MACHI 30, 2016
URUSI
Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Yaripoti Kwamba Urusi Imeweka Sheria Inayowalenga Hasa Mashahidi wa Yehova ya Kupinga Shughuli Zenye Msimamo Mkali
ST. PETERSBURG, Urusi—Kufikia mwaka 2016, miaka 125 ilikuwa imepita tangu utawala wa kimaliki wa czar ulipomfukuza Semyon Kozlitskiy, mmoja kati ya Mashahidi wa Yehova wa kwanza nchini Urusi, kwa kosa la kuhubiri ujumbe wa Biblia. Mwaka 1891, Bw. Kozlitskiy alifungwa mnyororo wa chuma na kuhamishiwa Siberia, ambapo aliishi hadi alipokufa mwaka 1935.
Katika kipindi chote cha karne ya Ishirini, Urusi imeendelea kuwa na maoni yaleyale kuwahusu Mashahidi wa Yehova. Kama ripoti ya hivi karibuni ya Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilivyosema, vyanzo mbalimbali vinaonyesha kwamba bado Urusi inaendelea “kunyima watu uhuru wa kusema, . . na uhuru wa kidini, ikiwalenga hasa Mashahidi wa Yehova.”
Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ina haki ya kisheria ya kufuatilia ikiwa nchi zilizo katika muungano wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), zinatenda kulingana na mkataba huo, na Urusi ni moja ya nchi zinazoshiriki katika muungano huo. Heiner Bielefeldt, Katibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa wa kutetea uhuru wa kidini au imani, anasema: “Waandishi wa ICCPR wanatambua kwamba jambo muhimu zaidi kuhusu uhuru wa kidini au wa imani, kimsingi ni kwamba, unapaswa kuwa uhuru ambao haupaswi kupuuzwa [hauwezi kunyang’anywa au kubadilishwa] hata ikiwa kuna dharura (Kifungu cha 4.2). Uhuru wa aina hiyo ni uhuru ambao unazingatiwa hata katika vipengele vingine vya haki za kibinadamu.” Katika mkutano wake wa 113 (ona picha iliyo hapo juu), Kamati hiyo ilitoa ripoti yake mpya inayohusu Muungano wa Urusi, na ikasema kwamba ingawa Urusi inaonekana kama inalinda uhuru wa kidini kwa kuwa ina sehemu katika ICCPR, lakini mahakama zote za Urusi zinajitungia sheria ya kulenga Mashahidi, na kuwahukumu kama watu wenye msimamo mkali.
Sheria ya Serikali ya Urusi ya “Kupambana na Watu Wenye Msimamo Mkali” (Na. 114-FZ), ilianzishwa mwaka 2002, kwa sehemu fulani, kusudi lao lilikuwa ni kupinga ugaidi. Hata hivyo, walirekebisha sheria hiyo mwaka 2006, 2007, na 2008 ili itie ndani “mambo mengi zaidi ya hofu inayosababishwa na shughuli zenye msimamo mkali zinazohusisha ugaidi,” kama ilivyotajwa na makala moja yenye kichwa, “Sheria za Urusi Zinazohusu Msimamo Mkali Zakiuka Haki za Kibinadamu” iliyochapishwa kwenye gazeti la The Moscow Times. Derek H. Davis, aliyekuwa mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Baylor, Taasisi ya J.M. Dawson ya Mafunzo ya Kanisa na Serikali anasema kwamba sasa, “neno ‘ugaidi,’ ambalo limekuwa neno la kawaida kwa mataifa yote tangu Septemba 11, 2001, baada ya majengo ya Twin Towers huko New York kulipuliwa, limetumiwa na sheria ya Urusi kufafanua vikundi vya kidini ambavyo havipendwi nchini humo. Hivyo kuwaita Mashahidi wa Yehova ‘watu wenye msimamo mkali’ hakulingani na kusudi la neno hilo na ni jambo linaloenda kinyume na haki.”
