Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kombe Ni Chakula cha Visiwani

Kombe Ni Chakula cha Visiwani

Kombe Ni Chakula cha Visiwani

Na mwandishi wa Amkeni! katika Visiwa vya Bahamas

“Niletee kombe wanne!” “Niletee kombe mmoja aliyechomwa na saladi mbili za kombe!”

Hivyo ndivyo watu huagiza chakula katika mikahawa huku Bahamas. Harufu nzuri ya kombe waliochomwa inayotanda katika hewa yenye chumvi, huamsha hamu. Lakini kombe ni nini?

KOMBE ni konokono wa baharini aliye na gamba moja, naye ni wa jamii ya moluska. Kuna aina nyingi za kombe kama vile hawk-wing, milk, rooster-tail, fighting, na kombe anayeitwa queen, au pink. Kombe anayependwa zaidi katika eneo hili ni queen. Katika Kilatini anaitwa Strombus gigas naye hupatikana hasa katika maji yenye joto kuanzia Florida hadi Brazili.

Kombe anayeitwa queen ana gamba kubwa lililopindika-pindika lenye ukingo mpana. Kombe wa queen waliokomaa wanaweza kuwa na urefu wa sentimeta 20 hadi 25.

Jinsi Kombe Wanavyovuliwa na Kutumiwa

Basil, anakumbuka walivyosafiri kwa mashua pamoja na baba yake ili kuvua kombe. “Baba yangu alitumia ndoo fulani ambayo ilikuwa imefanyizwa kwa glasi kwenye upande wake wa chini huku akiwa na ufito mrefu wenye ndoano mbili kwenye ncha yake. Baba alikuwa akitumbukiza ndoo hiyo yenye glasi ili atazame ndani ya bahari na kuwatafuta kombe. Alishika ndoo kwa mkono mmoja, huku akitumia mkono ule mwingine kuwanasa kombe kwa ufito na kuwavuta kwenye mashua.”

Watu wengi leo huwavua kombe kwa kupiga mbizi baharini na kuwakamata kwa mikono. Mvuvi anapopiga mbizi katika maji yenye kina kirefu anaweza kutumia mrija wa kuingiza hewa ili kuvua kombe, au ikiwa ana kibali cha serikali anaweza kutumia kifaa kikubwa cha kuingiza hewa kilichounganishwa na mashua.

Ili kumtoa kombe katika gamba lake shimo hutobolewa chini ya gamba. Kisha kisu huingizwa ndani ya shimo ili kumsukuma nje ya gamba. Mwili wa kombe una sehemu nne kuu: kichwa, viungo vya ndani, utando wa mwili, na mguu. Mguu wake una sehemu ya kahawia iliyo kama bamba. Mguu huo ambao umefunikwa kwa ngozi ngumu ndiyo sehemu inayoliwa. Ngozi na sehemu zisizoliwa huondolewa na kuacha nyama tamu nyeupe.

Kombe wana protini nyingi. Inasemekana kwamba kombe wanaweza kutumiwa kutibu magonjwa fulani. Watu wengi husema kwamba afya yao iliboreka sana baada ya kula kombe kwa ukawaida.

Leo biashara ya kutengeneza vito kutokana na magamba ya kombe imesitawi sana. Gamba la kombe lililo na ukingo wa rangi ya waridi ni maridadi na linapendwa sana na watu wanaokusanya magamba. Hata hivyo, kombe hutumiwa hasa kama chakula. Kwa muda mrefu wapishi wamegundua njia mbalimbali zenye kupendeza za kupika nyama ya kombe.

Chakula Kitamu

Kabla watu hawajaanza kutumia friji huku, kombe walikaushwa ili kuhifadhiwa. Kwanza nyama yao ilipigwapigwa kwa nyundo ili iwe nyororo. Kisha ilianikwa kwenye jua kwa siku kadhaa ili ikauke. Kabla haijapikwa nyama hiyo ililoweshwa ndani ya maji kwa saa kadhaa ili ilainike. Bado watu wengi wanafurahia nyama ya kombe iliyohifadhiwa kwa njia hiyo.

Wenyeji na wageni hupenda saladi iliyotengenezwa kwa kombe. Amini usiamini, nyama ya kombe huliwa ikiwa mbichi. Baada ya kuondolewa kwenye gamba, nyama ya kombe hukatwakatwa katika vipande vidogo na kuchanganywa na figili, pilipili, vitunguu, na nyanya. Kisha chumvi, maji ya limau na ya machungwa huongezwa. Ikiwa hupendi kula vyakula vibichi vya baharini, unaweza kumpika kombe. Kuna njia nyingi za kumpika. Hata hivyo, kuna tahadhari. Ukitaka kupika nyama ya kombe, kwanza ipigepige kwa nyundo ili iwe nyororo. Usipofanya hivyo itakuwa ngumu.

Unaweza kufurahia kula nyama ya kombe ikiwa imechemshwa, imetayarishwa katika mchuzi, imechomwa, imekaushwa, ikiwa imepikwa pamoja na wali au kwa njia nyingine yoyote. Mchuzi na kaimati za kombe huandaliwa ili kuamsha hamu ya walaji. Njia za kutayarisha nyama ya kombe zimepitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Hivyo, ukitembelea visiwa maridadi vya Bahamas, usikose kula kombe. Utafurahia sana chakula hicho kitamu cha visiwani.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 23]

Kumpika Kombe (Ona picha iliyo chini)

Sandra, ambaye ni mama na mke, anaeleza jinsi yeye hutayarisha mlo mtamu wa kombe aliyepasuliwa: “Kwanza lainisha kabisa nyama ya kombe. Kisha ipake unga uliokolezwa kwa chumvi na pilipili, halafu uichovye ndani ya mayai yaliyokorogwa. Ikaange katika mafuta moto hadi iwe na rangi ya kahawia. Tumia karatasi ili kuondoa mafuta, kisha uinyunyizie maji ya limau.”

Kwa kawaida kombe aliyetayarishwa kwa njia hii huliwa kwa chipsi na mchuzi wa nyanya au njegere na wali. Pia anaweza kuliwa kwa malai ya mayonesi na vitunguu. Mara nyingi nyama iliyogandishwa huuzwa katika nchi nyingine na hivyo unaweza kuipata nchini kwenu. Ukipenda unaweza kuionja. Huenda ukaifurahia.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kushoto hadi kulia: gamba la kombe anayeitwa “queen”; mvuvi akivua kombe kwa kutumia ndoo yenye glasi upande wa chini na ufito; kumtoa kombe; mchuzi wa kombe; saladi ya kombe; kaimati za kombe; mlo wa kombe aliyechomwa, ndizi, na mhogo