JE, NI KAZI YA UBUNI?
Uwezo wa Chembe Kubadilikana
Mimba yako ilipotungwa tumboni mwa mama yako, ulikuwa chembe moja ndogo inayoitwa zygote. Yai hilo ni dogo sana hivi kwamba unahitaji hadubini ili kuliona. Ajabu ni kwamba, miezi kadhaa baadaye ulizaliwa ukiwa mtoto. Kwa kuwa chembe hiyo moja iligawanyika na kufanyiza chembe zaidi ya 200 tofauti zilizo na umbo, ukubwa, na kazi tofauti.
Fikiria hili: Zygote inajigawanya katika chembe mbili tofauti na zote huwa na DNA ileile. Kisha chembe hizo mbili huendelea kujigawanya mara nyingi sana. Mwanzoni, chembe zinazofanyizwa hufanana kabisa. Zina DNA iliyobeba maagizo yote yanayohusu kila aina ya chembe.
Juma moja baada ya mimba kutungwa, kunakuwa na aina mbili za chembe. Moja inayofanyiza kiinitete na aina nyingine inayofanyiza kondo la nyuma pamoja na tishu nyingine zitakazosaidia kiinitete kukua.
Kufikia juma la tatu, chembe kwenye kiinitete hujipanga katika safu tatu. Chembe za safu ya juu huja kuwa neva, ubongo, mdomo, ngozi ya mwili, na chembe nyinginezo. Chembe za safu ya kati zitakuwa damu, mifupa, figo, misuli, na tishu nyinginezo. Chembe za safu ya ndani zitakuwa viungo vilivyo ndani ya mwili kama vile mapafu, kibofu, na pia zitafanyiza sehemu kubwa ya mfumo wa kumeng’enya chakula.
Katika kipindi chote kilichobaki, baadhi ya chembe hizo huhama—zinaweza kuhama katika makundi au mojamoja kutoka sehemu moja ya kiinitete hadi sehemu nyingine. Chembe nyingine hujikusanya na kufanyiza bamba au kufunika zile chembe za msingi au uwazi wowote. Hilo linaonyesha jinsi chembe hizo hushirikiana kwa ukaribu sana. Kwa mfano, kuna pindi ambapo bamba la chembe hujikunja na kuwa kama mrija. Hilo hutokea kwenye sehemu mbalimbali katika kiinitete. Kisha mirija hiyo huongezeka na kutokeza mirija mingine ambayo, kwa ujumla, hufanyiza mzunguko wa mirija inayozungusha damu mwilini.
Kufikia wakati ambapo mtoto mwenye afya anazaliwa, ana mabilioni ya chembe za aina nyingi sana zinazofanya kazi hususa, katika sehemu hususa, na kwa wakati hususa.
Una maoni gani? Je, uwezo wa chembe wa kubadilikana ulijitokeza wenyewe? Au, ulibuniwa?