NOVEMBA 14, 2024
MAREKANI
Moto Mkubwa wa Msituni Karibu na Makao Makuu ya Mashahidi wa Yehova, New York, Marekani
Novemba 9, 2024, moto wa msituni ulianza kilomita mbili hivi kaskazini-magharibi mwa Makao Makuu ya Mashahidi wa Yehova huko Warwick, New York, Marekani. Moto huo uliokuwa unasambaa taratibu tayari ulikuwa umeteketeza zaidi ya ekari 5000 za msitu. Maofisa wa serikali katika eneo hilo wanasema kwamba huenda moto huo ukaendelea mpaka mvua zitakaponyesha.
Kwa sasa majengo mbalimbali ya Betheli katika eneo hilo kutia ndani majengo ya Warwick, eneo la ujenzi la Ramapo, na studio zilizopo Tuxedo Park hazikabili hatari yoyote. Hata hivyo, ndugu zetu wako macho na wanachukua tahadhari ili kuilinda familia ya Betheli pamoja na majengo. (Methali 22:3) Ndugu Luke Saladino, mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Marekani, anasema hivi: “Baada ya moto huo kuanza, tuliwapa baadhi ya akina ndugu mgawo wa kufuatilia jinsi moto unavyoendelea saa 24. Wafanyakazi wa Idara ya Huduma ya Dharura walipewa mgawo wa kuondoa majani yaliyokauka karibu na majengo, kumwagilia maji mimea iliyo kwenye paa, na kuchukua tahadhari nyingine zinazohitajika. Pia, tuliwatia moyo Wanabetheli wa Warwick kuandaa mikoba yao ya dharura na kuwa tayari kukimbia ikihitajika. Hata hivyo, tunashukuru kwamba kufikia sasa hatujalazimika kuondoka.”
Wazimamoto na vikosi vya dharura kutoka kwenye maeneo ya karibu wanafanya kazi usiku na mchana ili kudhibiti moto huo. Ili kuonyesha uthamini wetu, idara mbalimbali za Betheli zinashirikiana ili kuwaandalia wazimamoto chakula, maji ya kunywa, na vifaa vingine. Ndugu Saladino aliongezea hivi: “Tunawashukuru wanaume na wanawake hawa wanaofanya kazi hii ngumu kwa ajili yetu na majirani wetu chini ya hali hizi hatari.”
Tunasali Yehova awapatie “hekima inayotumika na uwezo wa kufikiri” wote ambao wameathiriwa na moto huo.—Methali 3:21.