JUNI 11, 2014
Uturuki
ECHR Yawaunga Mkono Watu Wanne Waliokataa Utumishi wa Kijeshi Nchini Uturuki
Juni 3, 2014, mahakimu wote wa Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu (ECHR) walifikia uamuzi ambao haukupingwa kwamba Uturuki ilivunja Mkataba wa Ulaya a ilipowashtaki Mashahidi wanne wa Yehova nchini Uturuki kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Çağlar Buldu, Bariş Görmez, Ersin Ölgün, na Nevzat Umdu, walikataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya imani yao thabiti ya kidini. Uamuzi wa Mahakama ya ECHR ulisema hivi: “Kulingana na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya, hatua zilizochukuliwa dhidi ya washtakiwa . . . ni kuingilia kwa njia isiyofaa haki za watu katika jamii ya kidemokrasia.”
Machi 17, 2008, Mashahidi hao wanne waliwasilisha kesi yao kwenye Mahakama hiyo (Buldu na Wenzake dhidi ya Uturuki) dhidi ya serikali ya Uturuki, wakilalamika kwamba serikali ya Uturuki ilikataa kutambua uhuru wao wa kidini ilipowashtaki tena na tena na kuwahukumu kwa kukataa utumishi wa kijeshi. Kwa ujumla, waliwalazimisha kufanya utumishi wa kijeshi zaidi ya mara 30 na kuwafunga gerezani na katika kambi za kijeshi kwa zaidi ya miaka sita.
Mahakama ya ECHR ilisema hivi: “Mashahidi hao wa Yehova walikataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri, ambayo inategemea hasa imani zao za kidini. Mahakama haina shaka kwamba mara mbalimbali ambazo wamekuhukumiwa, . . . na pia uwezekano wa kwamba wataendelea kushtakiwa kuwa wahalifu, . . . ni kuingilia haki yao ya uhuru wa ibada inayohakikishwa na Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya.”
Hii ni mara ya tatu kwa Mahakama ya ECHR kutoa uamuzi dhidi ya serikali ya Uturuki kuhusiana na suala la kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Mara ya kwanza ilimtetea Yunus Erçep katika mwaka wa 2011 kisha katika mwaka wa 2012 ikamtetea Feti Demirtaş. Katika kisa kingine, mnamo 2012, Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa iliwatetea Mashahidi wengine wawili nchini Uturuki, Cenk Atasoy na Arda Sarkut, ambao pia walikataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri.
Huko Ulaya, uamuzi muhimu kuhusiana na suala hilo ulifanywa Julai 7, 2011, Baraza Kuu la Mahakama ya ECHR lilipotangaza uamuzi wake katika kesi ya Bayatyan dhidi ya Armenia. Kwa mara ya kwanza, Mahakama ya ECHR ilibaini kwamba Kifungu cha 9 cha Mkataba wa Ulaya kinawalinda wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri. Nchi zote zilizo wanachama wa Baraza la Ulaya zinapaswa kushikamana na uamuzi huo. Uamuzi kuhusu kesi ya Bayatyan, zile kesi tatu zilizoamuliwa dhidi ya Uturuki, na maamuzi mengine kama hayo yaliyotolewa na Mahakama ya ECHR yanaishurutisha Uturuki na nchi nyingine zinazofanyiza Baraza la Ulaya kuchunguza upya jinsi zinavyowatendea watu wanaokataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri na kurekebisha sheria zao ili zipatane na Mkataba wa Ulaya.
James E. Andrik, mmoja wa mawakili wa washtakiwa hao wanne katika kesi hiyo alisema hivi: “Ingawa kwa sasa hakuna Mashahidi walio gerezani kwa kukataa utumishi wa kijeshi kwa sababu ya dhamiri nchini Uturuki, serikali inaendelea kuwashtaki vijana Mashahidi wanaokataa utumishi huo. Tunatumaini kwamba uamuzi wa hivi karibuni wa kesi ya Buldu na Wengine dhidi ya Uturuki utaishinikiza serikali ya Uturuki kuheshimu haki ya msingi ya uhuru wa dhamiri.”
a Kifungu cha 3, ni sheria dhidi ya kuwatesa wanadamu na kuwatendea kinyama au kuwashushia heshima; Kifungu cha 6, haki ya kusikilizwa bila ubaguzi; Kifungu cha 9, uhuru wa kufikiri, wa dhamiri na wa kidini.