JANUARI 5, 2024
AFRIKA KUSINI
Miaka 50 Iliyopita Kulikuwa na “Ushindi wa Kimungu” Dhidi ya Ubaguzi wa Rangi Afrika Kusini
Jumapili Januari 6, 1974, kusanyiko la kihistoria la Mashahidi wa Yehova lilifanywa nchini Afrika Kusini. Watu 33,408, waliokuwa na rangi mbalimbali, walikusanyika kwenye Uwanja wa Rand ulioko Johannesburg kwa ajili ya kipindi cha mwisho cha Kusanyiko la Kimataifa la “Ushindi wa Kimungu.” Mwaka huu, miaka 50 imetimia tangu tukio hilo la pekee lilipotokea.
Sheria za ubaguzi wa rangi ziliwekwa Afrika Kusini mwanzoni mwa mwaka 1948. Hilo liliathiri jinsi mikutano na makusanyiko ya Mashahidi wa Yehova ilivyofanywa. Mwaka wa 1974, Ndugu Alfred Phatswana, ambaye sasa ni mshiriki wa Halmashauri ya Tawi ya Afrika Kusini alikuwa na umri wa miaka kumi. Naye alisema hivi: “Katika kipindi cha utawala wa serikali iliyoweka sera ya ubaguzi wa rangi, halikuwa jambo la kawaida kuona watu wa rangi mbalimbali wakikutanika pamoja.”
Kusanyiko hilo la kimataifa lilifanywa Januari 2 hadi Januari 6, 1974. Kwa sababu ya sheria zilizokuwepo za kutenganisha watu kulingana na rangi zao, haikuwezekana kufanya kusanyiko lenye watu wa rangi mbalimbali katika sehemu moja kuanzia mwanzo hadi mwisho. Basi, kwa siku nne na nusu za kwanza kulikuwa na mpango mwingine ambapo wajumbe walikutanika katika vikundi vidogo katika sehemu tofauti-tofauti kulingana na rangi na lugha zao. Hata hivyo, ruhusa ilipatikana ili wajumbe wote waungane pamoja kwa ajili ya kipindi cha mwisho cha Jumapili alasiri kwenye Uwanja wa Rand. Uwanja huo ndio sehemu pekee jijini Johannesburg ambapo mikusanyiko ya watu wa rangi zote iliruhusiwa.
Jumapili kuanzia saa sita mchana, wajumbe walianza kumiminika kwenye Uwanja wa Rand. Walikuja kwa basi, gari, au treni. Mipango ilifanywa ili programu itolewe kwa Kiingereza na wakalimani walitafsiri katika Kiafrikana, Kireno, Kisesotho, na Kizulu.
Uwanja huo ulijaa upesi na wengine walilazimika kusimama. Ndugu Keith Wiggill ambaye pia ni mshiriki wa Halmashauri ya Afrika Kusini, alikuwa na umri wa miaka 23 wakati huo. Anasema: “Lilikuwa jambo lenye kustaajabisha na wengi walikuwa wamemwomba Mungu nafasi kama hiyo itokee ili tuabudu kwa pamoja. Tulikuwa na imani moja, tuliamini kanuni zilezile, na kwa muda huo mfupi tu hatukutenganishwa na sheria za kibaguzi. Nilihisi nina umoja wa kweli na ndugu na dada zangu.”
Katika Kusanyiko la Kimataifa la “Ushindi wa Kimungu” la 1974, kulikuwa na wahubiri 25,000 Afrika Kusini. Leo, kuna ndugu za dada karibu 100,000 wanaomwabudu Yehova kwa umoja nchini kote. Tangu 1974, kumekuwa na makusanyiko mengine ya kimataifa nchini Afrika Kusini. La karibuni zaidi lilikuwa Kusanyiko la Kimataifa la “Upendo Haushindwi Kamwe”! la 2019 ambapo watu 60,000 kutoka tamaduni na lugha mbalimbali walihudhuria.
Tunapata shangwe kubwa tunapokumbuka mambo yenye kustaajabisha yaliyotokea katika kusanyiko hilo la kihistoria la mwaka wa 1974. Yehova aliwasaidia waabudu wake kushinda migawanyiko iliyosababishwa na ubaguzi wa rangi na pia matabaka ya kijamii. Tunashangilia kuwa sehemu ya undugu wenye umoja wa ulimwenguni pote ambao unamletea sifa Mungu wetu ambaye hana ubaguzi, Yehova.—Matendo 10:34, 35.