Hamia kwenye habari

FEBRUARI 15, 2023
ARGENTINA

Mahubiri ya Hadharani Kwenye Sherehe ya Kitamaduni Argentina

Mahubiri ya Hadharani Kwenye Sherehe ya Kitamaduni Argentina

Kuanzia Novemba 11 hadi 21, 2022, Sherehe ya 38 ya National Festival of Immigrant Communities ilifanywa jijini Rosario, Argentina. Sherehe hiyo hufanywa mara moja kila mwaka. Zaidi ya watu milioni moja walihudhuria sherehe hiyo ambayo inaonyesha utamaduni na desturi za watu wa mataifa na jamii mbalimbali wanaoishi nchini humo. Ofisi ya tawi ya Argentina ilifanya mipango kwa ajili ya kampeni ya pekee ya mahubiri ya hadharani ambapo ndugu na dada waliwaonyesha watu tovuti ya jw.org na kutoa machapisho. Machapisho yalipatikana katika Lugha ya Ishara ya Argentina, Kichina, Kiingereza, Kiguarani, Kikrioli cha Haiti, Kireno, Kikwechua cha Bolivia, na Kihispania. Zaidi ya ndugu na dada 400 walishiriki katika kampeni hiyo.

Wasimamizi wa sherehe hiyo waliwaruhusu ndugu zetu kuweka vigari vya machapisho katika sehemu ambazo watu wengi wangeweza kuviona. Ofisa mmoja wa jiji alisema: “Kila mmoja wenu ni nadhifu na mwenendo wenu ni mzuri.” Mwanasaikolojia mmoja kutoka jiji la Rosario alikaribia kigari na kusema: “Ninayasoma sana machapisho yenu, na ninayapenda! Mara nyingi ninayatumia kuwasaidia wagonjwa wangu.”

Novemba 14, 2022, gazeti linalosomwa zaidi jijini Rosario, yaani, La Capital, liliandika makala kuhusu kampeni hiyo ya kuhubiri. Makala hiyo ilikuwa na kiunganishi cha jw.org na ilitaja pia kuhusu idadi ya lugha zinazopatikana kwenye tovuti yetu.

Tunashangilia tunapowaona ndugu na dada zetu katika sehemu mbalimbali za dunia wakitumia kila fursa “kutoa ushahidi kamili kuhusu habari njema.”​—Matendo 20:24.