Kamati ya Haki za Kibinadamu inatambua kwamba chanzo cha tatizo ni sheria ambayo haitaji moja kwa moja maana ya shughuli zenye msimamo mkali. Geraldine Fagan, mwandishi wa kitabu Believing in Russia—Religious Policy After Communism, alipokuwa akizungumza na gazeti la The Washington Post, alielezea kwamba sheria hiyo ambayo haitaji mambo kihususa inafanya iwe rahisi kwa mahakama zilizo katika maeneo mbalimbali “kutumia baadhi ya wale wanaoitwa wataalamu ambao kihalisi hawawapendi Mashahidi wa Yehova, na kuwafanya waandike ripoti zinazoonyesha kwamba machapisho ya Mashahidi wa Yehova yana msimamo mkali.”
Hilo ndio jambo lililotokea mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo mtaalamu wa lugha alitoa ushahidi ambao ulifanya hakimu wa Mahakama ya Jiji la Vyborg atangaze kuwa magazeti mawili ya Mashahidi ni yenye msimamo mkali. Mwendesha-mashtaka huyohuyo alifungua mashtaka dhidi ya Biblia ya Tafsiri ya Ulimwengu Mpya iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova akidai kwamba ina msimamo mkali. Kesi hiyo ikaanza kusikilizwa Machi 15, 2016.
Matatizo ya kisheria yaliyowakabili Mashahidi mwaka 2016 yalianza na matukio yanayoshtua mwaka 2015. Roman Lunkin, mkuu wa Kituo cha Dini na Jamii katika Taasisi ya Ulaya, Chuo cha Sayansi cha Moscow, anasema kwamba, “mwaka 2015, mnyanyaso huo uliongezeka zaidi na kukua kwa kasi.” Mwezi Machi, wenye mamlaka nchini Urusi walikataza machapisho yoyote ya Mashahidi kuingizwa nchini, hata machapisho ambayo awali yalichunguzwa na mahakama za Urusi na kuonwa kuwa hayana viashiria vyovyote vya kuwa na msimamo mkali. Julai, wenye mamlaka walianza kuzuia Biblia za Kirusi zilizochapishwa na Mashahidi zisiingizwe nchini. Katika mwezi huohuo, Muungano wa Urusi ikawa nchi pekee duniani kupiga marufuku tovuti rasmi ya Mashahidi, jw.org. Mwezi Novemba Mashahidi wa Yehova walinyimwa kuingiza nchini, Biblia za Kirusi tafsiri ya Sinodi inayotumika kwa ukawaida na Wakristo nchini Urusi hata kutia ndani Kanisa Othodoksi la Urusi. Mwishoni mwa mwaka huo kulikuwa na tukio ambalo gazeti la The Washington Post liliita “mojawapo ya kesi kubwa zaidi ya kupinga watu wenye msimamo mkali katika miaka ya hivi karibuni,” hakimu wa jiji la Taganrog alihukumu Mashahidi 16 kwa kosa la kihalifu la kupanga na kuhudhuria mikutano hiyo ya kidini iliyofanywa kwa amani.
Katika kesi hiyo iliyosikilizwa Taganrog, na pia katika kesi nyingine kama hizo, kulikuwa na uwongo mwingi. Bw. Lunkin alisema kwamba “Kuna Mashahidi wa Yehova wa muda mrefu wanaoendelea kunyanyaswa ambao tayari wana vyeti wanavyopewa watu waliovumilia ukandamizaji.” Wakati wa utawala wa Muungano wa Sovieti, maelfu ya Mashahidi wa Yehova walifungwa. Na mwaka 1990, Shahidi wa mwisho akaachiliwa huru. Heshima ya ndugu hawa walioachiliwa huru ilirudishwa, kila mmoja wao akapokea Cheti cha Kuondolewa Lawama kilichosema kwamba “hawakuwa maadui wa taifa” bali ni watu waliokandamizwa tu. Hivyo Bw. Lunkin akasema, “Wenye mamlaka nchini Urusi wameamua kukiuka makubaliano hayo kwa kutumia sheria inayowafanya waonekana kama watu wenye msimamo mkali.
