APRILI 17, 2020
FIJI
Kimbunga Harold cha Kitropiki Chapiga Visiwa vya Vanuatu
Aprili 5, 2020, Kimbunga Harold cha Kitropiki kilipiga visiwa vya kaskazini vya Vanuatu na kusababisha madhara makubwa. Aprili 8, kimbunga hicho kilipiga pia maeneo ya kusini mashariki na kusini magharibi mwa visiwa vya Fiji na kusababisha madhara makubwa vilevile. Kulingana na ripoti za awali, hakuna yeyote kati ya ndugu zetu ambaye amejeruhiwa au kufa.
Wahubiri 280 hivi wanaishi Espiritu Santo, kisiwa kikubwa zaidi na kilicho upande wa kaskazini zaidi cha Vanuatu. Majengo na mimea katika kisiwa hicho na visiwa vingine vya karibu iliharibiwa kwa kadiri kubwa sana. Nchini Fiji, nyumba za wahubiri 260 hivi ziliharibiwa sana. Kuna upungufu mkubwa wa maji, umeme, na chakula.
Ofisi ya tawi ya Fiji inapanga kugawanywa kwa misaada. Wazee wa maeneo hayo wanawafanyia ziara za uchungaji ndugu na dada walioathiriwa. Tunafurahi kwamba ndugu zetu walioathiriwa na kimbunga hicho wanatunzwa kimwili na kiroho.—Methali 17:17.