Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Watu Wanaoota Jua Wanaungua
Watu wengi ambao huota jua hawajipaki mafuta ya kutosha ya kuzuia miale ya jua kama inavyopendekezwa katika maagizo yaliyo kwenye pakiti ya bidhaa hiyo, laripoti jarida Medical Journal of Australia. Dakt. Stephen Taylor anasema kwamba “watu wengi hujipaka thuluthi moja au hata robo tu ya kiasi cha mafuta kinachopendekezwa.” Hivyo basi, mtu anahitaji kujipaka mafuta mengi kadiri gani ili kuzuia miale ya jua? Katika kitabu Archives of Dermatology, Dakt. Jeffrey Schneider anapendekeza kupima mafuta kwa kutumia kijiko cha chai. Mtu mzima mwenye umbo la wastani anapaswa kujipaka angalau nusu kijiko cha mafuta hayo katika kila mojawapo ya sehemu hizi: kichwa, shingo, na mikono. Pia anapaswa kujipaka zaidi ya kijiko kimoja cha mafuta hayo kifuani, mgongoni, na miguuni. “Kujipaka kiasi kinachofaa cha mafuta ya kuzuia miale ya jua humzuia mtu asiunguzwe na jua kuliko ilivyo anapojipaka kiasi kidogo tu cha mafuta yanayozuia miale mingi zaidi,” anasema Schneider.
Bingwa wa Kuruka
Gazeti The Times la London linaripoti hivi: “Kuna bingwa mpya wa kuruka miongoni mwa wadudu.” Mdudu mdogo anayeitwa froghopper, anaweza kuruka juu kufikia sentimeta 70. Hilo linalingana na mtu anayeruka jengo lenye urefu wa meta 180! Akitumia kamera inayopiga picha kwa kasi sana, Profesa Malcolm Burrows wa Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza, aligundua kwamba misuli ya miguu ya nyuma ya mdudu huyo ni kama chombo cha kurushia mawe, kwani humrusha kwa nguvu sana. Burrows anakadiria kwamba mdudu huyo anaporuka hushinda nguvu za uvutano zinazozidi zile za dunia kwa mara 400, “ambazo ni mara 130 ya zile ambazo chombo cha anga hukabili kinaporushwa angani,” lasema gazeti hilo.
Unahitaji Usingizi Kadiri Gani?
Gazeti USA Today linaripoti hivi: “Watu wazima wanaolala usingizi kwa saa 7 kila usiku katikati ya juma huenda wasife katika kipindi cha miaka 10 ijayo wakilinganishwa na wale wanaolala kwa muda mrefu zaidi.” Watafiti nchini Japani waliwafanyia utafiti watu wazima zaidi ya 104,000 kwa miaka kumi hivi, na kuchunguza kwa makini mazoea yao ya kulala, afya yao ya kimwili na ya kiakili, na pia maisha yao. Wanasayansi hao waligundua kwamba “kulala kwa muda mfupi, hata kwa saa nne tu usiku mmoja, hakuongezi sana idadi ya vifo miongoni mwa wanaume, na kwamba wanawake waliolala kwa muda usiozidi saa nne ndio tu waliokabili uwezekano wa kufa.” Jambo hilo huungwa mkono na matokeo yaliyochapishwa ya miradi miwili muhimu ya utafiti na miradi mingine mingi midogo. Hata hivyo, wataalamu hao waligundua kwamba “watu wanaolala kwa saa nne hadi tano na nusu hawakufanya vizuri katika majaribio ya kupima uwezo wa kukumbuka, kufikiri, na kukaza fikira.” Daktari wa magonjwa ya akili, aliye pia mtafiti wa masuala yanayohusu kulala, Daniel Kripke, anasema: “Watu wanapaswa kulala kwa muda utakaowawezesha kupumzika vya kutosha.”
Vijana Wengi Watakabili Magumu
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya State of the World Population, ya mwaka wa 2003, ilisema hivi: “Karibu asilimia 50 ya watu wote wana umri usiozidi miaka 25, na hiyo ni idadi kubwa zaidi ya vijana katika historia.” Vijana hawa watakabili nini? Kulingana na gazeti The Independent la London, “Dakt. Thoraya Obaid, ambaye ni msimamizi wa Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa, alisema kwamba kizazi kikubwa zaidi cha vijana katika historia kinakabili hatari kubwa sana ya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa, kufunga ndoa na kupata mimba wakiwa wachanga, kuvunjika kwa familia, matumizi ya dawa za kulevya, jeuri, na kutumiwa katika biashara ya ngono.” Kwa mfano, asilimia hamsini ya watu wote wanaoambukizwa virusi vya UKIMWI wana umri wa miaka 15 hadi 24. Inakadiriwa kwamba katika kila sekunde 14, kijana mmoja anayebalehe huambukizwa virusi vya UKIMWI. Uwezekano wa vijana kufa wakati wa kujifungua unazidi mara mbili ule wa watu wazima. Na inasemekana kwamba kila mwaka vijana wapatao milioni 4, huingia katika biashara ya ngono.