Hata hivyo, Mei 27, 2015, Mashahidi wa Yehova nchini Urusi walishinda kesi ya kipekee, Wizara ya Sheria ya Shirikisho la Urusi ilirudisha usajili wa shirika la Mashahidi wa Yehova kama shirika la kidini jijini Moscow. Hii ni baada ya Mashahidi kupoteza utambulisho huo wa kisheria Machi 26, 2004. Juni 10, 2010, Mashahidi wa Yehova walikata rufaa katika Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR), na nchi ya Urusi ikapewa amri ya kuwarudishia usajili wao, na hata walipaswa kulipa fidia kwa sababu ya kuwaharibia sifa na walipaswa kulipia gharama za kesi.
Katibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa anasema hivi: “Ninakubaliana na uamuzi wa ECHR. Kuwanyima Mashahidi wa Yehova haki yao ya kutenda kulingana na dini yao ni jambo ‘linalopita mipaka’ na ‘lisilo na usawaziko,’ linalokiuka haki zao za kidini.” Kulingana na uamuzi wa ECHR, serikali ya Urusi iliwalipa Mashahidi faini lakini hawakurudishiwa majengo yao kisheria mpaka Mei 2015, miaka mitano baada ya uamuzi wa ECHR utolewe.
Yaroslav Sivulskiy, msemaji wa Mashahidi wa Yehova nchini Urusi anasema: “Zaidi ya Mashahidi 9,600 wanaishi jijini Moscow, na kuna Mashahidi 175,000 hivi wanaoishi nchini. Mashahidi wote; nchini Urusi na undugu wetu wa ulimwenguni pote wenye zaidi ya waabudu milioni 8, wanatarajia kwamba usajili huo uliotoka mji mkuu wa Urusi ni mwanzo wa kupata uhuru wa kidini katika muungano wote.” Hata hivyo, wataalamu kama Bw. Davis wanasema kwamba tendo hilo la kurudisha utambulisho wa Shirika la Mashahidi wa Yehova kama shirika la kidini linalotambuliwa kisheria, “ingawa ni muhimu kwa shirika hilo kuonekana kama linatenda kulingana na uhuru wao wa kidini, tendo hilo linapaswa kuonwa kama mbinu ya kisiasa tu lililokusudiwa kufurahisha mataifa mengine ulimwenguni.”
Mwaka 2015, Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilitamka tena mapendekezo iliyotoa mwaka 2003 na mwaka 2009, kwamba Urusi inapaswa “kupitia upya Sheria ya Serikali yake ya Kupambana na Watu Wenye Msimamo Mkali bila kukawia,” pia ilielezea kwa undani maana ya maneno “shughuli zenye msimamo mkali,” yanayorejelea shughuli zinazofanywa kwa ukatili na zinazochochewa na chuki, na wakatoa mifano ya jinsi habari mbalimbali zinavyoweza kuonwa kuwa zenye msimamo mkali. Kwa kuongezea, kamati hiyo imesihi nchi ya Urusi “ichukue hatua zote zinazohitajika ili kuepuka matumizi mabaya ya sheria na ipitie upya Orodha ya Serikali ya Vitabu na Habari Zinazowachochea Watu Kuwa na Msimamo Mkali.”
“Bw. Lunkin anasema hivi: “Ni wazi kwamba ubaguzi dhidi ya Mashahidi wa Yehova ni ubaguzi wa kidini, kwa kuwa wakati huo-huo dini nyingine zinaweza kufanya shughuli zinazofanywa na Mashahidi wa Yehova bila kuadhibiwa. Licha ya madai yote ya kisheria dhidi ya Mashahidi wa Yehova ambayo mara nyingi huongezewa chumvi na vyombo vya habari ambavyo haviwapendi, Bw Lunkin anaendelea kusema: “Bado Mashahidi wa Yehova wanabaki kuwa tengenezo lililoenea nchini pote na linaloendelea kukua.”
Wanahabari Wanaweza Kuwasiliana na:
David A. Semonian, Ofisi ya Habari za Umma, ++1 718 560 5000
Urusi: Yaroslav Sivulskiy, +7-812-702-2691