Wanawake Wanaopata Watoto Wakiwa na Miaka 40
Umri wa wastani wa kupata mtoto wa kwanza miongoni mwa wanawake nchini Italia unaongezeka. Katika mwaka wa 1980, wanawake 74.3 kati ya wanawake 1000 nchini Italia walipata mtoto wakiwa na umri wa miaka 20, lakini katika mwaka wa 2000 idadi hiyo ilikuwa imepungua kufikia wanawake 20.7 kati ya 1000. Katika kipindi hichohicho, idadi ya wanawake wenye umri wa miaka 40 waliopata watoto ilipanda kutoka wanawake 12.2 hadi 16.1 kati ya kila wanawake 1000. Takwimu hizo ambazo zilitolewa na Taasisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Italia na kuchapishwa na Corriere della Sera huonyesha kwamba kwa kawaida watu husubiri sana kabla ya kupata mtoto wao wa kwanza. Kulingana na taasisi hiyo, “watu wanasubiri ili wapate kazi inayofaa na kuwa na maisha mazuri, lakini pia wanafanya hivyo ili kuendelea kuwa huru. Vyovyote vile, kupata mtoto huonwa kuwa wajibu mzito na kizuizi.”
Wanaacha Kuungama
Mtaalamu wa masuala ya jamii wa Chuo Kikuu cha Katoliki, William D’Antonio, anasema hivi: “Siku hizi, idadi ya watu wanaokuja kwa ukawaida ili kuungama faraghani imepungua kufikia chini ya asilimia 25.” Gazeti The Miami Herald linaripoti hivi: “Wataalamu wanasema kwamba sababu kubwa ya jambo hilo ni maoni mapya ya watu kuhusu dhambi.” Kasisi Monsignor Thomas Kane wa Kanisa Katoliki la St. Patrick la Rockville, Maryland, aliye na umri wa miaka 76, anasema hivi: “Maoni ya kwamba viwango vya adili hutegemea mtu binafsi yameenea sana. . . . Watu hawaoni jambo lolote kuwa baya. Wanaona kwamba ikiwa wana sababu nzuri ya kufanya jambo fulani, basi kulifanya si dhambi.” Pia gazeti hilo linasema kwamba “idadi ya Wakatoliki wanaopinga msimamo wa kanisa kuhusu kupanga uzazi, ngono kati ya watu wa jinsia moja, na talaka imeongezeka.” Hivyo, “Wakatoliki hutegemea dhamiri zao ili kuamua ikiwa wamefanya dhambi.”
Ukosefu wa Maji Unatarajiwa
Koichiro Matsuura, msimamizi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, anasema hivi: “Wastani wa kiasi cha maji ambacho kila mtu hupata duniani kinatazamiwa kupungua kwa thuluthi moja katika kipindi cha miaka 20 ijayo.” Kiasi cha maji hakitapungua kwa sababu tu ya ongezeko la idadi ya watu, uchafuzi, na sababu za mazingira. Tunakabili janga hilo kwa sababu “viongozi wa kisiasa wameshindwa kubadili hali hiyo,” lasema UNESCOPRESS. Ripoti yenye kichwa Water for People, Water for Life, iliyotolewa na washiriki 23 wa Umoja wa Mataifa inasema: “Kwa kuwa viongozi wameshindwa kufanya lolote, na watu hawafahamu vizuri tatizo wanalokabili, hatua za kurekebisha hali hiyo hazijachukuliwa.” Bw. Matsuura anasema hivi: “Hakuna eneo lolote litakaloepuka janga hilo.”
Tahadhari kwa Wanawake Wajawazito
Gazeti FDA Consumer linaripoti kwamba wanawake nchini Marekani wanatayarisha “video za kumbukumbu” kwa ajili ya watoto wao ambao bado hawajazaliwa kwa kutumia tekinolojia ya hali ya juu. Tekinolojia hiyo inahusisha kutumia mawimbi ya sauti yanayopenya hadi kwenye viungo vilivyo ndani ya mwili na kutokeza picha kwenye kompyuta. Kisha picha hizo zinahifadhiwa katika kanda za video. Biashara nyingi za kupiga picha hizo zimeanzishwa katika maduka ya maeneo mengi nchini. Hata hivyo, huenda watu wanaopiga picha hizo wasiwe na ujuzi wala kibali cha kufanya kazi hiyo kama wataalamu wa kupiga picha hizo hospitalini. Hivyo, huenda wakatumia mashine za kupiga picha kwa muda mrefu au wakaziendesha kwa vipimo vya juu sana kuliko vile vinavyotumiwa na wataalamu. Gazeti FDA Consumer linasema kwamba ‘kuwapiga picha watoto ambao bado hawajazaliwa bila sababu yoyote ya kitiba ni jambo hatari.’